Kutafakari kuhusu
1Waf 17, 17-24; Wag 1, 11-19; Lk 7, 11-17
Liturujia ya jumapili hii inatualika kuona huruma ya
Mungu kwa kwa ajili ya wote wanaoteseka. Mungu anaguswa na hali yetu na kutenda
kwa huruma kwa sababu hii ndiyo tabia yake mwenyewe na kwa sababu tena anataka
tujifunze kutoka kwake mfano mzuri wa kutenda. Turuhusu
kusaidiwa na neno lake ambalo linaimarisha imani yetu na kuutoa mwelekeo kamili
kwa maisha yetu. Neno hili ni kweli kinywani mwa Eliya alipompa mama mjane
mtoto wake aliyefufuka. Hili tena ni kweli kupitia mahubiri ya Mtakatifu Paulo
alipoutangaza ufunuo wa Yesu Kristo kama habari iliyojaa maana. Neno hili
linaendelea kusababisha hali mpya kabisa maishani mwa wote ambao wanamtumainia
Mungu.
Katika sehemu ya mwisho injili inaongea kwamba “habari hii
ikaenea katika Uyahudi wote. Na katika nchi zote za kando kando. Hii ni habari
kuhusu kutembelea kwake Mungu kuwakomboa watu wake kupitia Yesu aliye Nabii
mkuu. katika Yesu Mungu anajifunua kama aliye karibu sana na mwenye unyeti sana. Kwa hivyo
ni halali kusema kwamba Mungu wetu anao “moyo”. Tulisherehekea hali hii katika
Ijumaa iliyopita kupitia Sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu. Yesu mwenyewe
alisema kwamba Yeye yu mpole na mnyenyekevu wa moyo. Katika moyo wake zinakaa hazina
za hekima na elimu. Kutokana na moyo wake tumeona tendo la huruma ya Mungu. Mfano
wake wa unyeti ni mwaliko wa kuboresha tabia za wema na upole kama alama ya
utunzaji wa Mungu. Habari ya njia maalum ya Mungu ya kuwajali watu wake
inapaswa kutangazika. Habari hii inaiimarisha imani na kuyafufua matumaini kama
ilivyotokea maishani mwa mama yule mjane ambaye alikuwa amempoteza mwanawe wa
pekee, lakini akampokea tena kwa sababu ya hisia za moyo wa Yesu.
“Wakati Yesu alipomwona mama yule... akamwonea huruma.” Injili zote zinamjulisha Yesu kama yule
aliyeguswa na mahangaiko na mateso ya watu. Huruma ni tabia yenyewe ya moyo
wake. Huruma hii inamsukuma kutenda vitendo, ili kuwapunguzia wanaoteseka uzito
wa mateso na mahangaiko yao. Mbele ya mahangaiko ya wanadamu Mungu amejibu
daima kwa jibu kamili ambalo linaonyesha njia maalum yake ya kupenda. Upendo
wake si kitu cha kinadharia bali “kwa mwonekano wake unaonyesha kitu cha
kushikika: nia, mitazamo na tabia zinazoonyeshwa katika maisha ya kila siku.”
Njia maalum ya Mungu ya kujibu mbele ya maumivu ya kibinadamu inamaanisha mahangaiko ya upendo wake kwetu. Watu
walitambua huruma na ukombozi wa Mungu kupitia tendo la Yesu. Hivyo, walifikia lengo
la utume wa Yesu, yaani, kudhihirisha huruma ya Mungu. “Kila kitu ndani yake
kinaongelea huruma. Hakuna chochote kwake kinachopungukiwa na huruma. Tendo
lake kwa ajili ya maisha ya watu linafunua kwamba Mungu anatamani wawe wenye
afya njema; anataka kuwaona wenye furaha, wenye kujaa furaha na amani."
Kanisa linatufundisha kutangaza kwamba “moyo wa Yesu ni
chemchemi ya huruma” na Neno la Mungu lenyewe linashuhudia kwamba “Kwa upande
wake tumepokea neema juu ya neema”. Tunaalikuwa kuamini kwamba Yesu ni
mwenye unyeti sana mbele ya hali yetu hasa nyakati za
maumivu na huzuni, ambazo zinaonekana kwamba sisi tumeachwa peke yetu. Katika
Kristo Mungu ni mwenye unyeti hasa kwa kutufundisha njia kamili ya kuwa
binadamu wa kweli, yaani, njia ya kusaidiana na kumpa
Mungu nafasi ya kutenda maishani mwetu kwa nguvu ya upendo wake. Yeye tunayemwamini
ni Mungu wa uhai naye amependezwa kutushirikisha katika uzima wake wa milele, kwa
sababu sisi tu wanawe wapendwa. Tujihakikishie kwamba Mungu hawezi kutuacha
wala kunyamaza mbele ya kinachotokea kwetu. Ikiwa katika Yesu, yeye anajifunua
kama ufufuko na uzima, tunapaswa kutangaza kwamba Mungu hataki kifo. Hali hii
inatupa matarajio kuhusu kufufuka kwetu na maisha kamili kwani yeye si Mungu wa
wafu bali wa wanaoishi. Kulingana na mapenzi yake maisha yetu yanafaa kupata
ukamilifu. Neema ya Mungu iimarishe imani yetu
katika riziki yake kwa sababu yeye yupo karibu nasi daima na hawaachi kamwe
wale wanaomwamini.
Fr Josuel Ndega
Mapitio na marekebisho: Sarah
Nenhum comentário:
Postar um comentário