sexta-feira, 1 de janeiro de 2016

BIKIRA MARIA NI MAMA WA MUNGU


Kutafakari kuhusu Lk 2, 16-21

Katika hali hii ya furaha na shukrani ya krismasi, tunaalikwa kusherehekea sikukuu ya Bikira Maria kama Mama wa Mungu. Yeye ni Mama wa Mungu kwa sababu ni Mama wa Yesu aliye Mwana wa Mungu na, kwa hivyo, ndiye Mungu. Maria ni mfano maalum katika safari yetu ya kikristu. Yeye ni kielelezo cha jibu letu kwa Mungu na mfano wa mafanikio ya Kanisa kama mama wa wote ambao wanamfuata Mwana wake. Ukweli wa Maria Mama wa Mungu uliheshimiwa na wakristo wa Kwanza tangu mwanzo wa safari yao, lakini ulitangazwa na Kanisa tu kupitia Mtaguso wa Efeso katika mwaka wa 431. Yeye ni kama kioo kwa ubinadamu wetu, yaani, tunapomwangalia tunajiona wenyewe vizuri. Siku hii pia ni nafasi nzuri kumshukuru Mungu kwa mwaka huu unaoisha na kumjulisha matarajio yetu kuhusu mwaka mpya hasa matarajio ya amani katika ushirika na watu wote wa dunia nzima kwa sababu leo ni siku ya amani.   
Katika Yesu, aliyezaliwa Bethlehemu, Mungu anaonyesha upendo wake mkuu kwetu, kufanya makao kati yetu na kutuletea wokovu. Wokovu ni kazi ya Mungu, lakini unatokea duniani na ushiriki wa binadamu, hasa wa Bikira Maria, aliyechaguliwa awe Mama wa Mwana wa Mungu. Mariamu alikubali kazi hii kwa upendo mkubwa na, kabla ya kuzaa Yesu katika tumbo lake, alimzaa moyoni mwake. Kama mwanamke mwangalifu, alikuwa makini sana kwa hali ya dunia na mahitaji ya wokovu kwa wanadamu wote. Aliikataa mipango yake binafsi kama kijana ili aishi mpango wa wokovu wa Mungu. Mariamu alipata kutenda wito wake kwa kulisikiliza na kulishika Neno la Mungu kwa njia ya ukimya, kuwa macho na kutafakari daima. Vile vile, alipata kuzitambua na kuzikubali ishara za huruma ya Mungu katika safari ya watu wake, kulingana na maneno haya ya Luka, “Bikira Maria aliyaweka maneno hayo yote, akiyatafakari moyoni mwake.” Mwendo huu uliwezekana kwa sababu moyo wake ulikuwa makao ya Mungu daima.
Bikira Maria aliandaliwa na Mungu ili awe mtumishi wake na, katika mwendo huu, akasaidiwa na neema yake Mungu. Hali hii ilimfanya Bikira Maria aliyefunguliwa kabisa kwa msukumo na mapitio ya Mungu. Tangazo la Malaika Gabrieli lilikuwa wakati wa maamuzi wa jibu lake. Ingawa Mungu aliamua kuiokoa dunia kupitia Mwana wake wa pekee, alitaka ushiriki wa Bikira Maria ambaye alikubali. Mariamu alikuwa mshirika mwaminifu wa Mungu kwa kazi ya wokovu. Katika udogo na unyenyekevu wake tunaweza kutambua ukuu wake, kulingana na maneno yake mwenyewe: “Mungu amemwangalia mtumishi wake katika unyenyekevu wake; watu wote wataniita mbarikiwa”. Maisha na chaguzi za Mariamu ni tangazo kubwa la makuu ya Mungu. Kulingana na maisha yake, yeyote aliyeamini katika ahadi za Mungu ni mwenye furaha, kwa sababu Yule aliyeahidi ni mwaminifu. Imani inakuwa kipimo cha msingi wa furaha.
Kama mama wa Yesu, Maria ni mmoja wetu ambaye ana ushiriki maalum katika fumbo la wokovu wetu. Yeye anakuwa ishara ya ubinadamu mpya, uliobadilishwa na kuokolewa na Mwanae. Kama hii, alimsaidia Mungu awe mmoja wetu, akichukua hali halisi yetu ya binadamu na kulitoa pendekezo mpya la maisha. Kwa njia ya Bikira Maria Mungu anaendelea kutenda makuu ulimwenguni. Kupitia jibu lake la ukarimu, Mariamu aliutoa uhai ulimwenguni. Jukumu lake lina maana pamoja na utume wa Mwanawe Yesu. Kama mwanafunzi aliandamana na utume wa mwanawe kwa uaminifu hadi matokeo upeo. Yeye anajua jinsi ya kupenda na jinsi ya kuteseka kwa ajili ya yule anayependa. Ukarimu na upatikanaji wake kama mtumishi wa Mungu unatuhamasisha katika majibu yetu ya kila siku kwa mapitio yake. Kulingana na Mariamu, jibu letu kwa Mungu linapaswa kuwa alama ya ukarimu na upatikanaji. Mfano wa Bikira Maria uwe mwaliko kwetu ili tupende Mwana wake kwa uhusiano wa ndani na kumsaidia kupitia utumishi wa ukarimu na unyenyekevu. Tukikaribisha pia mfano wa wachungaji tuwe tayari kukutana na Mungu na kumtambua katika hali zote. Kutokana na  mkutano huu tuwe vyombo vya amani katika mahali popote tuendapo.

Fr Ndega

Mapitio: Sara

Nenhum comentário: