domingo, 16 de abril de 2017

UZOEFU UNAOZAA UZIMA UNAOSHINDA MAUTI


Kutafakari kuhusu At 10,34a.37-43; Col 3,1-4; Yoh 20,1-9


Tufurahi sote, kwa sababu hii ni siku aliyotufanyia Mungu! Tangazo la ufufuko wa Yesu ni mwaliko wa furaha, yaani furaha ya maisha ambayo yanayashinda mauti, furaha ya upendo ambao unaushinda uchungu na kutembea kama rafiki katika njia za watu wa Mungu akiyaimarisha matumaini yetu. Wanafunzi wa kwanza walipotangaza tukio hilo, walianza kutokana na maisha ya Yesu ya kibinadamu, aliyetiwa na Mungu kwa kazi ya wokovu wa binadamu. Kwao Wanafunzi wa kwanza uzoefu walioishi pamoja na Yesu ulikuwa umejaa maana. Kutokana na uzoefu huu waliweza kuwa mashahidi. Basi, tangazo lao halikuwa maneno peke yake bali uzoefu wa maisha pia, yaani maisha yao yalibadilika. Kama alama ya wema wa Mungu, maana ya maisha ya Yesu ilikuwa kuwatendea watu mema. Matendo yake yote mengi yaliwezekana tu kwa sababu Mungu alikuwa pamoja naye.
Ikiwa Kristo hakuwa amefufuka, je, mahubiri ya wanafunzi wake yangekuwa na maana gani? Hakika yangekuwa tupu, yaani, pasipo maana. Mbele ya kifo kisicho na haki cha mwalimu wao walikufa moyo sana, lakini ushindi wa uhai unawapa maana mpya ya kuishi. Basi, ujumbe wa wanafunzi unatafsiri pia ushindi dhidi ya hali ya hofu ambayo waliishi baada ya kifo cha Mwalimu, yaani kikundi chao kilivunjika. Kwa wanafunzi ilikuwa vigumu sana kuendelea kwa safari baada ya kukatishwa tamaa kwao kuhusu mwalimu Yesu ambaye walitarajia mengi, hasa awe mfalme mwenye nguvu. Lakini maisha yao yalibadilishwa kabisa baada ya kuona ushahidi wazi wa ufufuko wa Mwalimu, yaani kaburi tupu, vitambaa alivyolalia, na baadaye Yeye mwenyewe akajionyesha kwao; kisha waliacha hofu, wakiitoa nafasi kwa imani na kuchukua maisha ya mashahidi.     
Lakini tunapaswa kutambua kwamba safari hii ya imani ya wanaume iliimarishwa na ushuhuda wa mwanamke mmoja anayeitwa Maria Magdalena ambaye alikuwa wa kwanza kuenda kaburini akutane na Yesu na kupokea habari kwa ajili ya Mitume. Walialikwa kukaribisha njia mpya ya Yesu ya kuishi kati yao na kuyaamini Maandiko yasemayo kwamba alipaswa kufufuka kutoka wafu. “Magdalena ni yule ambaye Yesu aliponya kwa kufukuza mashetani saba ndani yake. Katika Biblia namba saba inamaanisha ukamilifu. Basi, Maria Magdalena alikuwa ameponywa na Yesu kikamilifu.” Katika uhusiano na Kristo Maria alikuta upendo wa kweli ambao alikuwa ameutafuta sana kwa muda mrefu. Mwanamke huyo alijifunza jinsi ya kuwa mwanafunzi wa kweli, akimfuata Yesu wakati wa mahubiri, tangu Galilaya hadi msalabani. Kwa hivyo anastahili cheo cha “Mtume wa Mitume wa Yesu.” 
Baada ya kupokea habari kuhusu udidimizi wa mwili wa Kristo, wanafunzi wawili wakaenda mbio kuelekea kwenye kaburi, yaani Petro na mwanafunzi aliyependwa na Yesu (Yohane). Walikimbia pamoja, lakini huyo mwanafunzi alifika kwanza. Kama hivi ni upendo ambao unapaswa kufika kwanza katika kila kitu. Yule anayependa anapata kuwa wa kwanza katika maonyesho ya upendo na imani. Anaweza kutambua mabadiliko kandokando yake, kwa sababu yeye mwenyewe ana moyo ambao umebadilishwa na uzoefu wa kujiona kupendwa. Anaweza kushuhudia kuwa bila uzoefu wa upendo wa kweli imani yetu ni haba na bila maana.

Uzoefu wa ufufuko ni uzoefu wa upendo wa hiari na mwaminifu wa Mungu ambaye anaendelea kufanya upya mambo yote na kutuchagua ili tuwe mashahidi wa hali hii mpya. Tena ni uzoefu wa imani ambayo inakuta msingi wake katika Maandiko Matakatifu yanayoshuhudia kwa Yesu Mfufuka. Huu ni pia uzoefu wa ahadi ambao unatuimarisha kama wafuasi sio wa Mungu aliye mfu bali Mungu aliye mzima.  Upendo wake unazaa uzima katika sisi pia na kutufanya tuushinde vikwazo, hofu na mashaka yote. Kama ilivyotokea kwa wafuasi wa kwanza, sisi pia tunajaribiwa kufa moyo katika safari yetu, lakini Mungu anatutumia daima yeyote ambaye kama Maria Magdalena anatuletea habari inayofanya tofauti katika maisha yetu na kuonyesha njia tofauti ya kufikiri na kuishi imani. Ushuhuda wetu kama mashahidi wa Bwana Mfufuka uwe kama ilivyotokea na wanafunzi wa kwanza, yaani umejaa furaha na shauku.

Fr Ndega

Nenhum comentário: