sábado, 26 de março de 2016

TUFURAHI KWA SABABU BWANA WETU AMEFUFUKA


Kutafakari Kuhusu Lk 24, 1-12

Ndugu na dada zangu, tufurahi kwa sababu Bwana Yesu amefufuka! Amefufuka ili akae pamoja nasi na kutufanya watu wapya. Kufufuka kwake Yesu ni tendo la ajabu la Mungu na maana ya kweli ya maisha yetu. Kupitia Kristo Mfufuka uumbaji wote unafanyika upya. Mwanga wake unayaangaza magiza ya maisha yetu na kuufungua upeo wa macho wa uzima wa milele. Sikukuu hii ya ufufuko wa Bwana wetu inatualika kuishi furaha kubwa, yaani, furaha ya maisha ambayo yanayashinda mauti, furaha ya upendo ambao unaushinda uchungu. Yesu ni uwepo hai miongoni mwa wanadamu, kufufua matumaini yao. Ni nafasi nzuri ya kufanya upya ahadi yetu ya wanafunzi na kushinda hofu ambayo inatuzuia kuwa mashahidi wa kweli.
Masomo ya Agano la Kale yanatuonyesha mambo makuu ya Mungu ulimwenguni na hasa katika safari ya watu wake. Kupitia matendo ya Uumbaji, Agano, Ukombozi na Maisha mapya yeye anajifunua kuwa Mungu wa uhai na kutaka daima furaha kubwa kwa kila mmoja wa viumbe vyake. Furaha hii inatokana na uhai wa Utatu Mtakatifu, aliye ushirika wa upendo. Tangu uumbaji ametushirikisha katika uhai wake mwenyewe. Basi, uumbaji ulikuwa mwaliko wa tushiriki katika ushirika wa uhai na upendo wa Mungu. Matendo yake katika Agano la Kale hayakuwa kitu kingine ila kuwandaa watu wake kwa kuzaliwa upya kupitia ufufuko wa Mwanawe pekee. Hali hii ni wazi sana kupitia ubatizo ulio uzoefu wa ufufuko kwa njia maalum, kutufanya kuumba tena na kuchukuliwa na Mungu kama watoto wake tulio warithi pamoja na Mwanawe. Kwa maneno mengine, tunakufa na Yesu, kuzika hali zee ya wenye dhambi na kufufuka tena naye kama watu wamefanyika wapya kabisa.  
Katika injili, wanawake, yaani Mariamu Magdalene, na Yoana, na Mariamu mamaye Yakobo na wanawake wengine walikuwa na upendeleo wa kuwa mashahidi wa kwanza wa ufufuko wa Bwana. Waliamuka mapema asubuhi, kwa sababu waliimarishwa na upendo wa kweli kwa Yesu; upendo huu unawaongoza kumtafuta. Kwa muda, uzoefu wa ufufuko kwao ulikuwa kaburi tupu na tangazo la malaika, lakini ishara mbili zilitosha ili waweze kuishi tena furaha ya uwepo wa Bwana wao. Yesu hakuwako kaburini kwa sababu huko ni mahali pa wafu; naye ndiye alifufuka na kuishi milele. Habari njema hii ya furaha kubwa inapaswa kutangazwa. Baada ya tukio lililoonekana kuwa ushinde, yaani, kifo chake, Yesu aliruhusu uwezo wa kuziona ishara za ushindi wake kwanza kwa wale ambao walikuwa waathirika wa ubaguzi katika jamii na, kwa hivyo, walijiona waliotenganishwa. Kwa kweli kupitia chaguo hilo Yesu alithibitisha pendekezo lake la muda mpya, mawazo mapya na uhusiano mpya kati ya watu. kwa kufanya kazi muhimu ya tangazo la ufufuko, wanawake walipaswa kushinda hofu na mawazo kutoka jamii kuhusu wao wenyewe. Walikuwa na uhakika kwamba Mtu aliyechagua aliwaandamana nao daima.  

Kama wanawake na wanafunzi wa kwanza wengine, tunaalikwa kufanya uzoefu wa Bwana Mfufuka. Uzoefu huu siku hizi unaidai imani zaidi kuliko kugusa. Neno lake na ushuhuda wa wale waliotutangulia unatusaidia kushinda hofu na kuchukua ahadi ya kuwa mashahidi pia. Kupitia msaada wa wengine na msukumo wa Mungu tunaweza kushinda hofu zetu zote na kukubali kwa shauku utume wa kutangaza habari njema ya ufufuko wa Yesu. Yeye yupo miongoni mwetu na ndani yetu ili atufanye vyombo vya huruma yake. Uzoefu wa wanawake unatusaidia kumtafuta Bwana Mfufuka kwa mioyo yetu yote na kuruhusu kuongozwa na mwanga wake ili uwepo wetu uwe ufanisi katika mahali popote tuendapo. Uzoefu wa kumtafuta Bwana unatuwezesha kushinda vikwazo njiani, kutufanya mashahidi wa upendo ambao unauzaa uhai. Bwana Mfufuka anaishi miongoni mwetu! Tunapaswa kuwa macho ili tumtambue katika hali nyingi zinazoyahusisha maisha yetu. Yeye atupatie ujasiri ili tuwe mashahidi wake wa kweli.

Fr Ndega
mapitio na marekebisho: Sara

Nenhum comentário: