domingo, 27 de dezembro de 2015

FAMILIA TAKATIFU, YESU, MARIA NA YUSUFU


Kutafakari kutoka YbS. 3,2-6, 12-14; Wak 3, 12-21; Lk 2: 41-52


   Tunasherehekea Jumapili ya Familia Takatifu Yesu, Maria na Yosefu. Sikukuu hii inatukumbusha kwanza kuhusu mkutano wa wachungaji na Maria Yusufu, na Mtoto mchanga amelala horini. Hakika kutembelea huku kulisababisha kutafakari kubwa mioyoni mwa Maria. Sikukuu hii inataja pia ushiriki wa familia takatifu katika hekalu ya Yerusalemu. Tukio hili liliwasaidia wazazi wa mtoto Yesu kujua kidogo zaidi kuhusu hazina kubwa ambayo aliwakabidhi Mungu. Hasa kwa upande wa Mama Maria hii ilikuwa nafasi maalum ya kutafakari kuhusu mpango wa Mungu. Hii ni nafasi pia ya kutafakari kusuhu maana ya familia za binadamu na mahitaji ya kuishi thamani nyingi za Familia takatifu ambazo zinampendeza Mungu na kuisaidia jamii.       
        Ushiriki wa Familia takatifu (Yesu, Maria na Yosefu) katika jumuiya yake ni kielelezo/hamasa kwa Ushiriki wetu katika jumuiya/kanisa. Kulingana na andiko hili la Luka ushiriki wa familia hii ulikuwa desturi. Miongoni mwa Wayahudi kila Myahudi anapaswa kwenda Yerusalemu angalau mara moja kwa mwaka kwa sababu ya sherehe ya pasaka pamoja na wengine. Yesu alikuwa kijana wa umri wa miaka kumi na miwili, na ilionekana alipotea hekaluni, lakini kwa kweli yeye alijikuta mwenyewe kwa sababu inampendeza kuhusishwa na kushughulika kuhusu hali ya Baba yake. Hali hii ilikuwa ngumu sana kwa Maria na Yosufu wafahamu. Hasa Mariamu, ingawa hakufahamu hali hii, alikuwa na tabia nzuri ya kuweka moyoni mwake matukio muhimu, akitafakari na kutafsiri ili atende mapenzi ya Mungu. Maria alikuwa makini sana kwa matendo ya Mungu katika historia ya watu wake. Moyo wake ulikuwa makao ya Mungu, mahali pa kwanza, ambapo Yesu alizaliwa. Kwa hivyo haikuwa ngumu sana kwa yeye kuishi ushirika wa ndani na moyo wa mwana wake Yesu.
       Sehemu ya mwisho ya injili hii inasema kwamba Yesu alirudi Nazareti pamoja na wazazi wake na alikuwa akiwatii. Hii ilikuwa njia yake ya kuishi ambayo inampendeza Mungu na ni mfano kwa wanadamu wote. Kuhusu hayo somo la kwanza pia linathibitisha umuhimu wa uhusiano wa ndani kati ya wana wa familia, kufikiria watoto kama baraka kwa wazazi. kuwatii na kuwaheshimu wazazi kunayahusu mapenzi ya Mungu na kunazivutia baraka nyingi kwa familia. Kulingana na Mt Paulo mifano ya Kristo ya utii na upendo lazima kuwa kipimo cha uhusiano kati ya wanandoa kwa sababu thamani hizi zinampendeza Mungu na zinawahamasisha watoto katika safari yao. Familia inampedeza Mungu ambaye, tangu mwanzo, alimpanga binadamu kwa mfano wake, akisema: “Si vizuri huyu mwanamume kuwa peke yake. Nitamfanyia msaidizi wa kumfaa”. Basi Uumbaji wa wanadamu ulikuwa mwaliko kwa kuishi katika familia. Ni mapenzi ya Mungu waweze kuwa pamoja, kupendana na kusaidiana. Kwa nini familia ni muhimu sana? Kwa sababu familia ni msingi wa uzoefu wa binadamu; Kwa sababu pasipo familia uimara wa jamii hauwezekani. Kwa sababu bila familia mawasiliano ya thamani ya jamii kizazi kwa kizazi hayawezekani. Kwa maana uhusiano kati ya wazazi na watoto unawafanya kuwajibika na kukomaa zaidi. Kwa sababu bora kuliko chochote, familia inayaridhisha mahitaji ya hisia na fizikia/mwili, kuwapa watoto utoto salama na imara.
      Yesu anapenda sana kushiriki katika maisha ya familia. Yeye alizaliwa katika familia moja na kutokana na makao ya Nazareti alibariki familia zote za ulimwengu. Uwepo wake ni ufanisi ili familia  zetu zifikie lengo lao kulingana na utambulisho asili. Kumheshimu Maria, mama yake, kunatusaidia kutambua uwepo na matendo ya Mwanawe katika familia ili ishinde hofu, changamoto taabu na majaribio mengi, hasa majaribio ya uzinzi na talaka. Jukumu la Yosefu pia ni chanzo cha msukumo kwa akina baba wote ili wawe ishara za ulinzi na utunzaji wa Mungu, kuzaa hali ya usalama na utulivu katika familia. Uwepo wa Yesu, Maria na Yusufu unaiweka wakfu familia ukiifanya takatifu. Familia ni mahali pa kumcha Mungu; basi, ni mahali patakatifu. Baba Mt Yohane Paulo II alisema kwamba ni lazima kuiokoa familia. Nasi tunaweza kufanya hivyo hasa kwa kuziheshimu na kuzisaidia thamani ambazo zinaishiwa katika familia na zinatufanya binadamu wa kweli.
Fr Ndega

Mapitio: Sara 

Nenhum comentário: