sexta-feira, 30 de agosto de 2019

MAANA YA KUWA MWENYE HERI WA KWELI



Kutafakari kutoka Luka 14,1.7-14



       Yesu alialikwa kula chakula nyumbani mwa Mfarisayo mmoja na, kwanza kabisa, yeye alisababisha usumbufu kwa sababu alimponya mtu mmoja siku ya Sabato. Sheria ya Wayahudi inakataza hali hii, lakini Yesu anapendelea kuwatunza watu kuliko kuifuata sheria ambayo haikufuata nia ya Mungu ya asili. Akitarajia waweze kufikiri kama yeye aliwauliza swali: “Je, ni halali au la kumponya mtu siku ya Sabato?” Lakini walinyamaza. Tukumbuke kwamba Mafarisayo na Waandishi waliondoa maana ya kinabii ya sheria, wakitafsiri kulingana na mawazo yao ya upungufu. Hao wanapenda sana kujiinua na kupendezwa na watu. Mara nyingi Yesu alipokutana nao hakufikia mafanikio kuhusu mapendekezo yake ya maisha mapya kwa sababu hao ni wanafiki na kupendelea kumjaribu Yesu kuliko kubadilisha mawazo yao kulingana na matarajio yake. Kwa hivyo mara nyingi mkutano wa Yesu nao ni maana ya mapambano.

        Yesu yupo karamuni. Injili ya Luka inaonyesha kwamba kushiriki katika milo mbalimbali kulikuwa muhimu sana kwa Yesu aliyetumia vipindi hivi kama nafasi ya kuwafundisha watu. Karamu miongoni mwa Wayahudi inathaminiwa sana. Pamoja na maana ya uzoefu wa familia, kielelezo cha urafiki, mshikamano na hamu ya kukuwa pamoja, karamu pia ni mfano wa uhusiano wa upendo kati ya Mungu na watu wake (Hos 2:1-23, Isa 54:4-8, Eze 16:7-8). Katika mafundisho ya Agano la Kale, kushiriki katika Ufalme wa Mungu, mara nyingi hulinganishwa na kushiriki katika karamu (Isa 34:5-7, Zek 9:15,1 Nya 12:38, Zek 14:15-24). “Karamu za namna hiyo mara nyingi zilikuwa na ujumbe wa kimasiha. Zilisherehekea ushindi wa Mungu dhidi ya nguvu za uovu (Isa 25: 6-8), zikaimarisha uhusiano kati ya Mungu na watu wake, na kuwaunganisha watu kati yao.” Huu ni kweli, mfano kwenye karamu ya arusi. “Upendo wa Mungu ni kama ule wa Bwana arusi, jinsi alivyolipenda na kulichagua Taifa la Israeli kama mali yake mwenyewe. Wakristo wa kwanza, walifikiria pia juu ya uhusiano wao na Kristo kama mfano (Yoh 3:39, 2Kor 11:2, Efe 5:23-32).”

       Basi, katika injili ya leo, Yesu alishangaa kwa sababu ya mashindano ya watu kwa ajili ya kuchukua mahali pa kwanza katika karamu naye aliwapendekezea tabia tofauti. Mtu akipendelea kuwa wa mwisho, alichagua kuwa mtumishi kama vile Kristo aliyeja sio kutumikiwa bali kutumikia.  Katika jamii, kutafuta mahali pa kwanza, msimamo, upendeleo na umaarufu ni hali ya kawaida inayosababisha mapambano, chuki na ukatili kati ya watu. Hata katika Kanisa na jumuiya zetu tunaweza kukuta hali sawasawa na hii. Yesu alikwisha ameonya kuhusu hatari za hali hii na kufundisha unyenyekevu kama njia kamili. Unyenyekevu ni fadhila ambayo inampendeza Mungu na watu. Kuwa mnyenyekevu ni kuchukua hali ya udhaifu ya kibinafsi kwa kushinda mwelekeo wa kujiona mwema kuliko wengine. Inamaanisha kutumia nguvu zote za kibinafsi ili kuwatumikia wengine kwa ukarimu na upendo hasa wakiwa ni maskini na walio na shida ya kimwili ambao hawana cha kutulipa. Hii ni kipimo cha furaha ya kweli kwetu. Hii ni njia ya kuonyesha kwamba upendo wa Mungu unatolewa kwa hiari kwa ajili ya watu wote. Katika karamu ya arusi mbinguni, yeye atawakaribisha wale wanaomwelekea kupitia matendo ya upendo.

       Lengo la Yesu ni kuzaa ubinadamu mpya na aina mpya ya uhusiano miongoni mwa watu. Msingi wa ubinadamu mpya ni unyenyekevu na upendo. Thamani hizi zinapaswa kusaidiwa zaidi miongoni mwetu. Kupitia utumishi wa kindugu na wa kinyenyekevu tunaweza kufikia lengo la Yesu ambaye ana mawazo tofauti na yale ya jamii. Kwa Yesu, mtu ni mkuu ikiwa yeye ni mdogo; tena mtu ni wa kwanza ikiwa yeye ni wa mwisho; pia mtu anakwezwa ikiwa yeye anajishusha. Katika jumuiya zetu za wafuasi wa Yesu muhimu ni kutumikia wenzetu kama Mwalimu Yesu alivyo. Yeye anatuhakikishia kwamba yoyote tunayofanya kwa ajili ya walio na shida yatasahauliwa na Mungu. Maisha yake ya mtumishi ni kipimo kwetu. Hatuhitaji mahali pa kwanza, bali kutumikia kwanza kwa unyenyekevu na ukarimu. Tujifunze kutoka kwa Kristo aliyefahamika kama Mtumishi wa Bwana kwa namna ya kipekee ili utumishi wetu uwe bila unafiki na kuweze kumpendeza Mungu.

Fr Ndega  

Nenhum comentário: