domingo, 3 de janeiro de 2016

YESU ANATAKA KUWA MWANGA WETU DAIMA


Kutafakari kuhusu Mt 2, 1-12

    Kidogo kidogo liturujia inatusaidia kufahamu maana ya kuzaliwa kwa Yesu. Yeye alizaliwa katika Bethelehemu iliyo nchi ya Wayahudi, lakini siyo kwa Wayahudi tu, bali kwa mataifa yote. Maelezo ya kuzaliwa kwake katika matoleo ya Mathayo na Luka yanadhihirisha kwamba tangu mwanzo wa maisha yake ya ubinadamu, alikuwa aliyekataliwa na nchi yake, lakini alitafutwa na kuheshimiwa na wale wasiyo Wayahudi. Hali hii ni uwazi sana pia katika injili ya Yohane (1,11-12), ingawa hakuna maelezo kuhusu utoto wa Yesu kama yapo katika injili zingine mbili. Kulingana na Yohane, Yesu “alikuja katika nchi yake mwenyewe, nao walio wake hawakumpokea. Lakini wale waliompokea, wale waliomwamini, aliwapa uwezo wa kuwa watoto wa Mungu.” Basi, Yesu alikuja kwa wanadamu wote na akawaangazia wote kupitia mwanga wake. Kuzaliwa kwake kutuhakikishia kwamba wote wanaweza kuwa watoto wa Mungu na kwamba ni mapenzi ya Mungu kuwaokoa wote.

      Habari ya kuzaliwa kwa Yesu ingekuwa njema kwa wote, lakini makaribisho yalikuwa tofauti miongoni mwa watu. Hii ilikuwa habari ya furaha kubwa kwa upande wa walio na mioyo makini kuhusu ishara za ukaribu wa Mungu na walikuwa tayari kumkaribisha daima, kama ilivyotokea na wachungaji. Lakini kwa wenye nguvu hii ilikuwa habari mbaya kwa sababu iliwaalika kutafuta thamani za kweli. walijihisi kufadhaika na kutishiwa kwa sababu hawakutaka kuacha mawazo yao na walikuwa na hofu ya kupoteza msimamo na upendeleo wao. Kwa upande wa Wageni waliotoka Mashariki habari hii iliwaletea maana ya kweli kwa maisha yao; kwa hivyo walimtafuta mfalme mpya kwa hamu sana. Makaribisho haya kwa njia tofauti yalitajwa pia katika utabiri wa Simeoni hekaluni, “Mtoto huyo atakuwa sababu ya kupotea na kuokoka kwa watu wengi katika Israeli (Lk 2,34).

     Kulingana na injili Wageni walikuwa mamajusi; basi, si hakika kwamba walikuwa wafalme wala watatu. Lakini tangu wakati wa Wakristo wa kwanza kuna utamaduni mmoja ambao umeufuata utabiri wa nabii Isaya (60,3) ambao unasema, “Mataifa yataujia mwanga wako, wafalme waujia mwanga wa pambazuko lako.” Kuhusu nambari ya mamajusi haya, tunadhani kwamba wangekuwa watatu kwa sababu ya nambari ya zawadi ambazo walimtolea Yesu, yaani, dhahabu na uvumba na manemane.” Lakini Ishara muhimu katika andiko hili ni Nyota. Hii inamaanisha mwanga wa Mungu uliowaangazia watu ili wamtafute yeye kwa hamu. Mwanga huu ni Mwanawe mwenyewe ambaye mtu yeyote akimfuata hatatembea gizani (Yoh 8,12). Mamajusi waliacha nchi zao na kuruhusu kuongozwa na nyota hii ili wafikie mwelekeo kamili wa maisha yao. Mamajusi walithamini nyota. Hivyo, kuona nyota tunahitaji moyo wa kuthamini.


      Siku ya leo Mungu anatualika kuwa macho kuhusu nyota anayotumia kutuongoza. Je, umegundua nyota ambayo inatoa maana ya kweli kwa maisha yako? Katika injili zote tunaweza kukuta ishara nyingi za nyota hii. Tuchukue mfano wa wavuvi waliovua samaki wengi; kwao samaki walikuwa ni nyota ya Yesu. Kwa wakulima mbegu ulikuwa nyota ya Yesu. Kwa wanaharusi huko Kana divai ni nyota ya Yesu kwa sababu muujiza wa maji kubadilika na kuwa divai ulimtangaza Yesu. Kwa mwanamke aliyekuwa anachota maji nyota ya Yesu ilikuwa ni maji. Kwa Petro aliyemkana Yesu aliandaa moto na kuweka samaki moto ukawa nyota ya kumrudisha Petro kwa Yesu. Kwa wafuasi wake  wa Emmaus waliokata tamaa, nyota yake ulikuwa ni mkate. Walimtambua katika kuumega mkate. Kama mamajusi, maisha yetu ni safari ya imani tukutane na Mungu na kuruhusu aweze kuzibadilisha njia zetu. Tunaalikwa kuacha baadhi ya mawazo na usalama usio kweli na kuanza safari yetu walioongozwa na msukumo Mungu. Kwake tunaalikwa kujitoa muhimu sana ya maisha yetu kwa maana yeye anastahili. Zawadi ambazo tunaweza kuzitoa zinatokana na ukarimu wake mwenyewe. Huyo Yesu ambaye tunatambua katika uzoefu wetu wa ndugu anataka kuwa mwanga wetu daima ili tutafute thamani za kweli na kukuta maana ya kweli kwa maisha yetu.

Fr Ndega
Mapitio: Sara

Nenhum comentário: