Kutafakari
kuhusu Matendo 10: 34a. 37-43; Yoh 20,1-9
Tufurahi sote, kwa sababu hii ni siku
Mungu aliyotufanyia! Tangazo la ufufuko wa Yesu ni mwaliko wa furaha, yaani
furaha ya maisha ambayo yanayashinda mauti, furaha ya upendo ambao unaushinda uchungu
na kutenda kama rafiki katika safari ya watu wapya wa Mungu, kuyaimarisha matumaini
yao. Wanafunzi wa kwanza walipotangaza tukio hilo, walianza kutokana na maisha
ya binadamu ya Yesu, aliyetiwa na Mungu kwa kazi ya wokovu wa binadamu. Kwao
Wanafunzi wa kwanza uzoefu pamoja na Yesu ulikuwa umejaa maana. Kutokana na
uzoefu huu wanaweza kutenda kama mashahidi. Kama alama ya wema wa Mungu, maana
ya maisha ya Yesu ilikuwa kuwatendea watu mema. Nalo tendo lake liliwezekana
kwa sababu Mungu alikuwa pamoja naye. Alitaka kuupendekeza uzoefu wa maana
kabisa kwa wale ambao watakuwa mashahidi wake.
Kama Kristu hakuwa amefufuka, je, mahubiri
ya wanafunzi wake yangekuwa na maana gani? Hakika yangekuwa tupu, yaani, pasipo
maana. Mbele ya kifo kisicho na haki cha mwalimu wao walikufa moyo sana, lakini
ushindi wa uhai unawapa maana mpya ya kuishi. Basi, ujumbe wa wanafunzi
unatafsiri pia ushindi dhidi ya hali ya hofu ambayo waliishi baada ya kifo cha
Mwalimu, yaani kikundi chao kilivunjika. Kwa wanafunzi ilikuwa vigumu sana kuendelea
kwa safari baada ya kukatishwa tamaa kwao kuhusu mwalimu Yesu ambaye walitarajia mengi, hasa
awe mfalme mwenye nguvu. Lakini maisha yao yalibadilishwa kabisa baada ya kuona
ushahidi wazi wa ufufuko wa Mwalimu, yaani kaburi tupu, vitambaa alivyolalia,
na baadaye Yeye mwenyewe akajionyesha kwao; kisha waliacha hofu, wakiitoa
nafasi kwa imani na kuchukua maisha ya mashahidi. Ni njia kamili ambayo
tunapaswa kuishi ili tuwe wanafunzi wa Yesu wa kweli.
Lakini tunapaswa kutambua kwamba
safari hii ya imani ya wanamume ilisababishwa na mwanamke, yaani Maria
Magdalena ambaye alikuwa na upendeleo wa kuwa ni wa kwanza kuenda kaburini,
kukutana na Yesu na kupewa habari kwa ajili ya Mitume. Walipaswa kuiacha picha
ya Yesu kama alivyokuwa alipoteseka, amekufa na kuzika ili wakaribishe njia
mpya ya Yesu aliye mzima na anayeishi kati yao kwa njia mpya na tofauti kabisa.
“Magdalena ni yule ambaye Yesu aliponya kwa kufukuza mashetani saba ndani yake.
Katika Biblia namba saba inamaanisha ukamilifu. Basi, Maria Magdalena alikuwa
ameponywa na Yesu kikamilifu.” Katika Kristo Maria alikuta upendo wa kweli
ambao alikuwa ameutafuta sana kwa muda mrefu. Mwanamke huyo alijifunza jinsi ya
kuwa mwanafunzi wa kweli, akimfuata Yesu wakati wa mahubiri, tangu Galilaya
hadi msalabani. Kwa hivyo anastahili cheo cha “Mtume wa Mitume wa Yesu.”
Baada ya kupokea habari kuhusu
udidimizi wa mwili wa Kristo, wanafunzi wawili wakaenda mbio kuelekea kwenye
kaburi, yaani Petro na mwanafunzi aliyependwa na Yesu (Yohane). Walikimbia
pamoja, lakini huyo mwanafunzi alifika kwanza. Kama hivi ni upendo ambao
unapaswa kufika kwanza katika kila kitu. Yule anayependa anapata kuwa wa kwanza
katika maonyesho ya upendo na imani. Anaweza kutambua mabadiliko kandokando
yake, kwa sababu yeye mwenyewe ana moyo ambao umebadilishwa na uzoefu wa
kujiona kupendwa. Uzoefu wa ufufuko ni uzoefu wa upendo wa Mungu anayetuchagua
tumtumikie na kutubadilisha kabisa ili tuwe mashahidi wa upendo unaozaa uzima,
unatufanya kushinda vikwazo, hofu na mashaka na kutufanya kuishi kwa hamu
uzoefu wa ndugu. Kuhusu Petro, ndiye alama ya mapigano daima ya mtu ili aweze
kushinda kuchoka kwa kazi; ni alama pia ya mtu ambaye anajaribiwa kufa moyo,
lakini anashinda kwa sababu ya uzoefu mkubwa wa kujitolea ulio muhimu kwa
kuwaongoza na kuwashauri wengine. Ushuhuda wetu kama mashahidi wa Bwana Mfufuka
uwe kama ilivyotokea na wao. Tumsifu Bwana Mfufuka!
Fr Ndega
Mapitio na marekebisho: Sarah
Nenhum comentário:
Postar um comentário