Kutafakari kutoka Is 61: 9-11; Lk 2: 41-51
Tunaadhimisha kumbukumbu ya moyo safi kabisa ya
Bikira Maria. Kumbukumbu hii ni uenezi wa sikukuu ya Moyo Mtakatifu wa Bwana
ambayo tulisherehekea jana. Tunaalikwa kutafakari kuhusu uwezo wa Mama Maria wa kuweka moyoni mwake Neno la
Mungu na kuzaa tunda zuri kwa ajili ya dunia kulingana na mpango wa Mungu.
Tunaalikwa kutafakari pia mshikamano wa Mariamu mbele ya mateso
ya mwana wake kama ushirika wa mioyo miwili.
Somo la kwanza, kutoka kitabu cha Isaya, linaongea kuhusu
uhusiano wa kina kati ya Mungu na watu wake. Yeye anaitumia nguvu yake ili atende
matendo ya ajabu kwa ajili ya wokovu wa watu wa Israeli. Mungu ni mwaminifu kwa
watu hawa na kuahidi kuanzisha agano jipya la milele, kuuthibitisha ukaribu
wake nao na kuwaalika kuishi uhusiano naye kwa hisia ya miliki. Uhusiano huu na
Mungu unawahakikishia baraka nyingi na kuwabadilisha kuwa mfano kwa mataifa
yote. Hali hii inafanana na ndoa, yaani, Mungu ni kama mume na watu kama mke. Watu
wanaalikwa kwa shukrani na furaha kwa sababu Bwana mume wao ametenda makuu kwa
ajili yao, akiwavalisha kwa wokovu na ushindi. Jumuiya ya kikristu hutafsiri
hali ya mke huyo kama mfano wa Bikira Maria ambaye alikuwa mtumishi mwaminifu akikubali
kumzaa Yesu kwa ajili ya wokovu wa ulimwengu mzima.
Injili inaongea kuhusu ushiriki wa Familia takatifu
(Yesu, Maria na Yosefu) katika jumuiya yake. Ushiriki wa Familia hii katika
jumuiya ulikuwa desturi. Miongoni mwa Wayahudi kila Myahudi anapaswa kwenda
Yerusalemu angalau mara moja kwa mwaka kwa sababu ya sherehe ya pasaka pamoja
na wengine. Hivyo, Yesu alikuwa kijana wa umri wa miaka kumi na miwili, na
ilionekana alipotea hekaluni, lakini kwa kweli yeye alijikuta mwenyewe kwa
sababu kwa kuhusishwa na kushughulika kuhusu hali ya Baba yake kunampendeza.
Hali hii ilikuwa ngumu sana kwa wazazi wake wafahamu. Lakini walikuwako tayari
kuyakaribisha na kuyatenda mapenzi ya Mungu. Hasa kwa upande wa Bikira Maria,
ingawa hakufahamu vizuri hali hiyo, alikuwa na tabia nzuri ya kuweka moyoni
mwake mambo hayo yote, akitafakari na kutafsiri ili atende mapenzi ya Mungu. Kama
hitimisho, mtoto Yesu alirudi
Nazareti pamoja na wazazi wake na alikuwa anawatii. Hata utiifu kwa Mungu ulikuwa
utambulisho wa wana wa familia hii.
Kulingana na kumbukumbu ya leo, tunaalikwa kuulenga uangalifu wetu kwenye moyo
wa mama Bikira Maria, aliye mfano maalum wa mtumishi, wa mke na wa mwanafunzi
kwa wote. Maria aliishi uhusiano wa ndani na Mungu kwa sababu moyo wake ulikuwa
mali ya Mungu na ulikuwako kwa Mungu. Maria alikuwa makini sana kwa matendo ya
Mungu katika historia ya watu wake. Moyo wa Bikira Maria ulikuwa makao ya
Mungu, mahali pa kwanza ambapo Yesu alizaliwa. Kulingana na Wazee wa Kanisa,
“Kabla ya kumzaa Yesu tumboni mwake, Maria alimzaa moyoni mwake.” Kwa hivyo
haikuwa ngumu sana kwake Mariamu kuishi ushirika wa kina na moyo wa mwana wake
Yesu. Mbele ya mateso ya Mwana,
tunaitafakari huruma ya Mama, anayejua jinsi ya kupenda na jinsi ya kuteseka kwa ajili ya yule anayependa. Maria alichukua
katika moyo wake uchungu
wote wa mwanawe. Hivyo utabiri
wa Simeoni hekaluni ulitimizika, yaani, alipochukua mtoto Yesu mikononi mwake,
alimwambia mamaye, “Upanga utachoma moyo wako mwenyewe”.
Kati ya tabia kadhaa za Bikira
Maria tukaribisheni ushuhuda wake wa ukimya kama mwanafunzi wa kwanza na mwaminifu wa Mwanawe. Yeye
alichukua jukumu lake hadi matokeo ya mwisho. Wakati wanafunzi wengine walienda zao, Maria akabaki amesimama kando ya msalaba. Hebu mfano huu wa Maria utuimarishe ili tuweze kuishi kwa uaminifu utambulisho wetu kama wanafunzi wa Mwana wake Yesu na tujifunze
jinsi ya kujitolea kabisa kwa wema wa engine.
Fr Josuel Ndega
Mapitio na marekebisho: Sarah
Nenhum comentário:
Postar um comentário