sexta-feira, 7 de abril de 2017

MSHIKAMANO KATIKA MATESO


kutafakari juu ya Mt 21,1-11; Is 50,4-7; Waf 2,6-11; Mt 26,14-27,66


          Tunaingia katika wiki muhimu sana kwa Jumuiya za Kikristo. Hii ni wiki inayojumuisha matukio makuu ya imani yetu, kueleza kwa ishara nyingi na kwa kina vipindi vya mwisho vya maisha ya Yesu kama binadamu hapa duniani na kutualika kwa ukimya na kutafakari. Hii ni pia nafasi ya kufanya upya ahadi yetu kama wafuasi wa Yesu na kuimarishwa na mifano yake ya uaminifu na uamuzi.

         Tunaalikwa kumfuata Yesu anayeingia kama mshindi katika Yerusalemu ili kukamilisha kazi yake ya upendo. Kwa kweli, hakuja juu ya farasi kwa kiburi na kwa jeshi yenye nguvu kama walivyofanya majenerali wakiingia mijini, lakini amepanda punda, na kuja kwa wema na rehema kama imetokea wakati wa maisha yake yote. Yesu anajua sana nini itatokea nawe, hata hivyo hakukata tamaa. Kinyume, anaonyesha uhuru wa Mwana mpendwa aliyepelekwa kuokoa wanadamu. Kama tunakumbuka kuingia kwake katika “Mji wa amani”, sisi pia tunakumbuka mateso na kifo chake katika mji huu ulio na mazoea ya kutenda kwa ukatili dhidi ya wajumbe wa Mungu. Hivyo kifo chake sio hatima, bali matokeo ya kazi ya kinabii aliyeishi kwa uaminifu hadi upeo.

        Kama tunavyojua, nabii Isaya anatoa nyimbo nne kuongea juu ya utambulisho na kazi ya Watu la Mungu, ambao pia wanaitwa “Mtumishi wa Mungu.” Nyimbo hizi ziliandikwa wakati wa utumwa wa Babeli nasi tunaweza kuzipata katika sehemu ya pili ya Kitabu cha Isaya. Andiko tunalotumia hapo unafahamika kama ‘wimbo wa tatu’ na kulingana na huu, mtumishi anaishi wito wake kama zawadi inayotoka kwa Mungu kwa ajili ya kutoa maisha mapya kwa ndugu zake. Kwa sababu ya uaminifu wake, aliaibishwa, alikataliwa na kuteseka sana, lakini hakukata tamaa, kwa sababu aliona ukaribu na utunzaji wa Mungu. Mtumishi huyo ni mfano ya Yesu ambaye kwa utambulisho wake na hali ya binadamu, alijinyenyekeza, akaaibishwa, akateseka na kuuawa maana ya uaminifu wake kwa Mungu. Imani yake ya kimwana katika Mungu ndiyo maana ya uaminifu wake. Kwa njia ya utupu aliupata utukufu. Njia ya unyenyekevu, ya ishara ndogo na ya kuchagua kinachoonekana bila maana kwa jamii ndizo ishara halisi zilizo tabia za wanaoendelea kazi yake.

       Kulingana na masimulizi haya ya Mathayo, Yesu anafikiria kuwa kukamatwa kwake, mateso na kifo chake kitakuwa kashfa kwa wanafunzi wake, maana bado walikuwa na mawazo ya Masihi mwenye nguvu na umaarufu. Hata hivyo, anaongeza kusema - kama kawaida - kuhusu ufufuko wake na baadaye atafanya upya ahadi nao kutoka mahali ambapo yote yalianza, yaani kutoka Galilaya. Kwa Yesu hakuna maonyesho ya upendo kubwa kuliko kutoa maisha yake kwa ajili ya marafiki zake, hata wakati wao wametoroka (isipokuwa wanawake na mwanafunzi mpendwa). Katika kilio chake, yaani “Mungu wangu, Mungu wangu, kwa nini umeniacha?”, yeye alionyesha uchungu ambao alihisi kweli kama mwanadamu, yaani, uchungu wa kuachwa, uchungu wa vitendo viovu, uchungu wa dhambi za binadamu, n.k. Ghafla, wakati yote yalionekana yamefanyika bila mafanikio, tuko na tangazo kubwa la imani: “Kweli mtu huyu alikuwa Mwana wa Mungu.”

       Yesu aliachwa na marafiki zake, lakini yeye hakuwako peke yake msalabani wala wakati wa kazi yake. Maneno yake mwenyewe yanashuhudia kuhusu hayo, yaani “Yule aliyenituma yuko pamoja nami, hakuniacha peke yangu, kwa maana mimi nafanya yanayompenda yeye (Yoh 8.29).” Hivyo “kilio” ambacho Mathayo anaweka mdomoni mwa Yesu kinapaswa kufahamika kwa uhusiano na kujisalimisha kwake mikononi mwa Baba, kulingana na toleo la Luka, iliyo tabia yake daima, yaani “Baba, mikononi mwako naiweka roho yangu (Lk 23,46).” Vinginevyo, tungekuwa kukana sio tu kazi yake kwa ushirika na Baba bali pia uaminifu wa Baba huyo.

         Fumbo la mateso na kifo cha Yesu halionyeshi uchungu kama jambo la kwanza kwa kutafakari bali upendo wake mkubwa hadi upeo. Kifo hakikuwa kulazimishwa kwa Yesu, bali yeye alikubali kwa hiari. Yesu alijua kwamba alikuwa akifanya jambo sahihi na hivyo mateso yake ni mwanzo wa ushindi wake juu ya mauti, akifufua matumaini yote ya maskini na ya wanadamu wakosefu.


      Mateso ya Mwana wa Mungu yanatualika kutafakari juu hali ngumu ya mateso ya binadamu. Kama Mungu alijibu kwa ufufuko mbele ya kifo cha Mwanawe, tunaweza kuhitimisha kwamba Mungu hataki mateso wala mauti ya watu. Yeye hawaachi wale wanaoteseka wala hanyamazi mbele ya mateso yao. Kristo alichukua kwa nafsi yake uchungu wa watu wote wa nyakati zote. Yeye anaendelea kuteseka wakati sisi tunahisi maumivu na majaribio katika safari yetu. Mfano wake unatuimarisha tuwe na kuwepo ufanisi maishani mwa watu wanaoteseka zaidi kuliko sisi. Misalaba ya mshikamano na huruma tunayoitwa kuchukua kila siku kama yeye alivyo inafanya kujitolea kwetu kuwe ishara ya upendo pia kama ushiriki katika mateso yake kwa ajili ya wokovu wa watu wote.

Fr Ndega

Nenhum comentário: