Kutafakari
kuhusu 5,2-4; Waebrania 10, 5-10; Luka 1:39-45
Liturujia ya jumapili hii inatujulisha mtu muhimu sana kama
kielelezo cha matayarisho na makaribisho kwa Yule atakayekuja, yaani Bikira
Maria. Mkutano wake na dada yake Elizabeti ni alama ya mambo makuu ya Mungu
ambaye ana mtazamo maalum kwa hali ya wanyenyekevu na maskini. Kutokana na hali
hii alidhihirisha fumbo la mapenzi yake. Anawatumia waliopatikana ili mipango
yake yatimize. Katika somo la kwanza nabii Mika anatangaza kuzaliwa kwa
mkombozi mmoja kwa Waisraeli atakayetawala milele kwa nguvu za Bwana. Yeye ni
mfano wa mwokozi wetu Yesu Kristo aliyekuja kwa ajili ya ulimwengu wote akifanya
mapenzi ya Mungu, kulingana na ujumbe wa Waraka kwa Waebrania. Kupitia
kujisalimisha kwake mara moja tu tumepata utakaso na wokovu.
Alipoelewa mpango wa Mungu katika maisha yake Maria
alijibu: “Mimi ni mjakazi wa Bwana, nitendewe kulingana na neno lako”. Hili
lilikuwa jibu la ajabu la Bikira Maria mbele ya tangazo la Malaika Gabrieli. Wito
wa Maria ni maonyesho ya ukarimu wa Mungu. Ukarimu wa Bwana ulihamasisha ukarimu
wa mtumishi wake aliyeenda kwa haraka kutembelea dada yake Elisabeti ambaye pia
alikuwa amepata mimba na alikaribia kuzaa kwani ilibaki miezi mitatu. Mkutano
wa wanawake wawili ni mkutano wa agano, yaani Agano la Kale linalikaribisha
Agano Jipya. Kuna pia mkutano wa vizazi, yaani mzee anamkaribisha kijana na
kijana anamtumikia mzee. Mpango wa Mungu unajumuisha vizazi vyote na kila
kizazi kinaalikwa kuchukua ujumbe wake kulingana na mwendo wake wenyewe. Tukio
hili la wanawake hawa wawili linaonyesha njia maalum ya Mungu ya kutenda, dhidi
ya matarajio ya binadamu, ni kwamba, mwanamke asiyezaa anakuwa mwenye rutuba na
mwanamke bikira anapata mimba kwa njia ya ajabu.
Maria alitaka kushiriki furaha ya Elizabeti kwa kuwa
Mungu alikuwa ameingia katika maisha yake. Elizabeti na Yohana Mbatizaji ambaye
alikuwa bado hajazaliwa wanashiriki pia furaha ya Maria na Yesu ambaye
hajazaliwa. Wanawake wawili kukutana, watoto wao pia wanakutana. Maria anatukumbusha
kwamba ni lazima kuondoka na kuenda kukutana na wengine na kuyatambua matendo
ya Mungu maishani mwao. Maria anatusaidia kuamini kwamba matendo makuu ya Mungu
katika historia ni ishara ya uaminifu wake. Tunaalikwa kuchukua ahadi ya
kuondoka na kuenda kwa wengine kuona walivyobarikiwa na Mungu. Wengi wanangojea
kutembelea kwetu na mshikamano wetu. Kwa kufanya hivyo tunahitaji kushinda
baadhi ya vikwazo vinavyotuzuia kushirikiana na baadhi ya watu katika jamii au
kabila jingine.
Basi, ni mwenye furaha aliyeamini katika ahadi ya Mungu,
kwa maana Yule anayeahidi ni mwaminifu. Imani inakuwa kigezo/kipimo cha msingi
wa furaha. Maria anakuwa ishara ya ubinadamu mpya, uliobadilishwa na kuokolewa
na Mwanae. Maria ni mmoja wetu ambaye alijihisi aliyeangaliwa kwa huruma na
akaishi kwa shukrani. Aliyeangaliwa kwa huruma kwa sababu Mungu alitenda makuu
maishani mwake. Yeye aliishi kwa shukrani kwa sababu aliyapatikana maisha yake
ili, kupitia jibu lake, Mungu atende makuu maishani mwa watu hasa maskini. Kwa
kiwangu kidogo sisi pia tunapitia tabia hizi, ni kwamba, tumeangaliwa kwa
huruma kupitia zawadi kubwa ya wito. Tabia ya shukrani ndani yetu inaonyeshwa nje
kupitia utumishi kwa furaha na ukarimu. Hali ya kuwa walioangaliwa kwa huruma
haitutegemei sisi, bali inamtegemea Mungu ambaye anatujalia baraka nyingi; hali
ya kuwa kama walio na shukrani inatutegemea sisi peke yetu. Mbele ya majaribio
ya kufa moyo au kukata tamaa Maria ni kielelezo kwetu kwa upatikanaji kabisa kwa
mipango ya Mungu. Kama yeye tunaalikwa pia kuishi kama wamebarikiwa na kumchukwa
Yesu kwa wengine katika mahali po pote tuendako.
Fr Ndega
Mapitio: Sara
Nenhum comentário:
Postar um comentário