domingo, 22 de outubro de 2017

SISI TU MALI YA MUNGU


Kutafakari kuhusu Is 45: 1,4-6; 1 Thes 1: 1-5; Mt 22: 15-22

Maandiko haya yatualika kutafakari kuhusu vipengele viwili vya msingi: cha kwanza, ni kuhusu hisia yetu ya kuwa mali ya Mungu kama wana wa watu wake; cha pili, ni kuhusu jukumu letu katika maendeleo ya Taifa letu kwa kupitia malipo ya kodi halali. Kama Wakristo, tunakiri umuhimu ya kodi, lakini tunajua pia kuwa kodi ama pesa sio rejeo la maisha, ni msaada tu. Hatutaki ichukue nafasi ya Mungu maishani mwetu.
Somo la Kwanza ni mtazamo wa imani kuhusu ushindi wa Koreshi, mfalme wa Uajemi, ambaye aliwakomboa Wayahudi kutoka mamlaka ya Babeli. Kulingana na Isaya, ushindi wote wa Koreshi haukuwa uwezo wake, bali tendo la Mungu ambaye alimchagua Koreshi kama mjumbe wake ili kufanya Jina la Bwana lijulikane kwa Mataifa yote na kuyaalika kumwamini Mungu. Ingawa Koreshi alikuwa mfalme ambaye hakumjua Mungu wa Israel, alichaguliwa kwa ajili ya kuwa ni chombo cha ukombozi. Wayahudi waliweza kurudi nyumbani na kuishi utambulisho wao kama Watu wa Mungu kwa uhuru kabisa.
Paulo na wenzake wa kuinjilisha wanatambua Vipawa vya Mungu katika Jumuiya ya Wathesalonike, hasa fadhila za imani, upendo na tumaini. Paulo aliwaelekeza maneno ya kutia moyo ili waweze kuendelea safari yao kwa shauku kama wachaguliwa wa Mungu ili kufanya kazi kubwa kwa kupitia ushuhuda wao. Ndiye Roho ambaye anasababisha matokeo mema ambapo watu wanachukua ahadi kwa ajili ya kazi ya Mungu.
Katika injili, tuko na vikundi viwili vilivyopingana wao kwa wao, lakini walipata kukusanyika na kukubaliana ili kumpinga Yesu. Hao walimjia Yesu na kumsifu kwa fadhila zake, yaani walisema kwamba Yesu ni mtu wa kweli, anayefunza njia ya Mungu kulingana na ukweli. Ingawa waliuongea ukweli kuhusu Yesu, hawakukubali njia ya maisha ambayo Yesu alipendekeza. Jambo la mazungumzo yao ndilo kodi, yaani “Ni halali kumpa Kaisari kodi, ama sivyo?” Yesu alitambua nia mbaya katika swali hili. Akisema “ndio” angechukuliwa kama mshirika wa utawala wa Warumi dhidi ya Wayahudi. Akisema “hapana” angechukuliwa kama mwasi. Basi, Yesu aliiomba sarafu na baada ya kuitazama, aliwaambia kwa hekima, yaani: “Mpeni Kaisari kilicho cha Kaisari na mpeni Mungu kilicho cha Mungu”.
Kutokana na maoni yenyewe ya wapinzani wa Yesu tuko na kipengele kimoja muhimu sana kuhusu utambulisho wa Yesu na kazi yake, yaani yeye ndiye mtu wa kweli. Mafundisho yake yana nguvu ya kusababisha hali mpya maishani mwa watu kwa sababu ya ukweli. Wanafunzi wa Mafarisayo na wengine wanapaswa kukiri kwamba ukweli kama huu hawawezi kuukuta katika mafundisho ya viongozi wao. Akifundisha, Yesu analenga kuwakomboa kutoka unafiki na wazo la uongo juu ya mapenzi yake ambao unawavuruga kuwa na uhusiano mwema na Mungu.
Wakati Yesu alipochukua sarafu aliona picha ya Kaisari. Mtawala huyo wa Roma alipiga chapa picha yake katika fedha kwa kusisitiza utawala wake juu ya watu wengi, alijiona kama amestahili heshima ya mungu. Kwa hivyo, Yesu aliwakumbusha kuhusu amri ya kwanza ambayo inakataza kufanya sanamu ya Mungu kwa sababu ya hatari ya ibada ya sanamu. Kwa jibu lake Yesu alianzisha tabia kamili kumhusu Kaisari na tabia kamili kumhusu Mungu. Watu walio wa Mungu wanamchukua Mungu kama kipaumbele juu ya kila kitu.

Mahali pa kwanza katika maisha yetu ni kwa Mungu. Wakati hatuko na tabia kamili katika uhusiano wetu na Mungu tunakosa pia tabia kamili kuhusu mali, pesa na kadhalika. Yesu hakukataa umuhimu wa malipo ya  kodi halali na tena heshima kwa serikali, kinyume, aliweka kama sehemu ya utambulisho wa wanafunzi wake kushirikiana na maendeleo ya jamii. Lakini anatukumbusha kwamba Mungu peke yake anastahili kuabudiwa. Hata serikali yetu inaweza kufanya mapenzi ya Mungu ikiwa inatumia mamlaka yake kwa ajili ya kusaidia maisha ya heshima kwa wote. Tunaalikwa kufanya upya ahadi yetu kama wana wa Mungu na mali yake na kusaidia maendeleo ya haki na amani katika jamii yetu.   

Fr Ndega
Mapitio ya kiswahili: Christine

Nenhum comentário: