terça-feira, 4 de outubro de 2016

UTUMISHI WETU NI UTHIBITISHO WA IMANI YETU


Kutafakari kuhusu Lk 17, 5-10

     “Mwenye  haki ataishi kwa imani yake.” Tafakari yetu inalenga imani kama zawadi muhimu sana iliyo njia maalum ya kuishi nayo inatoa maana kwa maisha. Imani ni msaada kubwa katika majibu yetu kwa upendo wa Mungu. Hii ni zawadi inayochochea karama ya Mungu iliyo ndani yetu kupitia Roho Mtakatifu. Wakati wanafunzi wa Yesu walipomwomba wakisema, “Ongeza Imani yetu”, walionyesha tabia ya unyenyekevu wakitambua udhaifu wao mbele ya changamoto za kazi. Kwa dua hii walitaka kumaanisha kwamba walikuwako tayari kwa kila kitu kwa ajili ya Yesu, lakini walihitaji msaada wake. Kwa maneno mengine, ilikuwa tangazo la imani kuutambua uwezo wa Yesu kwa ajili ya imani yao haba. Jibu la Yesu linadhihirisha kwamba wanafunzi hawakuwa na imani jinsi walivyodhani walicho nacho. Jibu la Yesu linawasaidia kufahamu umuhimu wa Imani na lengo lake la kweli. Kulingana na Yesu imani inauhusu utumishi na kuthibitisha utambulisho wa wafuasi na mwalimu wao. Yesu hakujibu moja kwa moja, bali alipendelea kuonyesha kwamba imani sio jambo lolote. Haitoshi kusema “Nasadiki” ama “nakusadiki”. Ni kama ilivyotokea katika hadithi fulani:

“Kuna mtu ambaye alikuwa anatembea kwenye njia nyembamba bila kuwa makini kutazama alipokuwa anaelekea. Ghafla aliteleza kandokando ya mtelemko wa ghafla. Alishikilia tawi la mti kwenye mtelemko. Akigundua kuwa hawezi kushikilia kwa muda mrefu aliomba msaada. Aliita: “Kama kuna mtu huko juu anisaidie?” Sauti ilimjibu: “Nipo hapa.” Aliuliza: “Wewe ni nani?” Sauti ilimjibu: “Ni mimi Bwana Yesu Kristo.” Mtu huyo alisema: “Nisaidie Bwana.” Bwana Yesu: “Unaniamini?” Mtu huyo alijibu: “Nakuamini kabisa.” Bwana Yesu akasema: “Achia tawi la mti.” Mtu huyo alishangaa: “Nini?” Bwana Yesu: “Achia tawi la mti.” Baada ya kimya cha muda mrefu mtu huyo alisema: “Hakuna mtu mwingine huko juu?” 
       Bila shaka tabia ya mtu huyo siyo imani kwa sababu inakosa muhimu sana iliyo kuacha kitu ambacho kinaonekana kuwa usalama na kujiruhusu kuongozwa na Yule anayejua analofanya. Imani ya kweli inadai tabia ya kujisalimisha, kulingana na hadithi nyingine: “Siku moja ajali ilitokea katika nyumba ya ghorofa kubwa nayo nyumba hii ilianza kuwaka moto. Watu wote walipaswa kutoka nje. Familia moja ilipata kutoka, lakini mtoto mdogo wake alibaki nyuma. Wazazi hawakuweza kurudi tena ili wachukue mtoto kwa sababu moto ilikuwa kali sana. Mtoto alikaribia dirisha moja katika sehemu ya juu ya nyumba akilia sana. Yeye hakuweza kumwona yeyote nje ya nyumba kwa sababu ya moshi nyingi. Lakini, kutoka nje baba ya mtoto huyo aliyepata kumwona mtoto, alimwambia, ‘mwanangu, utupe chini kutoka huko kwa maana mimi nitakuchukua mikononi mwangu.’ Ingawa mtoto hakupata kumwona babaye, akaisikiliza sauti yake na kuamua kujitupa. Kisha, mara babaye alipata kumchukua mwanae mikononi mwake, akimwokoa.”
      Katika hadithi hii, kwanza kabisa kuna uhusiano wa kifamilia, yaani, baba na mtoto. Baba anatumia nafasi ya kusema kitu, yaani, ‘mwanangu, utupe chini kutoka huko kwa maana mimi nitakuchukua mikononi mwangu.’ Anasema hayo kwa sababu anajua mwanae na tena anajua kwamba huyo mwanae anahitaji msaada wake. Anaposema hayo, anahakikisha uwepo na utunzaji wake. Basi, hali ya imani inafanana na hivi. Hii ni zawadi iliyotoka kwa Mungu na inatenda ndani yetu ili lile ambalo lisilowezekana libadilishwe kuwa linalowezekana. Imani hii hata ndogo inaweza kushinda vikwazo vikubwa. Tukumbuke yale ambayo Yesu aliwaambia wanafunzi wake waliochanganyikiwa, yaani, “Kama mngekuwa na imani kiasi cha chembe ya haradali, mngeuambia mkuyu huu, Ng’oka, ukapandwe baharini, nao ungewatii”. 
        Imani hii tulipokea katika ubatizo kama mbegu ambayo inahitaji kuchipua, kukua na kuboresha. Tunahitaji kuiimarisha zawadi hii kwa sababu ni maonyesho ya utambulisho wetu na, kupitia ushuhuda wa imani halisi tunaweza kuwaimarisha wengine katika safari yao. Mt. Yohana Calabria asema: imani yetu iwe halisi na ya kweli; haiwezekani kuwa na tofauti kati ya imani tunayoamini na ile tunayoishi.” Si lazima imani kubwa; kweli imani yetu inapaswa kuwa hai na ufanisi. Kuhusu hayo, mtume Yakobo asema, “mwonyeshe imani yenu bila matendo nami nitaionyesha imani yangu kwa matendo yangu. Imani bila matendo imekufa.”  Katika sehemu nyingi za injili tunakuta mifano ya Imani hai na ufanisi, yaani, wakati Yesu alipokutana na mtu aliye na aina hii ya imani na mtu huyo alimwomba ili amponye, Yesu asema, “imani yako imekuokoa”.
        Kulingana na hadithi, ingawa mtoto hakupata kumwona babaye, lakini akaisikiliza sauti yake na kuamua kujitupa, vivyo hivyo sisi tunaalikwa kuchukua uamuzi wa kujisalimisha. Hii ndiyo imani. Mungu ambaye tunasadiki yu kama vile yule baba ambaye alipata kumchukua mwanae mikononi mwake, akimwokoa.” Tumeipewa imani na kupitia zawadi hii tunaweza kujibu kwa mwaliko wa Mungu. Bila shaka jibu ambalo yeye anatarajia ni kwamba tuweze kujikabidhi mikononi mwake kama ilivyotokea kwa Ibrahimu na kwa wenye haki wengine wa Biblia. Mfano, kulingana na uzoefu wa Ibrahimu, haitoshi kusema “nakuamini”; ni lazima kutii, kuruhusu kuongozwa na Mungu hadi palipompendeza. Kuhusu uzoefu huu wa Ibrahimu, waraka wa Waebrania unatuletea ushuhuda mzuri sana, yaani, “Kwa njia ya imani Ibrahimu alitii alipoitwa ahamie nchi ambayo angepewa kuwa mali yake. Alihama bila kujua anakokwenda” (Waeb 11:8).

       Kumwachia Mungu ni kuwa na imani ya Ibrahimu. Ni imani ya kumwacha Mungu aitwe  Mungu aliye Baba na Mtoaji. “Matatizo yote yapaswa kufikiriwa na kusomeka kwa maelewano na ubaba wake” (Mt. Yohane Calabria). Huyo, yaani, Mt. Yohane Calabria, anafahamiwa kama Mtakatifu wa Riziki kwa maana ya tabia ya imani ya kweli na kujisalimisha kwake katika Riziki ya Mungu. Kulingana naye, Riziki ya Mungu ni kama Mama ambaye anatenda mambo yote kwa wema wetu. Tunapaswa kujiona kubebwa mikononi mwake wa mama.” Kuhusu hayo, anaendelea kwa kusema, “Kama sisi tuko mikononi mwa Mungu, tuko mikononi pazuri.” Je, tabia yetu ni kama ile ya mtoto mdogo ambaye anaruhusu kuongozwa kwa sababu ana uhakika kuamba mama au baba yake anajua lile analofanya? Yeyote ambaye anaamini anaweza kujisalimisha mikononi mwa Mungu Baba kama Mt. Calabria alivyo.


     Ikiwa tunajiita Wakristo, ni kwa sababu tunajua kwamba sisi ni washiriki wa imani ya kanisa lilipo kwa karne nyingi. Wakati tunapotumia imani yetu kama jibu kwa mwaliko wa Mungu, hatuyategemei mawazo yetu peke yake, bali tunaitegemea imani ya watu wote wa Mungu, yaani, imani ambayo inawahusu Ibrahimu, Musa, manabii wa Israeli, mitume na wanafunzi wengine wengi wa Yesu Kristo, Mt. Yohana Calabria na kadhalika. Imani yangu ya kibinafsi ni urithi wa imani ya jumuiya ya kanisa. Kutokuwepo kwangu katika jumuiya ama kikundi kunasababisha shida kwangu na kwa kikundi. Basi imani inadhihirisha utambulisho wetu; hii ni njia yetu wenyewe ya kuishi na kutumikia. Imani yetu inauhusu utumishi ambao tunaweza kufanya. Kwa kutumikia kwa kweli tunataka kumwomba Bwana Yesu kama wanafunzi wa kwanza alivyo, tukisema, “Bwana Mkubwa, ongeza imani yetu!”

Fr Ndega