Kutafakari kuhusu Lk
7:36-8,3
Tukio hili la
mwanamke mwenye dhambi lilitokea humo nyumbani kwake Simoni Mfarisayo, aliyemwalika
Yesu kula chakula. Yesu Alipokuwa mezani akila pamoja na wageni wengine mwanamke
huyo anayefahamika kama mwenye dhambi akatokea na kuanza kumkaribia Yesu akimwonyesha
ishara za upendo na shukrani kwa sababu aliuona msamaha na upendo wa Mungu
katika hali yake ya dhambi. Ingawa Simoni alichukwa ahadi ya mwaliko, ni Yesu mwenyewe
aliyetaka kukutana na Simoni na kumwongozea njia mpya ya kuishi. Kwa kweli
Simoni alihitaji njia mpya, mtazamo mpya na kadhalika. Alimwalika Yesu lakini
hakujua jinsi ya kumkaribisha vizuri. Yeye alisahau ishara za msingi kama
zilivyokuwa desturi miongoni mwa Wayahudi, yaani, hakumpa Yesu maji kwa miguu
yake; hakumbusu Yesu akionyesha kwamba alipendezwa na kutembelea kwake; hakumpaka
kichwa chake Yesu mafuta.
Katika
injili ya Luka, Yesu anapenda kushiriki pamoja na watu katika chakula. Kwa
kushiriki milo na watu wa aina na ngazi zote katika jamii, Yesu alionyesha kuwa
yeye alikuwa wa watu wote, matajiri na maskini pamoja. Tukumbuke wakati
alipokula chakula nyumbani kwake Mathayo pamoja na wenye dhambi wengi;
tukumbuke pia wakati alipojikaribisha mwenyewe kwa karamu nyumbani mwa tajiri
Zakayo. Kutembelea kwake Yesu kunasababisha mabadiliko maishani mwa watu
kuwaongoza kufikiri na kutenda tofauti. Katika injili ya leo, ingawa alikuwa
Simoni ambaye alimwalika Yesu nyumbani kwake, ni mwanamke fulani ambaye
alimkaribisha vizuri. Mwanamke huyo ingawa hana jina, yaani heshima, hata hivyo
ana ishara ambazo Yesu alitarajia kukuta kutoka kwa Simoni aliyejiona amejaa
heshima. Mtazamo wa upungufu wa Simoni uliona kwanza udhaifu na makosa ya
mwanamke. Lakini Yesu alimwalika Simoni kuona vizuri, akisema, “unamwona
mwanamke huyo?” Huu ni mwaliko wa kuanza tena na kuona tofauti, kama Yesu
mwenyewe alivyo. Yesu anajua dhambi nyingi za mwanamke huyo, hata hivyo
anatambua kwanza ishara nyingi za upendo ambazo zinashinda udhaifu wake. Kwa
upande wa Yesu upendo unashinda dhambi naye mtu anathamini zaidi kuliko makosa
yake.
Katika
mazingira yale, Simoni ni mmoja miongoni mwa waliojiona kuwa wenye haki na kwa
hivyo, walijiona pia kwa mamlaka ya kuwachagua baadhi ya watu na kuwakataa
wengine. Yesu anaukubali mwaliko wa Simoni, lakini haukubali mwelekeo wake wa
kumhukumu mwanamke aliye miguuni mwake. Yesu anataka kwamba Simoni atambue kuwa
mgawanyiko kati ya watu wazuri na wabaya haukubaliki mbele ya Mungu. Katika
njia ya Mungu ya kutenda ubaguzi hauko. Pendo na huruma yake yapatikana kwa
wote. Kwa hivyo Yesu alimsamehe mwanamke huyo na kupendekeza toba kwa wengine.
Hili ni sharti ili huruma ya Mungu iwe ufanisi maishani mwao. Kama hivi Yesu
alitangaza ufalme wa Mungu na wale ambao walimfuata waliruhusu kuguswa na
huruma ya Mungu. Ni jambo la ajabu kwamba injili hii inaanza kwa mwanamke bila
jina na kuhitimisha kwa majina kadhaa ya wanawake, yaani, Mariamu, Yohana,
Susana na wengine wengi waliopokea tena heshima yao kwa sababu ya mkutano na
Yesu na huruma ya Mungu.
Kama
ilivyotokea kwa mwanamke huyo, sisi pia tunaalikwa kujiona kukaribishwa na
kubadilishwa kwa sababu ya mkutano na huruma ya Mungu hasa kupitia uzoefu wa
sakramenti ya kitubio na upatanisho. Uzoefu huu tena unatusaidia kuushinda
mwelekeo wetu wa kibinadamu wa kuwahukumu wengine na kuuona makosa yao kuliko
tabia zao nzuri. Wakati tunapowahukumu tunajiona wenye haki, yaani tunajiona
bora kuliko wengine. Je, ni nani aliye mwenye haki mbele ya Mungu? Tunaalikwa
kuweka juhudi zaidi ili tuweze kuwaona wengine kwa mtazamo wa Yesu. Kama ilivyotokea
katika tukio la mwanamke, Yesu anaona upendo wetu kwa kanisa, kwa jumuiya, kwa
familia juu ya yote. Nao upendo wetu unaonyeshwa kupitia uzoefu wetu wa kusamehe,
wa kuwakaribisha wengine vizuri na kuwatendea mema. Kusamehe ni asili ya Mungu
(Kut 34:6). Hatuununui msamaha wa Mungu kwa mapendo yetu bali tunaupokea kwa
hiari. Ekaristi hii takatifu itusaidie kupenda na kusamehe kama Mungu alivyo.
Fr Josuel Ndega
Mapitio na marekebisho: Sarah
Nenhum comentário:
Postar um comentário