quinta-feira, 12 de maio de 2016

ALIINUA MIKONO YAKE NA AKAWABARIKI


Kutafakari kutoka Mdo 1, 1-11; Waef 1, 17-23; Lk 24, 46-53

           Tunasherehekea kupaa kwa Bwana wetu Yesu Kristo. Yeye alifanya kazi miongoni mwa wanadamu kwa miaka mitatu. Kupaa ni hitimisho ya kazi yake, lakini anaendelea kwepo ulimwenguni kupitia Roho wake. Basi, sikukuu hii inatufafanulia fumbo la kuaga na uwepo wa Yesu kwa sababu yeye hakumwacha Baba alipokuja kwetu na hakutuacha alipomrudia Baba. Kupaa kwake kunaongea kuhusu njia mpya ya uwepo wake miongoni mwetu, kutangaza hatua mpya ya kazi yake. Huu ni wakati wa Kanisa, jumuiya ya wanafunzi wa Yesu. Ujumbe muhimu kuhusu hali hii ni wazi sana katika maandiko mawili ya Luka, yaani, Injili na kitabu cha Matendo ya Mitume. Katika Injili anajulisha vitendo vya Yesu, na katika Matendo ya Mitume anajulisha vitendo vya wanafunzi wake waliosaidiwa na Roho wake Mtakatifu.    

          Kuonekana kwa Yesu kwa muda fulani kuwaimarisha wanafunzi wake kugundua tena maana ya uanafunzi, wakishinda hofu na mashaka kuhusu hali ya ufufuko wake. Uzoefu huo ulikuwa mpya sana kwao naye Yesu alifahamu kwamba alipaswa kuwa na utulivu kwa sababu ya imani yao ndogo. Mwendo ulikuwa wa muda mrefu, lakini wenye ufanisi sana, ukisababisha mabadiliko makubwa maishani mwa wanafunzi, yaani, kutokana na uzoefu wa wanaume wenye hofu kuwa mashahidi wenye ujasiri. Katika maneno ya mwisho kwao, Yesu aliwasaidia kufahamu uhusiano kati ya yale aliyoyatenda na kufundisha na yale yaliyoandikwa na manabii wa zamani. Habari ya toba na ondoleo la dhambi linapaswa kuwa umuhimu wa ujumbe wa waliotumwa kwa jina la Yesu aliye uso wa huruma ya Mungu Asiyeonekana. Uzoefu wao pamoja na Yesu uliwawezesha kuwa wanafunzi wa kweli, lakini walipaswa kuingojea nguvu kutoka juu ili waweze kuwa mashahidi wa Bwana Yesu tangu Yerusalemu mpaka mwisho wa nchi. Roho mmoja aliyekwepo katika mwanzo wa uumbaji na wakati wa utume wa Yesu, anapaswa kuiongoza kazi ya wanafunzi wake.

       Yesu aliyashiriki mamlaka yake na wanafunzi wake ili wawatumikie watu, wakiwatendea mema. Kutokana na mfano wa kujisalimisha kwake Kristo ushuhuda wao wa kwanza ni kujitolea kwao bila kipimo. Wanafunzi  walitumwa kama wajumbe wa habari njema kwa mataifa yote kwa sababu injili haina mpaka. Yesu alikuwa amewaahidia kuandamana na safari yao mpaka upeo. Ingawa uwepo wake wa kimwili/fizikia hauwezi kuonekana tena, Roho wake yu dhamana ya kwamba hawatendi peke yao katika kazi yao. Uwepo wa Roho wa Yesu daima katika safari ya mitume yake umeyafanya maneno yao ufanisi kupitia ishara nyingi na matendo mazuri. Kulingana na Mtakatifu Paulo, Roho ambaye aliwapewa kwa jumuiya ya kwanza ni Roho wa umoja. Kupitia Roho huyo tunaweza kumjua Mungu vizuri na kuishi katika umoja miongoni mwetu kama anavyotarajia Bwana wetu. Kila mtu anaitwa kuchukua ahadi hii ya umoja kama maana ya utambulisho. Katika jumuiya ya kikristo tumezipokea zawadi nyingi kutoka kwa Mungu ili tuwe zawadi sisi kwa sisi, na kusaidia kujenga kwa mwili mmoja, ambao ni takatifu na hai kwa sababu ni Roho mmoja anayetenda ndani yake. Hili ni fumbo la uwepo wa Yesu katika kanisa lake ambalo ni mwili wake mwenywe naye yu kichwa cha mwili huu.


    Malaika waliwaambia wanafunzi wa kwanza na wanatuambia siku ya leo: “mbona mmesimama mkitazama mbinguni?” Hakika kama Wakristo tunahitaji kurudisha mtazamo wetu kwa Yesu, aliye mfano wetu na kichwa chetu ili tuendeleze kazi yake kwa uaminifu, lakini hatuezi Kubaki wamesimama kutazama mbinguni kama ishara ya uvivu, utazamaji na upoozaji. Bwana anatutaka tuwe waangalifu na wenye ufanisi. “Wabarikiwa watumishi wale ambao watakuwa wakitumikia Bwana wao atakaporudi”. Maisha ya Kikristu ni kutafakari na kitendo, imani na matendo. Ishara za uwepo ufanisi wa Yesu zinaonyeshwa kupitia mapendo ya wale wanaomwamini na wanazifuata nyayo zake. Roho Mtakatifu afanye uwepo wa Yesu uwe ufanisi katika maisha yetu na kazi zetu ili tuendelee utume wake kwa uaminifu.  

Fr Ndega 
Mapitio na marekebisho: Sarah

Nenhum comentário: