sábado, 28 de maio de 2016

ANATUFUNDISHA KUSHIRIKI KILE TULICHONACHO

Kutafakari kuhusu Lk 9, 11b-17


Tunaadhimisha sikukuu ya Mwili na Damu takatifu ya Bwana wetu Yesu Kristo. Sikukuu hii ni ukumbusho wa karamu ya mwisho tunayosherehekea katika Alhamisi kuu. Lakini, katika siku ile hatuwezi kusherehekea kwa shangwe kubwa kwa sababu ya kukumbuka mateso ya Bwana. Siku hii ya leo tunaalikwa kusherehekea kwa shangwe na shukrani pamoja na kanisa zima, hasa kwa maandamano, kwa sababu ya zawadi hii kubwa ambayo tunakumbuka kufa na kufufuka kwa Yesu na kujitolea kwake kama chakula chetu cha kiroho. Hiki ni chakula kinachodumu milele nacho kilishuka mbinguni kuutoa uhai kwa ulimwengu.

Neno Ekaristi linatokana na neno la kigiriki na kumaanisha shukrani. Huu pia ni mwaliko wa kumshukuru Mungu kwa zawadi nyingi ambazo tumepokea kutoka kwake na hasa kwa zawadi hii kubwa ya Ekaristi takatifu. Maandamano ni sehemu ya maonyesho ya shukrani hii. Tunaposhukuru tunaonyesha kwamba tunathamini zawadi tuliyopewa. Ili tuweze kushukuru tunahitaji kukumbuka. Kukumbuka katika Ekaristi ni kuishi na kushiriki, kwa sababu Yesu aliwaambia wanafunzi wake maneno haya, yaani, “Fanyeni hivi kwa kunikumbuka mimi.” Kwa maneno mengine, tunapokumbuka Yesu tunashiriki katika tukio ambalo tunaadhimisha. Basi kusherehekea Ekaristi takatifu ni kuishi pamoja na Yesu, uzoefu wa kujisalimisha kwake kwa ajili ya wokovu wa ulimwengu. Ndiye anatushirikisha katika sadaka yake yenye uzima na utakatifu.

Injili inaongea kuhusu kuzidishwa kwa mikate na samaki. Kupitia uzoefu huu Yesu aliwalisha chakula umati wa watu na kutangaza wakati mpya. Andiko hili linakuja baada ya mitume watumwe na Yesu kwa nguvu ya kuponya wagonjwa na kuondoa pepo wabaya. Waliporudi wakampasha Yesu habari kuhusu mafanikio ya kazi yao naye Yesu aliwaalika waende pamoja naye kwenye mahali pa faragha. Mwaliko huu wa Yesu haukumaanisha kujifunga ama kutofautiana kuhusu hali ya watu. Kisha, watu waliwatafuta; nao ingawa waliivuruga nia ya Yesu na wanafunzi wake, walikaribishwa vizuri na Yesu ambaye aliwahubiria habari ya ufalme. Hapo tuko na mwanzo wa uzoefu wa muujiza, kwa maana Yesu alitambua kuwa watu waliomfuata walikuwa na njaa mbili, yaani, njaa ya chakula cha kimwili na pia njaa ya kusikiliza neno la Mungu. Kama waliyatafuta maisha mapya, Yesu akawazungumzia juu ya ufalme na kuwaponya wagonjwa.

Wanafunzi wa Yesu walikuwa wametumwa kuwatumikia watu, lakini uamuzi wa kumwomba Yesu aufukuze umati unadhihirisha kwamba uzoefu ule haukutosha kwa kubadilisha mawazo yao. Kwa kutaka kuwaaga watu bila kufikiria hali yao ya njaa na ya mateso ni kutofautiana, yaani, hili ni kosa la ahadi. Yesu alishiriki na wanafunzi wake mamlaka yake na pia unyeti wake kuhusu hali ya watu. Kushiriki hata kile kidogo walichonacho kwa ajili ya watu wenye njaa ni sehemu ya utambulisho wao kama wafuasi wa Yesu. Kile ambacho walikidhania kuwa kitu kidogo sana kiweze kuwalisha watu, kwa upande wa Yesu kina thamani kubwa. Yesu angeweza kufanya muujiza peke yake lakini alipendelea kuwashirikisha Mitume, akiwasaidia kufahamu kwamba uzoefu wa kumfuata unadai mawazo mapya na tabia mpya. Shauri ya Kristo alibadilisha tabia ya wanafunzi na kuziweka kupatikana zawadi za Mungu kwa wote. Kama matokeo ya uzoefu huu, watu walishiba, wakishinda ukusanyaji na kuepuka ubadhirifu wa chakula. 


Kupitia Ekaristi takatifu iliyowekwa na Yesu, Mungu anatulisha kama alivyofanya na Waisraeli kupitia chakula cha mana. Katika kila Ekaristi tunayoadhimisha tunaishi tena matendo na maneno ya Yesu akiwahakikishia wote chakula na kutualika kushinda mwelekeo wa kijamii wa ukusanyaji  na ubadhirifu wa chakula ambao unauzuia uzoefu wa ndugu wa kweli ulio matokeo ya adhimisho la Ekaristi. Ikiwa uzoefu wetu wa Ekaristi ni wa kweli, tunapaswa kujifunza kushiriki kile tulichonacho na kufanya kwa ukarimu kile tunachoweza, tukiamini kuwa Yesu yupo nasi na kutunganisha naye ili matendo yetu yawe ushiriki katika kujitolea kwake kwa uhai wa ulimwengu. 

Fr Ndega
Mapitio na marekebisho: Sarah


Nenhum comentário: