sábado, 16 de maio de 2020

KUPENDA KAMA IPASAVYO



Kutafakari kutoka Mdo 8,5-8.14--17; 1Pt 3,15-18; Yoh 14, 15-21



       Kutoka maandiko haya tunaanza kuongea kuhusu nafsi na kazi ya Roho Mtakatifu aliye upendo wa Baba na Mwana ametolewa ili aandamane na kazi ya jumuiya ya wanafunzi ili wapate kujua kamili kuhusu ufunuo wa Mwalimu wao kuwa ufanisi katika ushuhuda wao hata kati ya dhiki.

     Kulingana na somo la kwanza baada ya mateso dhidi ya Kanisa katika Yerusalemu, watumishi wengi walikimbilia maeneo mengine ili kuinjilisha. Kwa sababu ya kazi nzuri ya Filipi kwenye Samaria Wasamaria wengi walikaribisha neno la Mungu kwa furaha kubwa. Ishara za ajabu alizotenda Filipi zilithibitisha ukweli wa maneno yake. Pedro na Yohana walifunga safari kutoka Yerusalemu kwenye Samaria ili kukutana na Filipi na kumsaidia kama ishara ya ushirika na wa Kanisa zima, linaloongozwa na Roho Mtakatifu, limejaa matunda mengi kwa wokovu wa watu.

      Uinjilisti hauna mipaka na kulenga kuondoa ukuta wa utengo ambao hugawanya watu. Kazi hii inaimarishwa na Roho Mtakatifu aliyetolewa sio kwa uzoefu umefungwa wa kikundi kimoja tu bali ni zawadi kwa wote. Kupitia yeye waliomfuata Yesu wako tayari daima “kumjibu kila mtu awaulizaye habari za tumaini lililo ndani yao”. Lakini hii ndiyo kazi ya kufanywa kwa upole na heshima ili mapenzi ya Mungu yakafanyike. Wamisionari ni vyombo tu. Kweli ndiye Mungu mwenyewe anayefanya kazi kwa Roho wake akisababisha mabadiliko na furaha kubwa maishani mwa watu.  

     Katika injili tunaendelea na hotuba ya mwisho ya Yesu. Yeye aliongea na wanafunzi wake moyo kwa moyo, akionyesha hisia zake za ndani kwa ajili yao. Hotuba hii inadhihirisha uhusiano wa ndani kati ya Yesu na Baba na pendekezo lake kwa wanafunzi wake ili waweze kuwa ufanisi katika utume wao.  Aliposema, “mkinipenda, mtazishika amri zangu,” aliwaomba ahadi kwa ajili ya mafundisho yake, yaani Neno lake. “Neno haliwezi kupunguzwa kuwa amri, hilo ndilo zaidi ya amri. Neno linafanya kazi ndani yenu mnaoamini (1Ts 2, 13), linaumba, linazalisha, linawasha, linaufungua upeo, linaziangazia hatua, linapanda uhai mashambani mwa maisha.”

     Ugumu wa kufahamu maana ya ndani ya mafundisho ya Mwalimu na kosa la ushirika kwa hisia zake (“Ikiwa mngalinipenda mngalifurahi...” – Yoh 14, 28) linafanya moyo yao uwe na huzuni. Kisha, Yesu kama kawaida anawasaidia kwa sababu ya magumu yao na kuwaimarisha kwa kuongelea ujio wa Roho Mtakatifu maishani mwao. Roho huyo atatenda kama Msaidizi kwa sababu ana jukumu la kutia moyo, kulinda, kufanya maombezi kwa ajili yao.

    Lakini andiko linampa Roho Mtakatifu maneno ya “Msaidizi mwingine”, kweli ni kwa sababu ndiye Yesu Msaidizi wa Kwanza. Tendo la Roho litawaongoza hadi kuelewa kamili mambo yote Yesu aliyoyatenda na kuyafundisha kama maonyesho ya upendo wake kwa hiari na kwa jumla ili kwa kupitia uzoefu wa kupendana wao kwa wao waweze kuuonyesha uwepo wa Yesu kwa wengine. Hivyo, Roho anatenda ili Yesu akae ndani yao nao upendo wao unamwonyesha kwa wengine.

    Tunaishi katika ulimwengu ambao upendo umepoteza maana yake ya kiasili, yaani mtu anasema, ninapenda ikiwa naweza kuchukua nafasi juu ya mwingine” ama “napenda mpaka wakati fulani” ama “nawapenda baadhi ya watu tu, lakini sipendi wengine”. Yesu anatuzungumzia sisi kuhusu upendo tofauti; ndio upendo wa kweli. Ukweli wa upendo wa mtu unaonyeswa na uwezo wa kujitolea na kutumikia bila kufanya ubaguzi wa watu. Mtu anayependa kweli anataka tu manufaa ya mtu anayempendwa. Ndio kwa upendo huu ambao Yesu anatualika siku ya leo nao ndio upendo huu unaotufanya kuwa wenye uhuru na watu wa kweli.  

     Kumpenda Yesu kama anataka ni zawadi ambayo tunapewa kupitia kulisikiliza Neno kwa uaminifu na kwa uvumilivu. Kupitia Neno na tendo la Roho, Mungu Baba anafanya ndani yetu moyo wa Mwanawe ili tupende kama Yeye. Huu sio upendo ambao unaniongoza kufanya lile ambalo linanipendeza tu bali unaniwezesha kujisalimisha kwa ajili ya wengine. Ndio upendo ambao unatufanya kuacha ubinafsi wetu na kuenda kukutana na wengine katika mahitaji yao. Huu ni upendo ambao unafanya kazi yetu iwe ufanisi daima naye Roho Mtakatifu peke yake anayeweza kuuimarisha upendo huu mioyoni mwetu. Kwa hivyo, tuombe kwa amini, uje Roho Mtakatifu na kutufundisha kumpenda Yesu kama inavyopaswa!  

Fr Ndega

Nenhum comentário: