sábado, 2 de julho de 2022

FURAHA ISIYOKATISHA TAMAA

 

Tafakari kuhusu Is 66: 10-14; Gal 6: 14-18; Lk 10: 1-12




     Muhtasari wa ujumbe wa maandiko haya ni uhakika kwamba sisi hatuko tu kwenye utume bali pia sisi ni utume hapa duniani. Si sifa yetu bali ni uzuri na ukarimu wa yule aliyetuita na kututuma kwa ajili ya wokovu wetu na wa wengine. Kuwa mmisionari ni kuitwa kwa furaha ambayo inautegemea uaminifu kwa Mungu mwaminifu. “Yeye anataka kuuanzisha moyo wa Mwana wake ndani yetu” na kwa ajili ya hilo anataka tupatikane na tuwe wakarimu.

    Akitumia lugha ya mama, Isaya anatoa mwaliko wa furaha kwa sababu ya kile ambacho Bwana anakaribia kutimiza katika maisha ya watu wake. Uwepo wa kudumu wa Mungu katikati ya watu wake hushinda nyakati za usumbufu na kukatishwa tamaa kwa kufungua nafasi za matumaini na furaha hata kama kila kitu kinaonekana kupotea. Kama watu hawa, sisi pia tunaombwa kuwa na imani isiyochoka katika utendaji wa Bwana kwa sababu Yule anayeahidi ni mwaminifu daima.

    Somo la pili linatoa mabishano makubwa: baadhi ya Wakristo wa Kiyahudi, ambao bado waliendelea kushikamana na mila zao za Kiyahudi, walitaka kuwalazimisha wapagani kutahiriwa kama wao. Kwa sababu hii Paulo anasema kwamba tukihukumu hivyo tunaufanya msalaba wa Kristo kuwa bure. Kwa njia ya msalaba Kristo alishinda kifo nao ulimwengu wa kale pia ulisulubiwa! Sisi ni viumbe wapya. Ni jukumu letu kuishi kama wamefufuka, tukiacha tabia za zamani, mawazo ya zamani, kila kitu ambacho kinapingana na hali yetu mpya.

    Kifungu cha Injili kinatujulisha kwamba Yesu pamoja na mitume kumi na miwili tena aliita na kuwatuma watu wengine 72 ili kuinjilisha. Nambari hii, katika Agano la Kale ilikuwa ishara ya jumla ya mataifa na kumaanisha utume wa ulimwenguni kote, yaani, kuinjilisha sio tu kazi ya mapadre na watawa bali inahusisha kila mtu anayebatizwa. Yesu anawatuma wawili-wawili, akiweka uzoefu na uhusiano wa jumuiya kama rejeo la shughuli zao. Utume ni ahadi ambayo mtu achukua sio peke yake. Tunahitaji msaada wa jumuyia kwa mafanikio ya kazi yetu ya kuinjilisha.

    Wanafunzi wanapaswa wawe watu wa sala kama tukio la msingi, yaani, kama msingi unaodumisha jengo la kuwepo kwao. Ni lazima wafahamu kwamba mavuno yana bwana wake, yaani Baba mwema na mkarimu, ambaye anajua mahitaji ya watoto wake kabla ya amwombe chochote. Akitumia neno mavuno, Yesu anataja umuhimu wa kuthamini kila mahali tunapofika kwa sababu Roho Mtakatifu ametutangulia kwa mbegu za Neno la milele. Kwa hiyo, mtu hatoki nje ya bustani yake kuelekea jangwani mwa wengine, bali aenda kutoka bustani moja hadi nyingine.

    Mungu hahitaji maombi yetu; ni sisi tunaohitaji kuomba kwa sababu tunapoomba tunakua katika ufahamu wa kuwa watoto na wanafunzi wanaopendwa sana; tunakuwa vile tulivyo kwa wito. Wanafunzi ni kama wana-kondoo katikati ya mbwa-mwitu, kwa sababu wameitwa kumwilisha utambulisho wa Mwana-Kondoo wa kweli, Yeye anayeondoa dhambi za ulimwengu kwa sababu anaweza kutoa maisha yake kwa ajili ya rafiki zake. Ni katika utambulisho huu - wa upendo, wa kujitolea - kwamba maisha yao yanapata maana yake ya kweli. Kuinjilisha ni kujitolea.

    Miongoni mwa mahangaiko ya Yesu pia kuna tatizo la miliki ambayo tunaitegemea sana kwa ajili ya kufanya baadhi ya shughuli. Yesu anatuomba busara, unyenyekevu, kujitenga na usalama hio wa uwongo ambao mara nyingi zinaelekea kuchukua nafasi ya Mungu maishani mwetu. Amini kwa Riziki takatifu ya Mungu ni tabia ya msingi ya mmisionari wa kweli na inakuwa tangazo la kinabii la upendo na utunzaji wa Mungu kwa watoto wake. Kuishi katika wingi wa mali kunahatarisha uaminifu wa ujumbe tunaotangaza kwa kuwa kikwazo kwa imani ya wengine.

     Wanafunzi wanarudi wakiwa wamejawa na furaha kwa sababu walipata mafanikio katika utume, hasa kuelekea pepo waliojisalimisha kwao kwa sababu ya jina la Yesu. Lakini bwana aliwaomba wawe macho kwa aina hii ya furaha inayoweza kutudanganya. Furaha ya kweli haitokani na mafanikio kwa kazi iliyofanywa au kuwa maarufu katika ulimwengu huu. Utukufu wa dunia hii hudumu sana. Furaha ya kweli ni kukaribishwa na Baba kama watoto wapendwa na kushiriki katika utume wa Mwana, kwa kupokea uhai wake mwenyewe. Tuweze kupata kufanana na maisha ya Yule ambaye tumeitwa kumtangaza kwa maisha kabla kwa maneno.


Fr Ndega

Nenhum comentário: