domingo, 29 de outubro de 2017

KUMPENDA MUNGU KWA KUMPENDA JIRANI PIA


Kutafakari toka Kutoka 22, 20-26; 1Thes 1, 5-10; Mt 22, 34-40



      Maandiko Matakatifu yanashuhudia uhusiano maalum kati ya Mungu na watu wake. Mungu alitaka kuanzisha agano na watu hawa akiwapa miongozo kadhaa ili watende mema na kujenga hali nzuri kwa maisha yao. Ndiyo katika hali hiyo kwamba Amri kumi zilizaliwa kama njia za uzima. Hakuna jambo lingine muhimu katika safari yao ya waliochaguliwa ila kuishi Amri za Sheria kwa uaminifu. Kweli kwa Watu wa Israeli Sheria ni kama Neno la Mungu na Neno la Mungu ni Sheria. Wakati wao husema “Sheria ya Mungu ni kamili, faraja kwa roho”, wanaongelea Neno la Mungu (Torati).

    Kuna uhusiano wa ndani kati ya Sheria na Neno, kwa sababu amri za Sheria zinaonyesha utunzaji na upendo wa Mungu kwa watu wake. Ndiyo njia yake ya kutenda ambayo ilileta ukombozi na utambulisho kwa watu wa Israeli. Mungu anatarajia tu watu hawa waweze kutenda kama yeye kati yao hasa kwa ajili ya wanyonge (yatima na mjane) na wageni wanaohitaji msaada. Msingi wa amri ni moyo na nia ya Mungu wa kihuruma. Kutii kwa amri ni chanzo cha baraka kinachoelekeza kwa uzima, bali kutotii kunaelekeza kwa mauti.   
    
       Kwa bahati mbaya, pamoja na Sheria kuu, Wayahudi waliweka sheria nyingi, akichukua lengo kutoka jambo muhimu lilioanzishwa na Mungu. Amri kumi za awali zilikuwa amri mia sita kumi na tatu. Watu maskini walichukuliwa kama wenye dhambi kwa sababu hawakuweza kukariri amri hizi zote na kwa hiyo, hawakuziweka vitendoni. Hata hivyo, walijua muhimu ya Sheria. Hili ni jibu la Yesu aliposema: “upende Bwana Mungu wako na moyo wako wote, na akili yako yote, na nguvu zako zote” (Dt 6: 4-5) “na jirani wako kama unavyojipenda mwenyewe” (Lev. 19: 18).     

      Kumpenda Mungu ni amri ya kwanza ya zote, lakini Yesu aliiunganisha na upendo kwa jirani, kuonyesha kwamba haiwezekani kumpenda Mungu bila kumpenda jirani. Yakobo katika waraka wake anamfikiria kama mtu mwongo anayesema kwamba anampenda Mungu na kutompenda jirani. Kutoka kumpenda Mungu amri ya kumpenda jirani inabubujika kama matokeo. Chanzo ni Mungu daima kwa sababu ndiye aliyetupenda kwanza. Ni kutokana na upendo wa Mungu kwetu tunaweza kuwapenda wengine halisi. “hiyo ni changamoto kwa tamaduni zote hasa katika Afrika, ambapo uaminifu kwa familia na mila unakuzwa mara nyingi kama amri ya kwanza.”        

       Uwepo na kazi ya Yesu miongoni mwetu yaonyesha kwamba kwa kupitia upendo peke yake binadamu anaweza kupata mafanikio kabisa kwa maisha yake. Bila shaka, kwamba kuwa mwana wa dini ama kuhudhuria misa ni ishara ya upendo kwa Mungu kama kipaumbele katika maisha yetu. Hata hivyo, katika mwisho wa maisha yetu tuliulizwa sio kuhusu dini ama misa bali kuhusu upendo kwa wengine. Kipimo cha upendo wetu kwa Mungu kinaonyeshwa katika njia kama tunavyowapenda wengine. Anapenda kweli yule anayetamani tu wema wa yule anayependa, hata wakati hastahili. Hivi ndivyo Mungu anatupenda, yaani kwa ukarimu na bure.

       Muhimu kwa Yesu ni kumpenda Mungu, kwa kupenda jirani pia. Ufundishaji wake wa ajabu ulibadilisha amri hizi mbili kuwa moja peke yake, yaani: tupendane kama alivyotupenda. Kama vile Mungu ametupenda katika Kristo, hivyo tunapaswa kupenda kutoka kwa Kristo. Yeyote anayependa kulingana na njia hii amefahamu muhimu ya Sheria na ya maisha, kwa sababu yeyote anayefuata Yesu hafuati sheria au mafundisho, bali anamfuata Mtu.


        Basi, uaminifu wa tangazo la Wakristu duniani ni katika kupenda wengine kama ndugu. Tunampenda Mungu wakati tunapompa mahali pa kwanza katika maisha yetu, kwa kutafuta kwanza ufalme wake na haki yake. Tunapenda jirani wakati chaguzi zetu zinalenga kusaidia maisha na undugu juu ya kila kitu katika jamii. Tunaonyesha upendo wetu kwa Mungu kwa njia halisi sana  wakati tunapochagua kuhudhuria jumuiya badala ya kuchukua ahadi ya kibinafsi na tena wakati tunapatikana kuwasaidia wengine kwa sababu ya hali fulani ya huzuni na mateso. Hivyo, ilisemwa kuhusu Jimuiya za kwanza: “Oneni wanavyopendana”. Hali hii iliwezekana tu kwa sababu walibakia umoja katika upendo wa Mtu aliyewaita. Tufanye vivyo hivyo.

Fr Ndega

Nenhum comentário: