Kutafakari
kutoka Yoh 8, 1-11
Andiko hili linatuletea tukio la mwanamke ambaye alifumaniwa
katika uzinzi na kutusaidia kutafakari kuhusu jambo muhimu katika sheria ya
wayahudi na maisha ya binadamu, yaani, hali ya umoja kati ya mume na mke
kupitia ndoa. Umoja huu ulichukuliwa kama mtakatifu na kubarikiwa na Mungu
tangu mwanzo. Katika mpango wake wanapaswa “kuwa mwili mmoja”. Lengo la umoja
huu ni kwa kuzaa watoto na kupata utimilifu kwa wanandoa. Mungu alijua kwamba
umoja huu ulihitaji kulindwa na, kwa hivyo, alianzisha kama amri “Usizini na Usitamani
mwanamke asiye na wako”. Alisema hivyo kwa sababu yeye ni wa kwanza anayejua
kwamba bila umoja binadamu haishi vyema na bila uaminifu umoja hauwezekani.
Wale ambao walimleta mwanamke huyo mbele ya Yesu
walitenda dhambi ya udhalimu mara mbili. Ya kwanza ni kwa sababu uzinzi
unawezekana tu kati ya watu wawili. Ikiwa washitaki hao walimleta mwanamke peke
yake kumshitaki na kumwachia huru mwanamme, walitenda dhidi ya sheria wenyewe. Kulingana
na kitabu cha Walawi (Wal 20, 10), “kama mwanamume akizini na mke wa jirani
yake, ni lazima wote wawili wauawe.” Ya pili ni kwa sababu hao washitaki
walijua kwamba wao wenyewe hawakuwa wasafi. Walikuwa wasio na haki na hata
walitaka kwamba Yesu atende kulingana na matendo yao. Ishara zilizofanywa na
Yesu zilikuwa nafasi ya watafakari kwamba maisha ya mtu ni bora kuliko sheria;
ya kutafakari pia kuhusu umuhimu wa mwanamke katika jamii; tena kuhusu haja ya
uhusiano wa kweli na Mungu pia na wengine, na kumpea mtu nafasi moja zaidi kama
vile Mungu anavyofanya kwa ajili ya wenye dhambi, kwa sababu hataki kifu cha
mwenye dhambi bali atubu na kupata uzima. Katika mwendo huu, Yesu aliamsha
dhamiri zao kuhusu udhalimu wa ubaguzi akiwafanya kufikiri na kutenda tofauti.
Kupitia njia ya Yesu ya kutenda, moyoni mwao waliweza kukiri kwamba wao pia
walikuwa wadhambi na hivyo walihitaji msamaha wa Mungu. Kama matokeo, wote
walisamehewa na Yesu, yaani, washitaki na mshitakiwa kwa sababu Yesu anataka
kujenga jamii mpya kupitia uhusiano mpya kati ya watu.
Kuhusu mwanamke huyo, alibaki katika mahali kamili, yaani,
katikati; lakini sio kama rejeo ya hukumu bali kama rejeo ya huruma. Yeyote anayekutana
na Kristo anakutana na huruma ya Mungu na kupata nafasi ya kuishi maisha mapya.
Mwanamke yule alikuwa amekufa na amefufuka, alikuwa amepotea na ameonekana.
“Enenda zako; wala usitende dhambi tena”. Yesu hakuja kuadhibu bali kuokoa; kwa
hivyo maneno na ishara zake zinamsaidia mwanamke achukue ahadi ya kuishi
tofauti, kulingana na mapenzi ya Mungu. Maneno haya yanaonyesha kwamba Yesu
hakubali udhalimu wala hapitishi kosa lolote. Anatarajia mabadiliko ya maisha.
Kwake mtu anathamini zaidi kuliko makosa yake. Kuhusu hili, yako maneno ya Mt. Yohana
Calabria yanayosema, “tunapaswa kuyachukia makosa ya mtu, lakini tunapaswa
kumpenda mtu huyu kwa sababu ndiye ndugu yetu”. Upendo unatufanya kusadiki
kwamba inawezekana kubadilisha hali mbaya kuwa hali nzuri. Tunapompenda mtu
tunausadiki uwezo wake wa kushinda udhaifu na mwelekeo mbaya wa maisha yake.
Kwa upande wa mtu aliyependwa hii ni nafasi ya kuonyesha kwamba anaweza
kujibadilisha.
Maneno ya Yesu yalikuwa faraja na kusababisha kitendo
tofauti. Ishara zake zilikuwa makaribisho na kusababisha mabadiliko ya maisha.
Ikiwa maneno na ishara zetu zinatokana na msukumo wa Mungu zinapaswa
kusababisha matokeo kama hayo. Mwanamke huyo ni mfano wa watu ambao
wanahukumiwa na kuadhibiwa miongoni mwetu. Mawe ni alama ya maneno na ishara
ambazo hazijatumika kwa kujenga ndugu, zikitia moyo na kuimarisha imani yao,
bali zimewazuia kuamini kwamba wanaweza kubadilisha maisha yao na kufikia
matarajio ya Mungu. Sisi pia ni kama mwanamke huyo. Baada ya kila mkutano na
Bwana, hasa kupitia sakramenti, tunaalikwa kuiacha dhambi na kuchukua mwelekeo
mpya wa kuishi. Neema ya Mungu ituongoze.
Fr Ndega
Mapitio na marekebisho: Sara
Nenhum comentário:
Postar um comentário