Kutafakari kuhusu Bar
5, 1-9; Wafil 1: 3-6, 8-11; Lk 3, 1-6
Liturujia ya jumapili hii inaendelea
kutumwalika kumkaribisha Bwana anayekuja kutuletea wokovu. Tunapaswa kujiandaa vizuri
ili tuweze kumpokee Masiya wakati wowote. Wakati wa Majilio unatusaidia
kutambua kwamba kwa matayarisho kamili ni lazima mabadiliko ya moyo, kwa njia
mpya kabisa. Maneno ya nabii Baruku
yalihamasisha watu utumwani Babeli yakitangaza ukombozi karibu. Baada ya mateso
hayo yote wataweza kurudi nyumbani Yerusalemu kwa furaha kubwa kwa sababu Mungu
aliwakumbuka na kuwaongoza katika mwangaza na utukufu wake. Huu ni mfano wa
wokovu wetu katika Kristo. Paulo anatambua kwamba imani na ushirika wa Wafilipi
ni uenezi wa injili waliyochukua kwa shauku na utayari. Kwa njia ya Kristo na
injili yake wanaweza kuzaa mazao mazuri kwa utukufu na sifa ya Mungu.
Injili
inaongelea Yohane Mbatizaji anayefikiwa na Neno la Mungu jangwani. Katika
biblia jangwa ni mahali maalum kwa uzoefu wa Neno la Mungu. Katika mahali huko
watu wengi walijibadilisha kuwa viongozi wenye nguvu kwa kuwaongoza Watu wa
Mungu kulingana na mwongozo wake. Yohane Mbatizaji anafikiriwa kuwa nabii wa
mwisho na mkuu wa manabii wote. Toleo la Luka linataja makuhani na viongozi wa kisiasa
ili kuonyesha kwamba kupitia mjumbe wake, Mungu huingia katika maisha halisi ya
watu kwa wakati fulani. Mungu haongei hewani bali hupitia katika matukio mazuri
au mabaya katika historia ya watu. Mungu
alijifanya mmoja wetu na bado yuko nasi kwa namna mbali mbali. Kwa kiyo hakuna
tukio lolote la historia lisilokuwa na maana. Kwa kuonyesha wito wa Yohane
katika matukio ya wakati wake, Luka anaonyesha kwamba tukio kubwa liko karibu.
Mungu anaingia katika historia kwa namna ya pekee na inabidi watu watayarishwe
kumkaribisha Masiya aliyetarajiwa kwa muda mrefu.
Kuja kwake Yohane Mbatizaji kuna maana na
kuufuata mpango wa Mungu ambaye ana wakati kamili kwa kila kitu. Neno lake
linayabadilisha maisha ya Yohane katika chombo cha wokovu. Kama Yohane ni
kiungo kati ya Agano la kale na Jipya, kazi yake inatangaza kwamba nyakati za
Masiya ziko karibu kuanza. Yeye ni sauti tu ambayo inatayarisha njia za Bwana.
Yohane aliwatayarisha watu kumpokea Masiya kwa ubatizo. Kupitia ishara hii
alitangaza huruma ya Mungu iliyopatikana kwa kila mtu kwa sababu ni mpango wa
Mungu kwamba wokovu wake ufikie wote. Basi ishara ya Yohane ilikuwa kielelezo
cha kupita kutoka katika dhambi na mauti kwenda katika neema na maisha mapya ya
Mungu. Kipengele muhimu katika tendo hili la Yohana ni kwamba aliwabatiza wale waliomhitaji
Mungu na kutubu dhambi zao. Yohane na watu hao waliamini kwamba ni Mungu
anayesamehe dhambi zao.
Ubatizo wa yohane ni tofauti na ubatizo wetu,
lakini yote mbili ni nafasi ya kuishi maisha mapya. Kwa upande wetu maisha
mapya ni zawadi ya Kristo na matokeo ya utume wake. Ubatizo wa kikristo, pamoja
na maondoleo ya dhambi, unadhamini ushiriki katika uzima wa Mungu mwenyewe.
Ubatizo ni wa kwanza katika sakramenti tatu za mwanzo ukifuatiwa na Kipaimara
na Ekaristi. Ubatizo wetu ni alama ya nje ya kufa katika dhambi, na pia ni
ishara ya ufufuko wa maisha mapya katika Kristo aliye mshindi dhidi ya dhambi
na mauti. Yeye ni mwanga wa kweli ambao unamtia nuru kila mtu. Kupitia mwendo
huu tumekuwa wana wa nuru ili tutembee katika nuru ya Mungu kila siku ya maisha
yetu.
Kipindi cha Majilio kinatusaidia kujiandaa
kusherehekea kuzaliwa kwa Yesu. Wakati ulimwengu wa biashara unashauri watu
wajiandae kwa Noeli kwa kununua vitu, kipindi cha Majilio kinatupendekezea
matayarisho ya ndani kiroho, na hamu ya kutaka kutupatanishwa na Mungu na
wenzetu. Kuna vikwazo vya kuondoa katika maisha yetu kwa msaada wa neema ya
msamaha wa Mungu. Kwa hivyo tuchukue wakati mzuri huu kuadhimisha msamaha wa
Mungu kwa sacramenti ya Upatanisho na kuishi kwa njia mpya uhusiano wetu na
Mungu na wengine.
Fr Ndega
Mapitio: Sara
Nenhum comentário:
Postar um comentário