sábado, 2 de maio de 2020

YULE ANAYEPENDA ANATUNZA



Matendo 2, 14a.36-41; 1Pt 2,20b-25; Yoh 10,1-10



    Tunaadhimisha Jumapili ya Mchungaji mwema na Jumapili ya miito. Jumapili hii inatualika kumshukuru Mungu kwa zawadi kuu ya wito na kumwomba aendelee kulibariki Kanisa lake kwa miito mingi. Pendekezo la Jumapili hili linatoka kwa Baba Mtakatifu Paulo wa VI. Yeye alilialika Kanisa zima kuchukua ahadi kwa ajili ya wito. Maombi kwa ajili ya miito ni pia utii kwa mwaliko wa Yesu ili tuombe kwa mwenye mavuno ili atume wafanyakazi kwa mavuno yake kwa sababu mavuno ni makubwa, lakini wafanyakazi ni wachache (cf. Mt 10, 37-38). Wito ni zawadi ya Mungu na ubatizo ni chemchemi yake na familia ni mwanzo. Mungu anayemwalika kila mtu hutarajia jibu kwa ukarimu kutoka kwa anayealikwa.    

       Katika somo la kwanza mitume wanatangaza kwa shauku fumbo la pasaka ya Kristo kwa nguvu wa Mungu, kama mwaliko wa mabadiliko ya maisha. Nguvu ya maneno yao yalitoka kwa Roho Mtakatifu akitenda maishani mwao na kusababisha kutubu. Kwao kila kipindi kilikuwa nafasi mpya ya kushuhudia maisha mapya aliyotoa Yesu kwa wote hata “kwa ajili ya wanaokaa mbali na kwa ajili ya kila mtu ambaye Bwana Mungu wetu atamwita kwake”. Hakuna hata mmoja anayekaa nje ya pendekezo hilo la uokovu.

      Kulingana na Mtakatifu Petro, Mungu hapendezwi na mateso ya watu bali anapendezwa na tabia ya uvumilivu ya mtu mbele ya mateso. Ndiye Kristo ukamilifu wa ahadi za Mungu na kupitia yeye watu wana uhakika wa kupata wokovu. Yeye ametufanya kuwa watoto wa Mungu naye kututunza sisi kama anavyofanya mchungaji na kondoo wake. Tukiufuata mfano tufanye vivyo hivyo kwa ajili ya wengine.

        Katika injili, Yesu anajifunua kama Mchungaji na mlango wa kondoo. Yeye anavitumia vitenzi kama kujua, kuita, kusikiliza, kufuata, kuongoza na kutoa kwa ajili ya kuongelea tofauti kati yake na wale waliokuja kabla yake. Yesu ndiye Mchungaji Mwema kwa sababu anawapenda wana kondoo wake. Utayari wake wa kufa kwa ajili yao ni maonyesho ya upendo huu. Anawajua wana kondoo wake na kuwaalika kuisikiliza sauti yake ambayo yanawaongoza kupata ukamilifu wa maisha yao.

       Akitumia mfano huu Yesu anataka kuongelea uhusiano kati yake na wanafunzi wake. Msingi wa uhusiano huu ni amini, upendo, upole nao unasababisha maisha kamili kwa wafuasi wake. Kama yeye anawajua wana kondoo wake, anatarajia kwamba wako tayari kumjua na kuyafuata mafundisho yake. Kosa la kujua njia na sauti ya mchungaji ni hatari kwa sababu linaweza kusababisha mgawanyiko wa kundi na hasara ya utambulisho wa mfuasi. Njia ya Yesu ya kuongoza na kutunza ni kipimo cha walio na jukumu la kuwaongoza watu.

       Yesu ni mlango wa uhusiano mwema kati ya watu na Mungu. Mlango huu unamaanisha vipengele vitatu. Cha kwanza, Yesu ndiye njia inayotuongoza kwa Baba; nafsi yake inatuhakikishia mkutano na Mungu. Cha pili, Yesu ndiye ukweli wa Mungu kwa binadamu na ukweli wote wa binadamu kwa Mungu; “kila mtu wa ukweli humsikiliza” (Yoh 18,37) na kuruhusu kuongozwa naye kwa ajili ya kupata ukweli kamili. Yesu ndiye uhai unaotolewa kwa hiari na kwa wingi kwa wote.

       Katika Yesu aliye Mchungaji Mwema, Mungu anaonyesha ulinzi na utunzaji wake kwa ajili ya watu wake. Upinzani dhidi ya sauti ya Yesu ni upinzani wa kuyafanya mapenzi ya Mungu na kuishi uhusiano wa upendo naye. Jibu yeye analotarajia kwa mwaliko wake siku hizi ndio uangalifu kwa msukumo wake ili tuweze kutenda kwa hekima katika maamuzi yote tunayopaswa kuchukua.

      Yesu ni mchungaji mwema na ahadi yetu kama kondoo wake ni kusikiliza sauti yake, yaani kuyafuata mafundisho yake. Wito wetu unapata mafanikio yake wakati tunaweza kuitambua sauti ya Bwana kati ya sauti nyingi zinazojaribu kutuongoza. Kupitia neno lake, sakramenti na mafundisho ya wachungaji wetu Mchungaji Mwema Yesu anaendelea kuwaongoza na kuimarisha kundi lake. Tunaalikwa kuruhusu kuongozwa kwa roho ya upole na ushirika. Hata sisi pia kupitia ubatizo tuko na jukumu la kuwaongoza wengine kwa kuwasaidia wachungaji wetu wafanye kazi yao vizuri. Tunaalikwa kutenda kama wanafunzi wa kwanza, ambao waliuchukua wito kwa furaha na kwa hamu kwa manufaa ya Watu wa Mungu na kundi la Yesu.

Fr Ndega

Nenhum comentário: