domingo, 17 de janeiro de 2016

UHUSIANO KATI YA MUNGU NA WATU WAKE UNAFANANA NA NDOA


Kutafakari kuhusu Isa 62: 1-5; 1Kor 12, 4-11; Yoh 2, 1-12

        Maadhimisho ya wakati wa kawaida ni mwaliko wa kuishi kwa hamu fumbo la imani yetu siku zote za maisha yetu. Liturujia siku hii ya leo aliongea kwamba hali ya ukombozi ambayo Waisraeli walihisi baada ya Utumwa wa Babeli ni matokeo ya uaminifu wa Mungu. Tangu Agano la Kale uhusiano kati ya Mungu na Watu wake unafananishwa na ndoa kati ya bwana na bibi arusi kama mwaliko wa uaminifu na ushuhuda. Mambo mengi makuu Mungu anayofanya kwa ajili ya watu wake ni alama ya utukufu wake na mwanga ambao unayalenga mataifa yote. Mfano wa Yerusalemu kama bibi arusi ni ishara ya hali mpya kabisa ambayo imetokea duniani kupitia kazi ya Kristo, aliye Bwana arusi wa watu wapya wa Mungu. Katika fumbo la uhusiano huu kila mtu anawezeshwa na Mungu atumikie wenzake. Kupitia njia tofauti tunamtumikia Bwana mmoja kwa msaada wa Roho wake ambaye anatupa vipaji vingi kwa wema wa wote.
        Katika injili Yesu amealikwa harusi pamoja na wanafunzi wake huko Kana. Mama yake pia yupo na anamwalika Yesu kuwasaidia maharusi wapya. Huu ni mwujiza wa kwanza wa Yesu, kulingana na toleo la Yohane. Katika andiko hili kuna mambo muhimu mengi kwa safari yetu ambayo tunataka kutafakari sasa. Kwanza kabisa, tukio harusi inaongea kuhusu kazi ya Yesu ambaye ni bwana arusi kwa namna ya ajabu. Yeye anafunga ndoa na ubinadamu, kuchukua ahadi ya kuwa mwaminifu milele. Harusi miongoni mwa wayahudi ilichukua muda mrefu wa siku nane. Ufikirie hali ya aibu kwa wanandoa ikiwa divai haitoshi kwa wote! Hakika si mwanzo mzuri kwa wale wawili ambao wana mipango mingi kwa maisha yao. Divai ni ishara ya furaha na sikukuu. Katika andiko hili ni alama ya Maagano mawili. Divai kukuu ni Agano la Kale hasa kuhusu sheria ambayo, Ingawa ilikuwa nzuri haikuwa inasababisha matokeo yaliyotarajiwa na Mungu kuhusu maisha ya watu wake. Divai hii haikutosha kama dhamana ya furaha milele. Walihitaji divai mpya.
     Maji iliyobadilika kuwa divai ni ishara ya kwanza ya nyakati mpya zilizoanzisha ulimwenguni kupitia Yesu. Yeye ni Bwana arusi na divai mpya, maana ya furaha milele kwa wote. Divai kukuu ilikuwa nzuri, divai hii mpya ni bora. Neno la bikira Maria ni msaada mkubwa katika kazi ya Yesu na hamasa katika maisha ya waliotenda kulingana na mapenzi ya Mwanawe. Yesu hatumii jina la mama yake bali alitaja cheo ambacho ni utambulisho kuhusu jukumu la mama yake katika mpango wa Mungu. Yeye alitaka kuonyesha heshima kwa mama yake na kumjulisha kama mfano kwetu. Katika Adamu na Awa, wanandoa wa kwanza wanadamu wote walifanya dhambi. Katika Yesu ubinadamu ni ulioumbwa tena na Maria ni Awa mpya. kama ilivyotokea kwa watumishi ambao walishika neno la Maria na kulitenda neno la Yesu, vivyo hivyo jukumu la mama Maria ni kutuongoza kwa Mwanawe. Yeye ni mfano wa ajabu wa kulishika na kutenda Neno la Mungu. Mariamu anatuambia kwamba kutii kwetu kwa Neno la Mungu kunampendeza. Mungu anafurahisha sana nasi.  

    Familia inampedeza Mungu ambaye, tangu mwanzo, alimpanga binadamu kwa mfano wake. Uumbaji wa wanadamu, wanaume na wanamke, ulikuwa mwaliko kwa kuishi katika familia. Ni mapenzi ya Mungu waweze kuwa wamoja, kupendana na kusaidiana. Mungu yupo katika familia na anatenda kazi kupitia Yesu. Yesu anapenda sana kushiriki katika maisha ya familia. Yeye alizaliwa katika familia moja na kutokana na makao ya Nazareti alibariki familia zote za ulimwengu. Uwepo wake ni ufanisi ili familia  zetu zifikie lengo lao kulingana na utambulisho asili. Kumheshimu Maria, mama yake, kunatusaidia kutambua uwepo na matendo ya Mwanawe katika familia ili ishinde hofu, changamoto, taabu na majaribio mengi, hasa majaribio ya uzinzi na talaka. Uwepo wa Yesu na Maria unaiweka wakfu familia kuifanya takatifu. Katika maneno mengine, familia ni mahali pa kumcha Mungu; basi, ni mahali patakatifu. Baba Mt. Yohane Paulo wa II alisema kwamba ni lazima kuiokoa familia. Nasi tunaweza kufanya hivyo hasa kwa kuziheshimu na kuzisaidia thamani ambazo tunaziishi katika familia na zinatufanya binadamu wa kweli.

Fr Ndega
Mapitio: Sara

Nenhum comentário: