domingo, 20 de março de 2016

SHANGWE KWA BWANA MSHINDI NI TANGAZO LA USHINDI WAKE


Isa 50, 4-7; Phil 2, 6-11; Lk 22, 14-23,56

    Kupitia liturjia hii tumeanza wiki kuu ya mwaka iliyo wiki kuu ya imani yetu. Kama inavyotokea katika sherehe hii, hivyo wiki hii takatifu inatualika kushiriki katika matukio ya mwisho ya utume wa Yesu wa binafsi. “Mwana wa Adamu atateseka na kufa, lakini atafufuka”. Mateso ya Mwana kwa upendo ni nafasi ya kumtukuza Baba yake na kuwaokoa ndugu zake. Tunaposhiriki katika mateso yake tena tutashiriki katika utukufu wake, kwa sababu mapenzi yake ni kwamba wale wanaomfuata washiriki katika furaha yake ya milele. Jumapili ya matawi inatufanya kusherehekea, kwa utangulizi, uhakika wa utukufu huu kwa sababu tunamshagilia Bwana mshindi anayeenda Yerusalemu bila hofu, hata akiijua nia mbaya ya adui zake. Mji huu ni maarufu kwa sababu ya upinzani kinyume na Mungu kupitia mauaji ya manabii wengi. Hata Yesu alipoongea kuhusu kazi yake ya nabii alitaja kuwa sio vizuri kwamba nabii akufe nje ya Yerusalemu. Kama wayahudi ambao walisherehekea ushindi kwa kushika matawi ya mtende, tunatumia matawi haya kama ishara ya utayari wetu wa kumfuata Yesu kwa uamuzi sawa naye mpaka upeo.

     Yesu anaanza safari yake ya kujisalimisha kama aliyebarikiwa kwa jina la Bwana. Matukio yaliyotangulia mateso na kifo chake yanadhihirisha yale yaliyokuwa sehemu ya uchaguzi wake wakati wote wa kazi yake, yaani, uamuzi wa kwenda Yerusalemu, wa kupanda mwana-punda, wa kuruhusu watu wamshangilie na wa kutaja neno mawe kama uenezi wa sifa kwa Mungu anayefanya upya uumbaji wote kupitia kujisalimisha kwake Mwanae. Somo la nabii Isaya linaitaongelea kazi ambayo Yesu alichukua kama mtumishi wa Bwana anayejua sana utambulisho wake kama mwenye ulimi wa wafundishwao. Yeye ana masikio makini kwa neno la Bwana na anaweza kusema daima maneno ya faraja kwa wale ambao wana mahitaji mengi; anajua pia kwamba kila kitu alichopokea kwa Baba kinalenga kutangaza ukaribu na wokovu wake Mungu. Tena anajua kwamba hatembei peke yake kwa sababu Bwana wake yu mwaminifu wala hawaachi wale ambao wanamtumainia.

       Njia iliyochaguliwa na Yesu awaokoe wanadamu ni njia isiyotarajiwa na mawazo ya kawaida. Hali hii inatajwa katika waraka wa wafilipi unaojulikana kama “injili ya tano”. Andiko hili linaonyesha njia ya utukufu wa Kristo kulingana na mapenzi ya Mungu. Hii ilikuwa njia ya utupu. Kwa kweli ingawa akawa sawa na Mungu, hakuona hali hii kuwa ni kitu cha kushikamana, lakini alipendelea kuacha utukufu na kuchukua hali ya binadamu na kama mtumishi alitii mpaka mauti, yaani, mauti msalabani. Yeye alijifanya maskini ili atufanye tajiri kupitia utajiri wake. Alikataa heshima kama hii ipasavyo kwa Mungu illi apate heshima kwa maskini na wasio na nguvu katika jamii.


        Mwendo wa utupu wa Kristo ni mwendo ambao tunahitaji kupita ili maisha yetu yaweze kumpendeza Mungu ambaye ana mazoea ya kuwashusha wakuu na kuwapandisha wadogo. Hii ni njia ya uanafunzi wa kweli kama alivyosema Yesu mwenyewe kwa wafuasi wake, yaani, “yeyote anayetaka kuwa wa kwanza akawe wa mwisho; na mtu anayetaka kuwa mkuu akawe mtumishi wa wote. Hakuna njia nyinigine ili tuweze kufikia matarajio ya Mungu kama wanafunzi wa Mwanae ambaye alikuja sio kutumikiwa bali kutumikia na kuutoa uhai wake kwa ajili ya wokovu wa ulimwengu. Nao utumishi wake umejaa maana kwa sababu ulifanyika kwa upendo. tujifunze kujisalimisha kutokana na kielelezo cha Yesu ambaye hata katika wakati wa huzuni na mateso, aliilenga imani yake katika tendo la riziki ya Mungu: “Ee Baba, mikononi mwako naiweka roho yangu”. Hili lazima kuwa kilio cha roho zetu ili tujihakikishie kwamba Mungu hawezi kutuacha wala kunyamaza mbele ya kinachotokea nasi. Mbele ya kufa kwake Yesu, jibu la Mungu ni ufufuko wa Mwanawe. Mfano wake ni mwaliko wa tujitolee kwa ajili ya wengine, kufananisha maisha yetu na njia yake ya kuishi na kutumikia.   

Fr Ndega
Mapitio na marekebisho: Sara

Nenhum comentário: