sexta-feira, 8 de julho de 2016

JIRANI YANGU NI NANI?


Kutafakari kuhusu Lk 10, 25-37


      Katika usomaji wake, mtaalamu fulani wa Biblia alifanya uhusiano wa ajabu kati ya mikutano ya maskini na Yesu na ile mikutano yake na matajiri. Kulingana na mtaalamu huyo, Maskini na wasio na nguvu walipokutana na Yesu wanalenga msaada kutatua shida za kimwili kwa sababu walijihisi kudharauliwa na kutengwa na wengine; hao wanataka kushiriki kamili katika maisha ya kijamii pamoja na wenzao. Kuhusu mikutano ya Yesu na tajiri na wenye nguvu, hali ni tofauti kabisa kwa sababu hao wanamiliki mali ya kutosha duniani, wanajiona watawala wa dunia na kutaka kutawala katika uzima wa milele pia. Mbele ya hayo Yesu anapendekeza kujinyima kama ilivyotokea kwa kijana tajiri aliyependelea kuenda zake kwa huzuni kuliko kukubali pendekezo la Yesu la kujinyima alicho nacho kwa ajili ya maskini – Mt 19: 16-22.

        Katika injili ya siku ya leo mwanasheria alimwendea Yesu na alimwuliza maswali mawili, yaani, la kwanza “nifanye nini ili niurithi uzima wa milele?”; na la pili, “Jirani yangu ni nani?” kuhusu swali la kwanza Yesu alimsaidia kugundua tena umuhimu wa sheria, yaani, “kumpenda Mungu na kumpenda jirani”. Amri ya Kumpenda Mungu tunapata katika kitabu cha Kumbukumbu la Sheria (6:5) na ya Kumpenda jirani kunapatikana katika kitabu cha Walawi (19:18). Ikiwa Yesu alimwambia mwanasheria kwamba yatosha kutenda hivyo ili apate uzima wa milele ni kwa sababu “Torati yaonyesha njia ya uzima  wa milele ikiwa mtu anampenda Mungu na jirani yake.” Katika Agano la Kale Mungu alianzisha Agano na Watu wa Israeli akiwafanya wana wake. Kama ishara halisi ya Agano hili tuko na Amri kumi ambazo zinalenga ushusiano mwema na Mungu na jirani. Lakini, kulingana na mawazo yao ya kiyahudi, jirani siyo yule ambaye anaishi karibu nao bali yule ambaye ni karibu katika uhusiano wa damu. Basi, wageni hawawezi kuwa jirani kwao. Hivi uelewa huu uliwazuia kuwa na uhusiano mwema hasa na Wasamaria waliofahamiwa kama maadui wao.

       Kupitia swali la pili, yaani “Jirani yangu ni nani?” mwanasheria alitarajia Yesu akubaliane na mawazo haya ya kivuo. Lakini Yesu alisimulia mfano wa Msamaria Mwema. Kulingana na mfano huu tuko na kuhani, Mlawi moja, Msamaria na yule aliyekuwa ameshambuliwa na wanyang’anyi. Wawili wa mwanzo, yaani kuhani na Mlawi, ni ishara ya wale ambao wanapaswa kuitii sheria, na kulingana na sheria hii, hawawezi kugusa ama kuguswa na “kitu kichafu”. Walitumia njia nyingine kwa sababu kuwa karibu na mtu yule aliye na haja ya msaada kungewazuia kumsifu na kumtumikia Mungu kamili. Kwa kweli wawili hawa wanapaswa kufahamu kwamba “ni jambo baya kutofanya mazuri kwa kutumia jina la Mungu au la dini”. Msamaria peke yake aliyefahamiwa kama adui wa yule aliyeanguka, alimwonea huruma, akasimama na kumsaidia. Kwa sabau ya sheria ya utakaso wawili wa kwanza walidhararau yule aliye mwenzao hata wakitotii sheria ya ujirani. Kupitia tabia yake ya huruma, “Msamaria alionyesha ujirani mwema” kwa sabau hakuhitaji kuitii sheria ya utakaso. “Msamaria mwema hakujifikiria mwenyewe, alimfikiria mwingine.” Kupitia mfano huu Yesu anaonyesha kuwa swali la msingi sio “ni nani jirani yangu,” bali ninawezaje kuwa jirani kwa mwenzangu?” Yesu anasahihisha mtazamo kuhusu jirani na kuonyesha kuwa upendo wa kweli kwa Mungu unatokea pamoja na kushiriki katika maisha ya wale anaowapenda.

             Kwa Yesu, upendo wa kweli unaonyeshwa kupitia ishara za upole na huruma. Yesu mwenyewe ni Msamaria Mwema kwa namna ya kipekee ambaye alichukua hali yetu na kuponya majeraha yetu ya dhambi. Yeye anajitambulisha na wale ambao “wameanguka kando ya njia za maisha”. Je, tunaweza kutambua uwepo wake Kristo katika watu ambao kwa kawaida tunakutana na hao ambao wanaudai msaada wetu? Kumwabudu Mungu kwa kweli kunatokea kupitia uhusiano mwema na ufanisi na wengine. Kusherehekea Ekaristi ni alama ya undugu ikiwa undugu uko miongoni mwetu. Vinginevyo sio Mwili na Damu ya Kristo tunayosherehekea. Haiwezekani kufanya uhusiano wa kweli na Mungu wakati tunapowasahau wenzetu katika mahitaji yao. Hatuwezi kuishi kwa kutofautiana kuhusu hali ya wengine kama ilivyotokea kwa Kaini, yaani “Je mimi ni mlinzi wa ndugu yangu?” (Mwanzo 4:9). Hali hii ni kutofautiana iliyo njia ya kukanusha utambulisho wetu wa wakristo. Sihitaji kujua ni nani jirani yangu ili nimpende na kumsaidia. Kumpenda jirani ni kumsaidia kushinda matokeo ya ukatili na udhalimu maishani mwake. Siku ya leo, kwa upande wetu kama wakristo, jirani ni yule ambaye tunamgundua kama aliye na haja na kuamua kuandamana naye kumhakikishia maisha kwa heshima hata wakati mwendo huu unapodai kutumia muda wetu na rasilimali zetu. Ekaristi hii itusaidie kuwa “jirani mwema”. 

Fr Ndega 
Mapitio na marekebisho: Sarah

domingo, 3 de julho de 2016

UTAYARI KWA MAMBO YOTE KWA AJILI YA UFALME WA MUNGU


Kutafakari kuhusu Lk 10: 1-12, 17-20


          Yesu alikuwa na wanafunzi wengi. Alichagua kumi na wawili kati yao ili wawe mitume, lakini alipowatuma wamtangulie katika kila mahali, aliwatuma wote, hata wasio na cheo cha mitume. Jambo hili muhimu tunakuta katika toleo la Luka peke yake. Injili zingine, yaani, Marko na Mathayo, zinataja utume wa Thenashara peke yake. Kama namba Sabini na mbili ilikuwa namba ya mataifa yaliyojulikana katika mazingira yale, hii inamaanisha kwamba mataifa yote yanaalikwa kuikaribisha na kuishuhudia habari njema ya injili na uwepo wa ufalme wa Mungu. Ushuhuda wa wanafunzi utatokea kati ya nguvu ambazo zinaupinga mpango wa Mungu unaowaletea wote maisha mapya. Basi, kutangaza ufalme wa Mungu na kuwaponya wagonjwa ni kiini cha utume wa wafuasi wa Yesu. Ili waweze kupata mafanikio katika kazi, walipaswa kumtegemea Mungu katika mambo yote kama sehemu muhimu sana kati ya mwongozo waliopewa na Yesu ulio karibu sawa na ule wa mitume Thenashara. Waliporudi kutoka kazi walimpasha Yesu habari kuhusu mafanikio yao naye Yesu aliwahakikishia kwamba maana ya mafanikio hayo hayatoki kwao, bali yatoka kwa Mungu kwa sababu utumishi wao ni ushiriki tu katika kazi zilizo za Mungu mwenyewe.

        Msingi wa namba sabini na mbili tunaweza kukuta katika vitabu viwili vya Agano la Kale, yaani, cha Hesabu na cha Kutoka. Katika kitabu cha Kutoka namba 70 inatajwa tu miongoni mwa walioalikwa kwenda milimani Sinai pamoja na Musa. Katika kitabu cha Hesabu tuko na kuwekwa kwa wazee sabini wakati Musa alipolalamika kuhusu mzigo wa kuwatunza watu wote, akisema: “Siwezi kuwatunza watu wote hawa peke yangu; hilo ni jukumu kubwa mno kwangu!... Basi, Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “wakusanyeni wazee sabini wa Israel, ambao wewe unajua wanaheshimiwa na kukubaliwa na watu kuwa viongozi... Nitashuka sehemu ya roho niliyokupa, niwape watu hao. Nao watabeba jukumu la kuwatunza watu hawa pamoja nawe (Hes 11, 14.16-117).” Pamoja na hao wazee wengine wawili ambao walikuwa wamebaki kambini walipokea pia roho na kutabiri bila kuacha (Hes 11, 26). Andiko hili linahitimika kuonyesha matarajio ya Musa kuhusu wito wa Watu wa Mungu wawe manabii. Kama andiko hili, Maandiko Matakatifu yote yanayashuhudia mahangaiko ya Mungu kuhusu maisha ya Watu wake na furaha yake ya kuwashirikisha wanadamu katika kazi ya wokovu wao wenyewe.

       Utume wa wanafunzi hawa unafanana na utume wa Yohane Mbatizaji, yaani walipaswa kutangaza ukaribu wa ufalme wa Mungu wakimtangulia Yesu ambaye alikuwapo na kutenda mema, lakini watu hawakumjua bado. Yesu akawatuma wawili wawili kwa sababu utume wa kuutangaza Ufalme wa Mungu si kazi ya mtu achukue peke yake. Ni kazi ya jumuiya nzima nayo ni lazima ichukuliwe pamoja. Yesu alisema kwamba ni muhimu kusali kwa sababu sala ni msingi wa utume na siri ya mafanikio yake. Aliushiriki uwezo wake nao pamoja na unyeti wake kuhusu hali ya mateso ya watu ili waweze kuwatumikia. Utumishi kwa watu ambao ni wa Mungu ni utumishi kwa Mungu. Kwa hivyo ni lazima kuwa macho kuepuka kuyatumia mamlaka hayo kwa njia mbaya. Ni jukumu lao kutangaza maisha kamili ya ufalme wa Mungu, lakini ikiwa watu hawalikubali pendekezo lao si jukumu lao tena. Wanafunzi wa Yesu wanapaswa kutenda kama mwalimu wao alivyo, yaani wanapaswa kuuheshimu uhuru wa watu. Habari ya ufalme inatokana na ukarimu wa Mungu nayo ni njema kwa sababu ni matokeo ya huria/hiari. 


      Sisi ni wanafunzi wapya wa Yesu na siku ya leo yeye anatarajia utayari sawa kutoka kwetu. Kwanza kabisa, tunapaswa kuwa macho kwa msukumo wa Mungu na kuzifuata nyayo za Yesu, kuchukua njia yake ya maisha, yaani njia ya unyenyekevu, na kufikiri tofauti na mwelekeo wa jamii. Kulingana naye mafanikio ya utume wetu yanawezekana ikiwa uzoefu wa kutenda pamoja unapata kushinda uzoefu wa kutenda kwa njia ya ubinafsi, kusaidiana katika jumuiya na kwa wema wa jumuiya. Tunapochukua kazi pamoja tunasaidiwa na wengine; hivi ni rahisi kufikia mafanikio yanayotarajiwa. Tunaweza kutangaza halisi ukaribu wa ufalme kupitia utumishi wetu wa ukarimu na wa hiari, kuheshimu wale wanaotenda tofauti nasi. Baadhi ya ugumu katika safari yetu tunapaswa kukabiliana kupitia roho ya sala na kujirekebisha daima. Ukarimu wetu katika safari ya wito uwe alama ya utayari wetu kwa mambo yote kwa ajili ya ufalme wa Mungu.   

Fr Ndega
Mapitio na marekebisho: Sarah