sexta-feira, 8 de julho de 2016

JIRANI YANGU NI NANI?


Kutafakari kuhusu Lk 10, 25-37


      Katika usomaji wake, mtaalamu fulani wa Biblia alifanya uhusiano wa ajabu kati ya mikutano ya maskini na Yesu na ile mikutano yake na matajiri. Kulingana na mtaalamu huyo, Maskini na wasio na nguvu walipokutana na Yesu wanalenga msaada kutatua shida za kimwili kwa sababu walijihisi kudharauliwa na kutengwa na wengine; hao wanataka kushiriki kamili katika maisha ya kijamii pamoja na wenzao. Kuhusu mikutano ya Yesu na tajiri na wenye nguvu, hali ni tofauti kabisa kwa sababu hao wanamiliki mali ya kutosha duniani, wanajiona watawala wa dunia na kutaka kutawala katika uzima wa milele pia. Mbele ya hayo Yesu anapendekeza kujinyima kama ilivyotokea kwa kijana tajiri aliyependelea kuenda zake kwa huzuni kuliko kukubali pendekezo la Yesu la kujinyima alicho nacho kwa ajili ya maskini – Mt 19: 16-22.

        Katika injili ya siku ya leo mwanasheria alimwendea Yesu na alimwuliza maswali mawili, yaani, la kwanza “nifanye nini ili niurithi uzima wa milele?”; na la pili, “Jirani yangu ni nani?” kuhusu swali la kwanza Yesu alimsaidia kugundua tena umuhimu wa sheria, yaani, “kumpenda Mungu na kumpenda jirani”. Amri ya Kumpenda Mungu tunapata katika kitabu cha Kumbukumbu la Sheria (6:5) na ya Kumpenda jirani kunapatikana katika kitabu cha Walawi (19:18). Ikiwa Yesu alimwambia mwanasheria kwamba yatosha kutenda hivyo ili apate uzima wa milele ni kwa sababu “Torati yaonyesha njia ya uzima  wa milele ikiwa mtu anampenda Mungu na jirani yake.” Katika Agano la Kale Mungu alianzisha Agano na Watu wa Israeli akiwafanya wana wake. Kama ishara halisi ya Agano hili tuko na Amri kumi ambazo zinalenga ushusiano mwema na Mungu na jirani. Lakini, kulingana na mawazo yao ya kiyahudi, jirani siyo yule ambaye anaishi karibu nao bali yule ambaye ni karibu katika uhusiano wa damu. Basi, wageni hawawezi kuwa jirani kwao. Hivi uelewa huu uliwazuia kuwa na uhusiano mwema hasa na Wasamaria waliofahamiwa kama maadui wao.

       Kupitia swali la pili, yaani “Jirani yangu ni nani?” mwanasheria alitarajia Yesu akubaliane na mawazo haya ya kivuo. Lakini Yesu alisimulia mfano wa Msamaria Mwema. Kulingana na mfano huu tuko na kuhani, Mlawi moja, Msamaria na yule aliyekuwa ameshambuliwa na wanyang’anyi. Wawili wa mwanzo, yaani kuhani na Mlawi, ni ishara ya wale ambao wanapaswa kuitii sheria, na kulingana na sheria hii, hawawezi kugusa ama kuguswa na “kitu kichafu”. Walitumia njia nyingine kwa sababu kuwa karibu na mtu yule aliye na haja ya msaada kungewazuia kumsifu na kumtumikia Mungu kamili. Kwa kweli wawili hawa wanapaswa kufahamu kwamba “ni jambo baya kutofanya mazuri kwa kutumia jina la Mungu au la dini”. Msamaria peke yake aliyefahamiwa kama adui wa yule aliyeanguka, alimwonea huruma, akasimama na kumsaidia. Kwa sabau ya sheria ya utakaso wawili wa kwanza walidhararau yule aliye mwenzao hata wakitotii sheria ya ujirani. Kupitia tabia yake ya huruma, “Msamaria alionyesha ujirani mwema” kwa sabau hakuhitaji kuitii sheria ya utakaso. “Msamaria mwema hakujifikiria mwenyewe, alimfikiria mwingine.” Kupitia mfano huu Yesu anaonyesha kuwa swali la msingi sio “ni nani jirani yangu,” bali ninawezaje kuwa jirani kwa mwenzangu?” Yesu anasahihisha mtazamo kuhusu jirani na kuonyesha kuwa upendo wa kweli kwa Mungu unatokea pamoja na kushiriki katika maisha ya wale anaowapenda.

             Kwa Yesu, upendo wa kweli unaonyeshwa kupitia ishara za upole na huruma. Yesu mwenyewe ni Msamaria Mwema kwa namna ya kipekee ambaye alichukua hali yetu na kuponya majeraha yetu ya dhambi. Yeye anajitambulisha na wale ambao “wameanguka kando ya njia za maisha”. Je, tunaweza kutambua uwepo wake Kristo katika watu ambao kwa kawaida tunakutana na hao ambao wanaudai msaada wetu? Kumwabudu Mungu kwa kweli kunatokea kupitia uhusiano mwema na ufanisi na wengine. Kusherehekea Ekaristi ni alama ya undugu ikiwa undugu uko miongoni mwetu. Vinginevyo sio Mwili na Damu ya Kristo tunayosherehekea. Haiwezekani kufanya uhusiano wa kweli na Mungu wakati tunapowasahau wenzetu katika mahitaji yao. Hatuwezi kuishi kwa kutofautiana kuhusu hali ya wengine kama ilivyotokea kwa Kaini, yaani “Je mimi ni mlinzi wa ndugu yangu?” (Mwanzo 4:9). Hali hii ni kutofautiana iliyo njia ya kukanusha utambulisho wetu wa wakristo. Sihitaji kujua ni nani jirani yangu ili nimpende na kumsaidia. Kumpenda jirani ni kumsaidia kushinda matokeo ya ukatili na udhalimu maishani mwake. Siku ya leo, kwa upande wetu kama wakristo, jirani ni yule ambaye tunamgundua kama aliye na haja na kuamua kuandamana naye kumhakikishia maisha kwa heshima hata wakati mwendo huu unapodai kutumia muda wetu na rasilimali zetu. Ekaristi hii itusaidie kuwa “jirani mwema”. 

Fr Ndega 
Mapitio na marekebisho: Sarah

Nenhum comentário: