Kutafakari kuhusu Sef 3, 14-18; Wap
4, 4-7; Lk 3, 10-18
Liturujia
ya jumapili hii tatu inaleta mwaliko kwa furaha kwa sababu ya ukaribu wa ujio
wa Bwana wetu. Hali hii tunaweza kutambua kupitia ujumbe wa nabii Sefania
ambaye waliwahamasisha waisraeli wafurahi na kumshangilia Mungu mfalme wao.
Maana ya furaha kubwa ni kwa sababu uwepo wa Mungu katikati yao ulileta
ukombozi ukidhamini usalama na ulinzi dhidi ya maadui yao. Ujumbe wa furaha
unaendelea pia kupitia waraka wa Paulo kwa Wafilipi kwa sababu Mungu yu karibu
na neno lake ni alama ya ukaribu wake. Ukaribu wa Mungu ni uwepo wake kwa
wakati sawa na uwepo wake ni ufanisi, yaani ni nafasi ya wokovu.
Kuhusu
injili tuna vipengele vingi kwa kutafakari kwetu. Andiko hili ni mwendelezo wa
injili ya jumapili iliyopita. Luka anaendelea kueleza kuhusu kazi ya Yohane
Mbatizaji na kipengele cha kwanza ni kuhusu uwezo wa Yohana wa kuwathibitishia
wasikilizaji wake. Kama ilitokea na manabii wa zamani, tunaamini kwamba uwezo
huu unatokana na uzoefu wa kweli wa Neno la Mungu. Yohane alifikiwa na Neno la
Mungu jangwani. Yeye aliishi katika upweke wa jangwa, aliyefunguliwa kabisa kwa msukumo wa
Mungu. Alijifunza kutokana na Neno la Mungu jinsi ya kuwa shahidi wa habari
njema ya wokovu. Miongoni mwa wasikilijazi wa Yohane, Luka anawataja watoza
ushuru na askari ambao walitaka kubatizwa. Hasa watoza ushuru walichukiwa na
Wayahudi wenzao kwa sababu walikuwa washirika wa Roma. Wakati wa Yesu, watoza
ushuru waliwekwa katika kundi maalum la wenye dhambi. Kuchanganyika nao
kulimfanya mtu apate dhambi yao pia. Yesu alichanganyika nao, akivuka mipaka
iliyowekwa na watu. Kikundi hiki pamoja na askari walitambua ukweli wa hali yao
na hivyo wakaomba msamaha. Lakini nia njema pekee haitoshi. Yohane anawataka
watende haki. Kwa hivyo aliwaalika
washiriki mali yao.
Ukuu wa Yohane Mbatizaji
ulikuwa kutambua ukuu wa Bwana, akijifikiria mwenyewe kama sauti tu na
asiyestahili kuulegeza ukanda wa viatu vyake. Yesu mwenyewe alitambua ukuu wa Yohane akiweka
unyenyekevu wake kama rejea. Hatuhitaji kumlinganisha Yesu na Yohane Mbatizaji
ili tugundue ni nani kati yao ni mtu mkuu. Bila shaka Yesu ni mkubwa zaidi
kuliko Yohane. Lakini ni vizuri sana kutambua uhusiano huu wa ajabu kati ya
wote wawili. Ikiwa Yohane anaongea kuhusu Yesu anamsifu; ikiwa Yesu anaongea
kuhusu Yohana anafanya vivyo hivyo. Tunahitaji kujifunza sana kutokana na uhusiano
huu, kwa manufaa ya Kanisa na kwa wema wa uhusiano wetu kama wakristo,
watumishi wa mwili wa Bwana.
Basi,
ni kazi ya Yohane kutangaza mwisho wa wakati wa kumgojea Masiya na mwanzo wa
historia mpya, ambayo ilifanywa na watu wapya waliofanywa upya katika Roho wa
Kristo. Kama huu ni uzoefu wa ubatizo. Lakini ni lazima kukumbuka baadhi ya
tofauti kati ya ubatizo uliotolewa na Yohane na ule atakaotoa Masiya. Yohana
aliwabatiza watu kwa maji kama kielelezo cha kugeuka kwao. Uzoefu huu ulikuwa
hatua muhimu, bali haikufikia mabadiliko kamili ya ndani. Ubatizo wa Roho
Mtakatifu na moto una nguvu ya kufanya mabadiliko kwa sababu unamfanya mtu
kuzaliwa katika familia ya Mungu. Alama yetu kama watoto wa Mungu haiwezi
kufutika. Hii ni chapa ya ubatizo wetu. Ipo daima!
Wakati
wa Yohane Mbatizaji unaomhusu Kristo ni mwendelezo, lakini unaushinda wakati wa
maandalizi wa zamani. Huu ni wakati wa kutangaza kuhusu mahitaji ya
kumkaribisha Bwana aliyetaka kukutana na binadamu. Basi kwa upande wa Mungu,
mwendo wa mkutano uko tayari. Kwa upande wa binadamu ni lazima imani na
kukubalika kwa uhuru na binafsi. Ikiwa ukuu wa Yohana ulikuwa kutambua ukuu wa
Bwana, ukuu wa kila mtu katika ufalme wa Mungu ni kuyakubali mapendekezo ya
Yesu na kuzifuata nyayo zake. Kielelezo cha Yohane kiwe daima rejea kwa safari
yetu ya kukubalika kwa mipango ya Mungu na kuutangaza wakati wa kutembelea
kwake kwetu daima.
Fr Ndega
Nenhum comentário:
Postar um comentário