Kutafakari kuhusu Isa.
42:1-4, 6-7; Mdo. 10:34-38; Lk 3: 15-16, 21-22
Tunasherehekea sikukuu
ya ubatizo wa Bwana Wetu Yesu Kristo. Hii ni nafasi maalum ya kuukumbuka
ubatizo wetu na kuweka upya ahadi ya kuwa wakristo, kuishi wito wetu wa wana wa
Mungu kama Kristo alivyo. Yeye ni mtumishi wa Bwana, katika somo la kwanza,
aliyeitwa awe “agano la watu na nuru ya mataifa; kuyafunua macho ya vipofu,
kuwatoa gerezani waliofungwa, kuwatoa wale walioketi gizani katika nyumba ya
kufungwa.” Kulingana na kitabu cha Matendo, Yesu alifanya kazi njema kwa maisha
ya watu kwa sababu Mungu alikuwa pamoja naye. Vivyo hivyo ni maisha mapya ya
sisi sote tuliobatizwa katika Kristo, yaani tunakuwa Kristo tena, kwendelea
utume wake kwa manufaa ya Kanisa lake na wokovu wetu kwa sababu yeye yuko
pamoja nasi. Tumshukuru Mungu kwa zawadi ya ubatizo wetu ulio ushiriki katika
uhai wake.
Injili
inatusaidia kukumbuka kitu kuhusu Yohana na kazi yake. Ukuu wa Yohane ulikuwa
kutambua ukuu wa Bwana, akijifikiria mwenyewe kama sauti tu na asiyestahili
kuulegeza ukanda wa viatu vyake. Yesu mwenyewe alitambua ukuu wa Yohane akiweka
unyenyekevu wake kama mfano kwa safari yetu. Yohana aliwabatiza watu kwa maji
kama kielelezo cha kugeuka kwao. Kupitia ishara hii alitangaza huruma ya Mungu
iliyopatikana kwa wote. Basi ishara ya Yohane ilikuwa kielelezo cha kupita
kutoka katika dhambi na mauti kwenda katika neema na maisha mapya ya Mungu. Jambo
muhimu katika tendo hili la Yohana ni kwamba aliwabatiza wale waliomhitaji
Mungu na kutubu dhambi zao. Yohane na watu hao waliamini kwamba ni Mungu
anayesamehe dhambi zao. Lakini Yesu hakuwa na dhambi, kwa nini alibatizwa?
Kwa Yesu
ilikuwa nafasi maalum ya kuonyesha mshikamano wake kuhusu kazi ya ajabu ya
Yohana, kuthibisha kwamba Mungu anatarajia kwamba watu ambao ni wake warudi
kwake. Kama inatokea katika somo la kwanza, kabla ya Yesu kuongea na watu kwa
mamlaka aliyoipokea kutoka kwa Baba, Mungu mwenyewe alimjulisha akisema: “Wewe
ni Mwanangu mpendwa, nimependezwa nawe”. Sauti hii itasikika tena katika tukio
la milima. Huko milimani Mungu Baba alionyesha pendo lake kuhusu Mwanawe na
kuwaalika wote wamsikilize. Yesu alionyesha pia unyenyekevu akijifananisha na
binadamu ambaye ana udhaifu na kuhitaji kuishi katika ushirika na Mungu. Yesu
alikuja si kuishi kujitengwa na watu bali aishi kuhusishwa katika safari yao.
Kabla ya Yesu maji yalikuwa na nguvu ya kutakasa mwili pekee yake. Kutokana na
uzoefu huu Yesu aliyatakasa maji ili yawe na nguvu ya kutakasa pia roho ya watu,
yaani maji ya ubatizo.
Baada ya kupokea ubatizo wa Yohana na
kujulishwa kama Mwana mpendwa wa Mungu Yesu aliwezeshwa na Roho Mtakatifu ili
aanze kazi yake akipendekeza uzoefu huu kwa wote ambao wanataka kuwa watoto
wapendwa wa Mungu. Tunaweza kusema kwamba ubatizo ambao Yesu anapendekeza ni uwezo
wa kushiriki katika uzoefu wake wa Mwana wa Mungu. Ubatizo huu ni ishara ya
utambulisho wa kikristo, yaani Ubatizo wa Roho Mtakatifu na kwa moto, kulingana
na maneno ya Yohane Mbatizaji. Ubatizo huu una nguvu ya kufanya mabadiliko katika
maisha ya mtu yeyote kwa sababu unamfanya kuzaliwa katika familia ya Mungu.
Alama yetu kama watoto wa Mungu haiwezi kufutika. Ipo daima! Tunaweza kuishi
maisha mapya ambayo ni zawadi ya Kristo mwenyewe na matokeo ya utume wake.
Ubatizo wetu, pamoja na maondoleo ya dhambi, unadhamini ushiriki katika uzima
wa Mungu mwenyewe. Kupitia alama hii ya nje tunakufa kweli kwa maisha ya
dhambi, na pia tunapitia ufufuko wa maisha mapya katika Kristo aliye mshindi
dhidi ya dhambi na mauti. Yeye ni mwanga wa kweli ambao unamtia nuru kila mtu. Yeyote akimfuata hatatembea gizani bali atakuwa na nuru
ya milele. Kupitia
mwendo huu tumekuwa wana wa nuru ili tutembee katika mwanga wa Mungu kila siku
ya maisha yetu. Ekaristi hii itusidie kuishi lengo hili la safari yetu ya kikristo,
walio wana wapendwa wa Mungu.
Fr Ndega
Mapitio: Sara
Nenhum comentário:
Postar um comentário