sexta-feira, 8 de julho de 2022

NINAWEZAJE KUWA JIRANI?

 

Kutafakari kuhusu Lk 10, 25-37


 



 

    Katika injili ya siku ya leo mwanasheria alimwendea Yesu na alimwuliza maswali mawili, yaani la kwanza “nifanye nini ili niurithi uzima wa milele?”; na la pili, “Jirani yangu ni nani?” kuhusu swali la kwanza Yesu alimsaidia kugundua tena umuhimu wa sheria, yaani “kumpenda Mungu na kumpenda jirani”. Amri ya Kumpenda Mungu tunapata katika kitabu cha Kumbukumbu la Sheria (6:5) na ya Kumpenda jirani inapatikana katika kitabu cha Walawi (19:18). Ikiwa Yesu alimwambia mwanasheria kwamba yatosha kutenda hivyo ili apate uzima wa milele ni kwa sababu “Torati yaonyesha njia ya uzima wa milele ikiwa mtu anampenda Mungu na jirani yake.”

    Katika Agano la Kale Mungu alianzisha Agano na Watu wa Israeli akiwafanya wana wake. Kama ishara halisi ya Agano hili tuko na Amri kumi ambazo zinalenga ushusiano mwema na Mungu na jirani. Lakini, kulingana na mawazo yao ya kiyahudi, jirani siyo yule ambaye anaishi karibu nao bali ndiye yule aliye na uhusiano wa damu nao. Basi, wageni hawawezi kuwa jirani kwao. Hivi mawazo haya yawazuia kuwa na uhusiano mwema hasa na Wasamaria waliofahamiwa kama maadui wao kwa sababu waliichangamana damu yao na ya wageni.

    Kupitia swali la pili, yaani “Jirani yangu ni nani?” mwanasheria alitarajia Yesu akubaliane na mawazo haya ya kivuo. Lakini Yesu alisimulia mfano wa Msamaria Mwema. Kulingana na mfano huu mtu mmoja alishuka toka Yerusalemu kwenda Yeriko na kushambuliwa na wanyang’anyi ambao walimwacha karibu na kufa. Wote wawili, yaani kuhani na Mlawi walipomwona mtu walipita kando lakini Msamaria alipomwona mtu alimwonea huruma na kumsaidia. Wawili wa kwanza  ni ishara ya wale ambao wanapaswa kuitii sheria, na kulingana na sheria hii, hawawezi kugusa ama kuguswa na “kitu kichafu”. Walitumia njia nyingine kwa sababu kuwa karibu na mtu yule aliye na haja ya msaada kungewazuia kumsifu na kumtumikia Mungu kamili. Walisahau kwamba “ni jambo baya kutofanya mazuri kwa kutumia jina la Mungu au la dini”.

    Kwa sababu ya sheria ya utakaso wawili wa kwanza walidharau yule aliye mwenzao kushindwa kuonyesha ujirani. Kupitia tabia yake ya huruma, “Msamaria alionyesha ujirani mwema” kwa sababu hakuhitaji kuitii sheria ya utakaso. “Msamaria mwema hakujifikiria mwenyewe, alimfikiria mwingine.” Kupitia mfano huu Yesu anaonyesha kuwa swali la msingi sio “ni nani jirani yangu?,” bali ninawezaje kuwa jirani kwa mwenzangu?” Yesu anasahihisha mtazamo kuhusu jirani na kuonyesha kuwa upendo wa kweli kwa Mungu unatokea pamoja na kushiriki katika maisha ya wale anaowapenda hasa walio na shida.

    Kwa Yesu, upendo wa kweli unaonyeshwa kupitia ishara za upole na huruma. Yesu mwenyewe ni Msamaria Mwema kwa namna ya kipekee ambaye alichukua hali yetu na kuponya majeraha yetu ya dhambi. Tena anajitambulisha na wale ambao “wameanguka kando ya njia za maisha”. Je, tunaweza kutambua uwepo wake Kristo katika watu ambao kwa kawaida tunakutana na hao ambao wanauomba msaada wetu? Kumwabudu Mungu kwa kweli kunatokea kupitia uhusiano mwema na ufanisi na wengine. Kusherehekea Ekaristi ni alama ya undugu ikiwa undugu uko miongoni mwetu, vinginevyo, sio Mwili na Damu ya Kristo tunayosherehekea. Haiwezekani kufanya uhusiano wa kweli na Mungu wakati tunapowasahau wenzetu katika mahitaji yao.

     Hatuwezi kuishi kwa kutojali kuhusu hali ya wengine kama ilivyotokea kwa Kaini, yaani “Je mimi ni mlinzi wa ndugu yangu?” (Mw 4:9). Hali hii ni kutojali iliyo njia ya kukanusha utambulisho wetu wa Wakristo. Sihitaji kujua ni nani jirani yangu ili nimpende na kumsaidia. Nimekuwa mwanafunzi wa Kristo ili kuwa jirani wa wote ka ma Kristo alivyo. Kumpenda jirani ni kumsaidia kushinda hali mbaya ya maisha yake. Kwa upande wetu tulio Wakristo, jirani ni yule tunayomgundua kama aliye na haja nasi twamua kuwa jirani kwake kwa kuandamana naye kumhakikishia maisha ya heshima hata ikiwa mwendo huu unapodai tutumie muda wetu na rasilimali zetu. Neema ya Bwana itusaidie kutenda kama “msamaria mwema”.


Fr Ndega

Nenhum comentário: