Kutafakari kutoka Mdo 15,1-2.22-29; Ufu 21,
10-14.22-23; Yoh 14, 23-29
Ujumbe muhimu wa liturjia ya
siku ya leo ni kuhusu hali ya makao ya Mungu ulimwenguni na ndani ya kila mtu kupitia
upendo. Hali hii inatualika kufanya upya ahadi zetu za waliobatizwa na kuboresha
uhusiano wa kweli na yule ambaye anapendezwa kukaa ndani yetu. Hali ya somo la
kwanza inaongea kwamba mwanzoni mwa uinjilishaji wanafunzi wa Yesu walihitaji
utambuzi sana watangaze habari njema ya Yesu bila kipimo na masharti. Baadhi ya
desturi za binadamu ni kama mzigo katika uhusiano wa watu na Mungu. Mazungumzo
ya Pulo na Barnaba pamoja na mitume wengine wameongozwa na Roho Mtakatifu ni
mfano wazi kuhusu njia ya Kanisa ya kutenda ili liweze kutatua shida na ugumu miongoni
mwa wana wake kwa sababu ya tofauti ya tamaduni, ya mawazo na kadhalika. Kulingana
na mtazamo wa Yohana, Mungu alifanya makao duniani na kupitia Yesu, aliye
hekalu la kipekee tunaweza kukutana na Mungu kwa kweli. Mwelekeo wa safari yetu
kama watu wa Mungu ni kushiriki katika utukufu wake na kutiwa nuru kupitia
Mwana wake ambaye ni mwanga wa ulimwengu.
Katika injili tuko na hotuba ya
kuaga ya Yesu anayewashauri wafuasi wake walishike neno lake kama alama ya
upendo wao kwake. Wanafunzi wana maana nzuri ya kufanya hivyo kwa maana hiyo ni
njia maalum ya kuwa makao ambapo Utatu Mtakatifu wanaweza kuja na kukaa.
Uhusiano wa ushirika kati ya Mwana na Baba na Roho Mtakatifu ni mwaliko wa
ushiriki wa wale watakaoendeleza kazi ya Yesu ulimwenguni. Kipimo cha mwendo
huu ni neno lake linalo asili katika Baba na linapatikana katika nyakati zote
kupitia tendo la Roho Mtakatifu. Roho huyo ni msaadizi anayeweza kubadilisha
maisha ya yeyote anayejifungua kwa tendo la neema ya Mungu. Wanafunzi
wanaalikwa kuishi hatua mpya katika safari yao na maneno haya ya Yesu ni faraja
inayoijaza mioyo yao kwa matumaini. Yesu
anawafundisha kwa uvumilivu jinsi ya kuishi utambulisho wa wanafunzi na
kumkaribisha nyakati zote. Ingawa tangu mwanzo wa kazi yake Yesu alijifunua
kupitia hali ya kawaida, mpaka hapo wanafunzi wake walikuwa na mazoea ya
kumtambua Yesu kupitia mambo makuu. Kutoka hapo, wanapaswa kumtambua Yesu na
kumdhihirisha kwa njia tofauti kabisa.
Yesu atatoweka kimwili lakini
ataendelea kwepo ndani ya wanafunzi wake kupitia upendo. Mahali ambapo Yesu
yupo vivyo hivyo Baba na Roho Mtakatifu wapo. Ikiwa mara iliyopita (Yoh 13,
31-35) tulitafakari kuhusu haja ya kupendana kama Yesu alivyopenda, yaani, amri
ya kupendana kama kipimo ili watu watambue nani ni kweli wanafunzi wa Yesu,
sasa umuhimu wa kutafakari kwetu ni upendo kati ya Yesu na wanafunzi wake ambayo
ni njia ya kweli ya kumfanya Mungu atambuliwe kwa wote baada ya kifo cha Yesu. Yesu
hakuwaacha wanafunzi wake kama walio yatima bali ataendelea miongoni mwao kwa
njia tofauti. Yeye, pamoja na Baba na Roho Mtakatifu wanakuja daima kwetu na
kutarajia kukaribishwa vizuri. Ujio wao ni ufanisi sana, kulingana na Baba wa
Kanisa Gregori, yaani, “wanakuja kwetu twende kwao; wanakuja kusaidia wakati wa
dhiki; tunakwenda kwao kwa kutii; wanakuja kwa kutuelimisha, tunawaendea kwa kutafakari;
wanakuja kwa kutujaza, tunawaendea kwa kushikilia; ufunuo wao si wa nje bali wa
ndani; makao yao kwetu si ya muda bali ya milele. Imesemwa tutakuja kwake na
kufanya makao kwake.”
Yesu anaongea kuhusu Baba kwa
hamu na kutambua sana msaada wa Roho Mtakatifu katika kazi yake. Huu ni mwaliko
wa tuishi uhusiano mpya miongoni mwetu hata tufikirie wengine muhimu kuliko
sisi wenyewe na kutambua kazi yao muhimu zaidi kuliko zetu. Ufunuo wa Yesu unaleta
changamoto kwetu tulioalikwa kuendeleza kazi yake. Alitaka kwamba kupitia
maneno na matendo yetu dunia itamjue. Bila shaka kwamba tunapaswa kuwa waaminifu
na mwendo huu ni matokeo ya kulisikia na kulishika neno lake ambalo ni kipimo
cha upendo wetu kwake. Wakati tunalishika neno lake Yesu tunaruhusu kuingia kwa
Utatu Mtakatifu ndani yetu. Hali hii tumeona tangu ubatizo wetu, lakini tumekosa
ahadi ya kuishi kulingana na uwepo huu. Kuhusu hayo Mt. Paulo anatukumbusha
haja ya heshima kwa miili yetu kwa sababu hii ni hekalu la Roho wa Mungu.
Fr Ndega
Nenhum comentário:
Postar um comentário