sábado, 28 de novembro de 2020

MATARAJIO YA FURAHA NA MAKINI

 

Kutafakari kuhusu Isaya 63: 16-17; 64: 1, 4-8; 1Wak 1, 3-9; Mk 13: 33-37

 

Kulingana na liturjia ya Kanisa Katoliki, tunaanza wakati mpya uitwao Majilio. Wakati huu unajumuisha wiki nne: wiki mbili za kwanza tunatafakari kuhusu kuja kwa Bwana mara ya pili katika mwisho wa umri. Ujio wake kama Bwana wa maisha yetu na wa historia unalenga kuimarisha matumaini yetu ili kushiriki katika furaha yake. Wiki mbili zingine zinatukumbusha Ujio wa kwanza wa Yesu na kutuandaa ili tusherehekee sikukuu ya kuzaliwa kwake katika Krismasi.

Masomo ya leo ndio mwaliko wa kukesha ili tutambue na kuzikaribisha ishara za uwepo wa Bwana katika hali yetu ya kila siku. Ndio mwaliko pia wa shukrani maana Bwana anakuja kukutana nasi daima ili kutupa wokovu wake. Matukio yote makuu yahitaji maandalizi mema na ndani ili kusherehekewa mema. Hivyo ndivyo Majilio kama maandalizi ya tukio kuu la Krismasi.

Katika somo la kwanza, nabii Isaya anamwomba Mungu kwa njia ya imani na upendo, akimtambua kama Baba. Nabii huyo anaongea kwa kutambua vipengele viwili: kwanza, uaminifu wa Mungu anayewaokoa watu wake na kingine ni kosa la uaminifu wa watu kwa ajili ya Agano. Upinzani dhidi ya maongozi ya waliotumwa na Mungu uliwafanya watu wajione mbali na Mungu. Maombi ya nabii ni faraja na msaada ili kufufua matumaini katika Bwana ambaye yuko tayari kutoa nafasi mpya kwa yeyote anayetaka kumrudia yeye. Tuchukue nafasi hii inayotupwa.

Katika somo la pili, Paulo anamshukuru Mungu, kwa sababu ya tendo la neema yake katika jumuiya ya Wakorintho, ambayo imezaa matunda mazuri kama jibu la tendo hili. Jumuiya hii inatarajia ujio wa Bwana sio kwa njia yoyote bali kwa imani halisi iliyo maonyesho ya ahadi yao kwa karama ilizopokea. Matakwa ya Mtakatifu Paulo ni kwamba jumuiya hii iendelee kwa imara katika ujumbe uliotolewa kuhusu Yesu na kukua kwa imani kwake anayeaminika.

Katika Injili Yesu anaongelea fumbo la Kuja kwake. Ni sehemu ya mpango wa hekima na wema wa Baba. Hii ni nafasi ya wokovu na sio ya hofu. Wokovu ni zawadi ya Mungu; hakuna hata mmoja anayeustahili. Sote tunaalikwa kukesha. Yesu analinganisha ujio wake na mfano wa mtu ambaye alifunga safari na kuikabidhi nyumba yake kwa watumishi wake. Kila mmoja alipokea jukumu fulani na wote waliombwa kukesha. Hapo ni muhimu kipengele cha wakati. 

Kulingana na lugha ya Kigiriki wakati ndio Kronos na Kairos. Neno ambalo andiko hili linatumia ndilo Kairos linalomaanisha wakati mwafaka, nafasi ambayo Bwana anatupa ili tuwe wenye furaha. Tunaalikwa ni watumishi na katika biblia, watumishi ni wale waliotoa maisha yao kwa ajili ya mpango wa Mungu. Bwana alitukabidhi mpango wake ili tuutekeleze maishani mwetu na jamii yetu. Yeye anatarajia tutende jukumu hili kwa uaminifu kwa sababu anataka kukutana nasi ili kutuzawadisha kwa kushiriki naye furaha yake.

Anatarajia kukaribishwa vizuri, kulingana na maneno yake mwenyewe: "Mimi nasimama mlangoni na kubisha hodi. Mtu akisikia sauti yangu na kufungua mlango, nitaingia nyumbani kwake na kula chakula pamoja naye, naye atakula pamoja nami” (Apocalypse 3, 20). Kulingana na andiko hili Bwana Yesu atakuja usiku, yaani kama mwanga ili kufukuza giza, huzuni na kuanzisha hali mpya kabisa maishani mwetu. Turuhusu kuangazwa na mwanga wake.

 Kuja kwake Bwana badala ya kuwaogopesha watu, kunayaimarisha matumaini katika wokovu wake, kwa sababu yeye ni Mwokozi na kuja ili kuokoa. Safari ya Kikristo ni safari ya furaha ili kukutana naye kwa sababu yeye huja daima kukutana na sisi. Maonyesho halisi ya makaribisho yetu kwa Bwana ndio utumishi wetu katika jumuiya kwa ukarimu na furaha.

Hivyo, Majilio ni wakati wa kufanya upya ahadi yetu na Bwana, katika mwendo wa mabadiliko daima. Kuhusu hili, Bwana anatuambia tena: "Wewe unayo saburi, umestahimili taabu nyingi kwa ajili ya jina langu, wala hukuvunjika moyo. Lakini ninalo jambo moja dhidi yako: wewe hunipendi tena sasa kama pale awali. Basi, pakumbuke pale ulipokuwa kabla ya kuanguka, ukatubu na kufanya kama ulivyofanya pale awali” (Ufu 2, 3-5a). Kusali zaidi na kupatikana ni tabia za mwanafunzi wa kweli anayejua Bwana wake naye uko tayari daima ili kumkaribisha. Kukesha kwa uaminifu na ukarimu ni ishara halisi ya matarajio yetu kwa ujio wa Bwana.


Fr Ndega

Nenhum comentário: