segunda-feira, 16 de maio de 2016

TUMEPOKEA NGUVU KUTOKA JUU


Mdo 2: 1-11; 1Wak 12: 3b-7, 12-13; Yo 20: 19-23

    Tunaadhimisha sikukuu ya Pentekoste, iliyo ukamilifu wa wakati wa Paska. “Neno Pentekoste linatokana na neno la Kigiriki linalomaanisha “–a hamsini”, yaani siku hamsini. Jina lingine la Pentekoste ni “Sikukuu ya Majuma.” Iliitwa sikukuu ya Majuma kwa sababu sikukuu ya Pentekoste iliangukia siku ya hamsini, juma la majuma saba baada ya Sikukuu ya Paska (Tobiti 2,1). Katika Agano Jipya sikukuu ya majuma imepewa maana mpya. Sikukuu ya Pentekoste ni sikukuu ya kushuka kwa Roho Mtakatifu.” Sikukuu hii inasherehekea ujio wa Roho Mtakatifu juu ya wanafunzi wa kwanza na mwanzo wa utume wa Kanisa, lililo Jumuiya ya Agano Jipya. Katika sikukuu hii tunasherehekea uhakika wa uwepo wa Roho Mtakatifu kanisani na ndani yetu. Huyo ndiye Roho wa Yesu na Baba; aliye Roho wa faraja kwa wale wanaohisi kutokuwako kwa Yesu; huyo ndiye Roho wa nguvu kwa wale wanaohitaji ujasiri ili wawe mashahidi wa Yesu kwa wote; yu Roho wa umoja ili ushuhuda kuhusu Yesu uwe kuaminika.

      Masomo mawili, yaani, somo la kwanza na somo la tatu, yanaongea kuhusu mahali ambapo wafuasi walikuwa wamekusanyika, kushiriki pamoja matarajio yao kuhusu ahadi ya Yesu, lakini bila shauku kwa sababu ya upinzani wa jamii ya Wayahudi dhidi ya mafundisho ya Yesu na wafuasi wake. Yesu aliahidi kuwepo pamoja nao siku zote na aliwashauri kusubiri nguvu kutoka juu, ambaye atakuja juu yao hivi karibuni. Hivyo imani yao iliimarishwa katika neno la Yesu na waliweza kusubiri kwa uvumilivu, wakimwomba Mungu ili wapate nguvu hii. Ghafla, kulingana na mapenzi ya Mungu, Roho aliwashukia akiwajaza wote na mahali pote. Kulingana na Injili ya Yohane zawadi hii ya Roho Mtakatifu ilitolewa katika siku moja ya Ufufuko kama alama ya maisha mapya ya Yesu kwa wote. Kutokana na uzoefu huu Sikukuu ya Pentekoste ya Wayahudi ikawa Sikukuu ya uumbaji mpya kupitia tendo la Roho wa Yesu. Wote walibadilika na kuumbwa tena. Kama hii, kanisa, jumuiya ya wafuasi wa Yesu, lilianza safari yake ya umoja kwa nguvu ambayo ikalifungua kwa dunia nzima.

      Kuingia kwa Yesu katika mahali ambapo wanafunzi walikusanyika kuliwasaidia kushinda hofu na kugundua tena shauku katika safari yao. Yesu alimvuvia Roho Mtakatifu juu yao, kutimiza ahadi yake na kuwapa maana ili wawe mashahidi. Kupitia tendo la Roho wanafunzi walipokea zawadi ya amani na furaha ili watangaze matendo ya ajabu ya Mungu, wakiusaidia upatanisho kati ya watu. Zawadi ya lugha tofauti inaonyesha kwamba Kanisa linaitwa kuwepo katika hali ya watu na kuongea nao kwa lugha rahisi, ambayo inajenga ufahamu na ushirika. Kupitia tendo la Roho Mtakatifu watu wote wameitwa kwa ushirika na ndugu, yaani, kutokana na uzoefu wa lugha nyingi kuwa lugha ya kipekee, yaani lugha ya upendo. Lugha za binadamu ni ishara ya tamaduni zote, zinazofikiwa na upendo wa Mungu na kualikwa kujenga familia moja ya kipekee, yaani familia ya watoto wa Mungu, kutangaza maajabu yake kwa njia tofauti.


      Liturujia hii ni mwaliko wa kuishi katika umoja na upendo wa Kristo. Kama wakristo sisi tu sehemu za mwili wake. Mwili huu unahitaji kutenda vizuri ili weze kufikia lengo lake. watu wanahitaji si tu kusikiliza mambo mema kuhusu Yesu, bali wanahitaji pia kuona ukweli wa tangazo hili kupitia  ushuhuda wa ushirika wa Wakristu. Mtakatifu Yohane Paulo wa II aliandika katika waraka wake, yaani, Ut Unum Sint, kwamba kutafuta umoja na ushirika kamili miongoni mwa Wakristo sio shughuli huria, lakini ni sehemu ya ahadi ya Kanisa kama mtumishi wa Kristo (UUS, 20). Ingawa siku za nyuma zilikuwa chungu kwa Ukristo na kuendelea kusababisha majeraha mengi miongoni mwa Wakristo, tunasukumwa na upendo wa Roho Mt. tusameheane na kuishi kama ndugu. Upatanisho ni zawadi tumepokea kama kipimo ili tuweze kuishi umoja, uliotarajiwa na Kristu, “ili wao wawe kitu kimoja”. Roho Mtakatifu atusaidie katika lengo hili.

Fr Ndega

Nenhum comentário: