sexta-feira, 30 de agosto de 2019

MAANA YA KUWA MWENYE HERI WA KWELI



Kutafakari kutoka Luka 14,1.7-14



       Yesu alialikwa kula chakula nyumbani mwa Mfarisayo mmoja na, kwanza kabisa, yeye alisababisha usumbufu kwa sababu alimponya mtu mmoja siku ya Sabato. Sheria ya Wayahudi inakataza hali hii, lakini Yesu anapendelea kuwatunza watu kuliko kuifuata sheria ambayo haikufuata nia ya Mungu ya asili. Akitarajia waweze kufikiri kama yeye aliwauliza swali: “Je, ni halali au la kumponya mtu siku ya Sabato?” Lakini walinyamaza. Tukumbuke kwamba Mafarisayo na Waandishi waliondoa maana ya kinabii ya sheria, wakitafsiri kulingana na mawazo yao ya upungufu. Hao wanapenda sana kujiinua na kupendezwa na watu. Mara nyingi Yesu alipokutana nao hakufikia mafanikio kuhusu mapendekezo yake ya maisha mapya kwa sababu hao ni wanafiki na kupendelea kumjaribu Yesu kuliko kubadilisha mawazo yao kulingana na matarajio yake. Kwa hivyo mara nyingi mkutano wa Yesu nao ni maana ya mapambano.

        Yesu yupo karamuni. Injili ya Luka inaonyesha kwamba kushiriki katika milo mbalimbali kulikuwa muhimu sana kwa Yesu aliyetumia vipindi hivi kama nafasi ya kuwafundisha watu. Karamu miongoni mwa Wayahudi inathaminiwa sana. Pamoja na maana ya uzoefu wa familia, kielelezo cha urafiki, mshikamano na hamu ya kukuwa pamoja, karamu pia ni mfano wa uhusiano wa upendo kati ya Mungu na watu wake (Hos 2:1-23, Isa 54:4-8, Eze 16:7-8). Katika mafundisho ya Agano la Kale, kushiriki katika Ufalme wa Mungu, mara nyingi hulinganishwa na kushiriki katika karamu (Isa 34:5-7, Zek 9:15,1 Nya 12:38, Zek 14:15-24). “Karamu za namna hiyo mara nyingi zilikuwa na ujumbe wa kimasiha. Zilisherehekea ushindi wa Mungu dhidi ya nguvu za uovu (Isa 25: 6-8), zikaimarisha uhusiano kati ya Mungu na watu wake, na kuwaunganisha watu kati yao.” Huu ni kweli, mfano kwenye karamu ya arusi. “Upendo wa Mungu ni kama ule wa Bwana arusi, jinsi alivyolipenda na kulichagua Taifa la Israeli kama mali yake mwenyewe. Wakristo wa kwanza, walifikiria pia juu ya uhusiano wao na Kristo kama mfano (Yoh 3:39, 2Kor 11:2, Efe 5:23-32).”

       Basi, katika injili ya leo, Yesu alishangaa kwa sababu ya mashindano ya watu kwa ajili ya kuchukua mahali pa kwanza katika karamu naye aliwapendekezea tabia tofauti. Mtu akipendelea kuwa wa mwisho, alichagua kuwa mtumishi kama vile Kristo aliyeja sio kutumikiwa bali kutumikia.  Katika jamii, kutafuta mahali pa kwanza, msimamo, upendeleo na umaarufu ni hali ya kawaida inayosababisha mapambano, chuki na ukatili kati ya watu. Hata katika Kanisa na jumuiya zetu tunaweza kukuta hali sawasawa na hii. Yesu alikwisha ameonya kuhusu hatari za hali hii na kufundisha unyenyekevu kama njia kamili. Unyenyekevu ni fadhila ambayo inampendeza Mungu na watu. Kuwa mnyenyekevu ni kuchukua hali ya udhaifu ya kibinafsi kwa kushinda mwelekeo wa kujiona mwema kuliko wengine. Inamaanisha kutumia nguvu zote za kibinafsi ili kuwatumikia wengine kwa ukarimu na upendo hasa wakiwa ni maskini na walio na shida ya kimwili ambao hawana cha kutulipa. Hii ni kipimo cha furaha ya kweli kwetu. Hii ni njia ya kuonyesha kwamba upendo wa Mungu unatolewa kwa hiari kwa ajili ya watu wote. Katika karamu ya arusi mbinguni, yeye atawakaribisha wale wanaomwelekea kupitia matendo ya upendo.

       Lengo la Yesu ni kuzaa ubinadamu mpya na aina mpya ya uhusiano miongoni mwa watu. Msingi wa ubinadamu mpya ni unyenyekevu na upendo. Thamani hizi zinapaswa kusaidiwa zaidi miongoni mwetu. Kupitia utumishi wa kindugu na wa kinyenyekevu tunaweza kufikia lengo la Yesu ambaye ana mawazo tofauti na yale ya jamii. Kwa Yesu, mtu ni mkuu ikiwa yeye ni mdogo; tena mtu ni wa kwanza ikiwa yeye ni wa mwisho; pia mtu anakwezwa ikiwa yeye anajishusha. Katika jumuiya zetu za wafuasi wa Yesu muhimu ni kutumikia wenzetu kama Mwalimu Yesu alivyo. Yeye anatuhakikishia kwamba yoyote tunayofanya kwa ajili ya walio na shida yatasahauliwa na Mungu. Maisha yake ya mtumishi ni kipimo kwetu. Hatuhitaji mahali pa kwanza, bali kutumikia kwanza kwa unyenyekevu na ukarimu. Tujifunze kutoka kwa Kristo aliyefahamika kama Mtumishi wa Bwana kwa namna ya kipekee ili utumishi wetu uwe bila unafiki na kuweze kumpendeza Mungu.

Fr Ndega  

domingo, 25 de agosto de 2019

KATIKA UFALME WALIO WA MWISHO WATAKUWA WA KWANZA



Kutafakari kuhusu Lk 13, 22-30



    Wakati wa safari ya kwenda Yerusalemu, Yesu alitumia nafasi ya kuwafundisha wanafunzi wake hasa kuhusu masharti ya kuingia katika ufalme wa mbinguni. Kwanza kabisa haitoshi kuwa wanafunzi wake ili kupata wokovu. Hivyo, aliwapendekezea mlango mwembamba kama changamoto. Ikiwa Yesu anajulisha mlango mwembamba ni kwa sababu pia kuna mlango mpana.

     Wakati Mt. Yohane Paulo wa II alipoongea na vijana katika mwaka wa 1993, alitofautisha vizuri njia hizi mbili, akisema: “kataeni barabara rahisi: barabara ya anasa, uhalifu, kudharau mazuri, na kukwepa wajibu. Ulevi na matumizi ya madawa ya kulevya na uasherati visiwe na nafasi katika maisha yenu. Pitieni mlango mwembamba. Chagua barabara ielekeayo kwenye uzima wa milele na furaha pamoja na Mungu.” Katika kifungu kingine Yesu alisema kwamba mlango mwembamba ni njia ambayo inaongoza kwenye uzima na wachache tu wanaoweza kuigundua njia hiyo. “Huu ni mlango wa uvumilivu, busara, kujitoa, ukarimu, wema, shukrani na kazi”. Kuhusu mlango mpana, hii ni njia rahisi inayoongoza kwenye maangamizi na waendao njia hiyo ni wengi. Basi, ili wanafunzi wa Yesu waweze kupata mafanikio katika safari yao wapaswa kupitia mlango mwembamba.   

     Katika mazingira yetu mlango mwembamba ni ishara ya juhudi yetu ya kushinda mwelekeo mbaya wa maisha yetu na kuwatendea watu mema. Katika mwendo huu ndio sisi wa kwanza wa kupata mafanikio ama bahati mbaya, kwa sababu lile tunalofanya kwa ajili ya wengine linasababisha hali nzuri ama mbaya kwetu pia. Hadithi fulani inatusaidia kuelewa vizuri hali hii. “Siku moja mwandishi wa habari alimhoji mwenye shamba ambaye ameshinda mara ya tano mashindano kuhusu mahindi mazuri zaidi katika eneo hilo. Mwandishi alimwuliza swali akisema, “unapataje kuzaa mahindi bora kuliko wengine?” Mwenye shamba alijibu, mwendo huu ni rahisi sana; nina mazoea ya kushiriki mbegu zangu nzuri na majirani wangu.” Mwandishi aliendelea kwa swali akisema, “Kwa nini unashiriki mbegu zako nzuri na majirani wako ikiwa hao wanashindana pia katika mashindano haya pamoja?” “kwa sababu ni upepo ambao unasambaza poleni ya mahindi na tena ni upepo ambao unaweka poleni mashambani na unafanya mbegu zikue. Ikiwa majirani wangu watakuwa na mahindi mabaya, upepo utasambaza poleni mbaya shambani kwangu nayo mahindi yangu yatakua mbaya. Basi ili mahindi yangu yawe mazuri ninapaswa kuwasaidia majirani wangu wote ili wawe na mbegu nzuri.”

     Basi, lile zuri ambalo tunatarajia kwa maisha yetu tunapaswa kusaidia kwa ajili ya wengine. Katika mwendo huu hatuwezi kuitafuta furaha kwa njia ya ubinafsi. Ikiwa tunataka kuwa wenye furaha, tunapaswa kuisaidia hali hii nzuri kwa wale wanaoishi karibu nasi nao wako na shida sawasawa nasi. Tunapaswa kushinda mwelekeo wa jamii wa kufikiria wengine kama washindani nasi. Wengine sio washindani, bali ni ndugu. Kujaribu kupata upendeleo tukiwavuruga wengine ni udhalimu na kutuacha mbali sana na pendekezo la Yesu. Ikiwa tuko mbali na pendekezo la Yesu, matokeo yatakuwa mbali sana na yale tuliyotarajia kwa maisha yetu. Tunaweza kuongea vizuri sana kuhusu Yesu ili kuonyesha kwamba tunamjua Yeye na Biblia pia. Tunaweza hata kufikiri kwamba kuongea bora kuliko wengine kunatuhakikishia faida ili tupokee baadhi ya tuzo kutoka kwa Mungu. Lakini, kulingana na andiko hili, maneno hayatoshi kuingia katika ufalme wa Mungu. Wokovu si astahili yetu, lakini hii ni zawadi ya ukarimu wa Mungu.

        Je, inawezekanaje tuseme kwamba tunamjua Yesu naye aseme kwamba hatujui sisi?” Hii ni kwa sababu katika biblia kitenzi kujua kinamaanisha uhusiano wa ndani, uzoefu wa kina ambao ni muhimu sana katika safari yetu ya wanafunzi wa Yesu. Ikiwa yeye anasema kwamba hatujui sisi ni kwa sababu sisi hatumjui yeye. Katika mwendo huu hakuna makubaliano kati yetu na pendekezo lake, hakuna utambulisho. Hatuwezi kuwa wanafunzi wa Yeu kupitia maneno peke yake. Ushuhuda wa maisha unathamini zaidi kuliko maneno. Tukijifikiria bora kuliko wengine hatuuhakikishii wokovu. Kila kitu tunachofanya kinasababisha matokeo makubwa kwetu na katika hali iliyo kandokando yetu. Kwa maneno mengine, kufikia mafanikio ama bahati mbaya kwa maisha yetu kunatutegemea sisi wenyewe; huu ni uamuzi wetu. Kwa upande wa Mungu tunaumbwa ili kushiriki katika maisha yake, yaani ili kuokokewa. Neema ya Mungu ituongoze ili tuweze kufanya mapenzi yake na kupata uhai.

Fr Ndega