domingo, 3 de outubro de 2021

“BILA UAMINIFU HAKUNA FURAHA”

 

Kutafakari kuhusu Mw 2: 18-24 Mk 10: 2-16


 

    Yesu alikuwa akiwafundisha watu kama ilivyokuwa desturi yake. Ghafla baadhi ya Mafarisayo walimwendea wakimjaribu. Jambo lilikuwa kuhusu talaka likidhihirisha mtazamo wao kuhusu ndoa na familia. Yesu alisahihisha mtazamo huo, akiwakumbusha mpango wa kiasili wa Mungu kwa mwanamume na mwanamke ambao tumesoma katika somo la kwanza.

    Baadaye alipoingia nyumbani aliendelea kuongea na wanafunzi wake kwa kina kuhusu uzinzi akiuweka kwa uhusiano na talaka. Hatimaye, alionyesha tabia ya upendo kwa watoto wadogo walio waathirika wa tabia mbaya ya wazima wazima katika ndoa na familia. Yesu anajitambulisha na watoto anawakumbatia anawabariki anawalinda na kuwaweka kama mfano na kipimo ili kumkaribisha na kuingia katika ufalme wake. Hao wanastahili kuheshimiwa na kuthaminiwa ili waweze kukua kwa usalama na furaha.

    Baadhi ya Mafarisayo wanatumia sheria ya Musa kumjaribu Yesu. Kulingana na mawazo yao, Sheria hiyo inaruhusu talaka, lakini Yesu anaikataa hayo kwa sababu sio mpango wa Mungu na tena hali ya mwanamke ilikuwa ngumu sana kwa sababu daima alionewa na daima alitegemea huruma tu ya mwanamume. Kulingana na Kitabu cha Kumbukumbu la Sheria, sura 24, mwanamume aliweza kumpatia mkewe talaka ikiwa hakupendezwa naye “kwa sababu ameona kwake kitu kisichofaa”. Mwanamke alikuwa na nafasi chache za kutoa talaka kwa mmewe, mfano mwanamume akiugua ukoma. Mbele ya hayo Yesu aliwasaidia kufikiri vizuri kwa sababu Sheria zimewekwa kwa manufaa ya watu na si watu kwa ajili ya sheria.

    Kulingana na mpango wa Mungu uliofunuliwa na Yesu, wote mwanamume na mwanamke wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu naye ameweka ndani yao upendo unaowafanya watamaniane na hatimaye kuwaacha wazazi wao, kuungana na kuwa mwili mmoja. Jambo hili linaonyesha kuwa mme hana haki ya kuamua atakavyo kwa mkewe, mfano kumwacha mke wake kwa muda wowote anaotaka.

    Umoja wao ni mtakatifu naye Mungu mwenyewe akiutaka na kuuweka. Mwendeleo ama kupasuka kwa umoja huu haupatikani kwa hukumu ya kibinadamu. Inamaanisha kuwa hawawezi kuachana au kutenganishwa. Lengo kuu la Yesu, ni kweka tena hali ya ndoa isio na mwisho na hivyo kukarabati nafasi ya mwanamke kwa uhusiano na mmewe uliyoharibiwa na sheria. Kulingana na Yesu Mwanamke ana haki kama mwanamume naye anastahili kuheshimiwa kama sura na mfano wa Mungu. Nia ya Mungu ni kuwa mume na mke waendelee kukua katika upendo na kupata uzima wa milele.

    Tamani ya kibinadamu ya kupenda na kupendwa ni maana ya uzoefu wa ndoa na wa familia. Familia ni msingi wa uzoefu wa kibinadamu na yoyote ambayo ni dhidi ya kanuni hii ni marufuku katika biblia. Kwa hiyo “Usizini” ni moja miongoni mwa Amri Kumi. Kwa nini uzinzi hutishia familia? Uzinzi unaweza kuharibu familia kwa sababu pamoja na uwezekano wa kusababisha ujauzito na kuzaliwa kwa mtoto bila mpango kuna pia madhara ya kutisha kwa ndoa, kama hisia ya usaliti na upotevu wa itibari. Kwa kifupi uzinzi unamaanisha maisha ya ulaghai.   

    Maana ya Amri “Usizini” ni ulinzi wa familia. Kwa nini familia ni muhimu sana? Kwa sababu pasipo familia uimara wa jamii hauwezekani; tena kwa sababu bila familia mawasiliano ya thamani ya jamii kizazi kwa kizazi hayawezekani. Zaidi ya hayo uhusiano kati ya wazazi na watoto unawafanya kuwajibika na kukomaa zaidi. Familia inayaridhisha mahitaji ya hisia na fizikia/mwili, kuwapa watoto utoto salama na imara. Yesu alijitambulisha na watoto na kuwajulisha kama mfano wa kukaribisha mafundisho yake ili tuweze kuingia katika ufalme wake na kupata furaha kubwa. Kwa upendo na wema mkubwa alikubali kuwa mmoja wetu na kuishi hali ya familia akituletea furaha kubwa vile vile tunaalikwa kupendana sisi kwa sisi na kupatikana kwa kutumikia wanaoishi pamoja nasi ili tuone furaha kubwa na kupata kushiriki katika furaha yake kamili. Familia zetu iweze kukuta njia kamili ya kuishi vizuri kwa kutambua haja ya kuishi kwa uaminifu. “Bila uaminifu hakuna furaha.


Fr Ndega

Nenhum comentário: