quinta-feira, 24 de março de 2016

MATESO YA KRISTU NI ALAMA KUU YA MSHIKAMANO WAKE KWA AJILI YA WANAOTESEKA


Kutafakari kutoka Yoh 18-19

Kanisa zima linakumbuka siku ya leo mateso na kifo cha Kristu, mume wake na mkombozi wa ulimwengu. Kuadhimisha mateso na kifo cha Yesu ni kuadhimisha upendo wake mkuu hadi matokeo upeo. Yesu ni zawadi kuu ya Mungu na alama ya upendo wake kwa dunia nzima, “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee... Maana Mungu hakumtuma Mwana ulimwenguni ili auhukumu ulimwengu, bali ulimwengu uokolewe katika yeye (Yo 3,16-17).” Mwana wa Mungu aliuleta wokovu ulimwenguni akafa msalabani na akiyashinda mauti kupitia ufufuko wake mtukufu. Kwa hivyo kupitia msalaba mtakatifu tunakumbuka si mateso na kifo cha Kristu tu, lakini pia ushindi wake na wokovu wetu. 

Somo la kwanza linatujulisha historia ya mateso makali ya mtumishi wa Bwana, ambaye ni mwaminifu kwa kazi aliyomkabidhi Bwana wake, akichukua dhambi za watu wote. Mtumishi huyu aliuleta ukombozi, akibeba huzuni ya wote, akijiruhusu kujeruhiwa na makosa na maovu yao. Ingawa yeye alidhulumiwa na kuteswa, akaweza kuyasalimisha maisha yake mikononi mwa Mungu, akiuhakikisha msamaha kwa wenye dhambi wote. Mafanikio ya kazi yake hayakutokana na uwezo wa binadamu, lakini yalitokana na nguvu ya Mungu aliye kimbilio lake na ulinzi wake. Wakristo hutafsiri kazi ya mtumishi huyo kama mfano na utabiri wa maisha na kazi ya  Kristu ambaye alichagua kuwa mtumishi, akikubali fedheha na mateso ili afanye mapenzi ya Mungu.

Simulizi ya mateso, kulingana na mwinjilisti Yohana, inatusaidia kutafakari kwa njia ya ndani kuhusu maana ya mateso na kifo chake Yesu. Tunaalikwa kutambua katika kusulubiwa alama kuu ya upendo wa Mwana wa Mungu, aliyeutoa uhai wake kwa ajili ya wanadamu wenye dhambi. Mateso yake ni mwanzo wa ushindi wake juu ya mauti, kufufua matumaini ya watu. Kwake hakuna upendo mkuu isipokuwa kuyatoa maisha kwa wema wa marafiki. Tabia hii inatusaidia kutafakari kuhusu hali ngumu ya mateso ya binadamu na kuamini kwamba Mungu hawaachi wale wanaoteseka. Kama binadamu, Yesu hakutaka kuteseka, lakini alikubali hiyo kwa sababu alitaka kuwapea wanaoteseka nafasi ya kuishi maisha mapya. Mateso ya Kristu yanatufundisha jinsi ya kukaribisha mateso kwa utulivu na kuwa uwepo ufanisi maishani mwa watu wanaoteseka.

Mateso na kifo cha Kristu hakiwezi kufahamiwa kama kilichotakwa na Mungu, lakini kilikuwa matokeo ya ahadi yake ya kinabii na ufunuo wa upendo na huruma ya Mungu kwa namna ya ajabu. Kristo “alikufa kwa sababu ya uaminifu wake kwa mpango wa Mungu mpaka upeo”. Yesu hakufa kama asiye na matumaini na huzuni zake hazikumaanisha kutelekezwa na Mungu. Ushuhuda kuhusu hili ni kujisalimisha kwake mikononi mwa Baba yake, kulingana na toleo la Luka, yaani, “Ee Baba, mikononi mwako naiweka roho yangu (Lk 23,46)”. Ishara yake kuu ya upendo ilikubaliwa na Baba, aliyejibu kwa ufufuko mtukufu, akiyapa maisha ya binadamu maana kabisa. Katika kifo chake vifo vyote vinashindwa na katika ufufuko wake matumaini yote yanafufuka. Nasi tunashiriki katika mwendo huu. Kwa hivyo Mt. Paulo asema, “Kila wakati tumekuwa tukichukuwa mwilini mwetu kifo cha Kristo, ili uhai wake Yesu udhihirike katika miili yetu (2Cor 4,10).”  

Pamoja na mateso ya Mwana tunatafakari pia huruma ya Mama yake ambaye anajua jinsi ya kupenda na pia jinsi ya kuteseka kwa ajili ya mtu anayependa. Maria alichukua katika moyo wake huzuni zote za mwanawe. Kama hii ilitimizwa unabii wa Simeoni katika Hekalu: "Upanga utachoma roho yako mwenyewe". Kama mwanafunzi wa Kwanza na Mwaminifu wa Mwanawe, Maria alichukua jukumu lake hadi matokeo upeo, akibaki kusimama mbele ya msalaba. Pamoja naye, wanawake wengine watatu na mwanafunzi aliyependwa na Yesu wanabaki pia. Upendo tu unaweza kueleza maana ya nguvu na uvumilivu wa wanawake katika mazingira haya magumu. Kweli, walijifunza kumfuata Yesu kwa njia ya ukarimu na kujisalimisha kabisa. Ishara ya upendo ya Kristo na safari ya kumfuata kutoka kwa wanawake ni mwaliko wa kujitolea kwetu, kuibeba misalaba yetu na kumfuata Yesu kulingana na matarajio yake kwa ajili ya wokovu wa ulimwengu mzima.  

Fr Ndega
Mapitio na marekebisho: Sara

Nenhum comentário: