sábado, 29 de abril de 2017

UWEPO HAI NA UFANISI WA KRISTO ULIMWENGUNI


Kutafakari kuhusu Mat 2, 14a.22-33; 1Pd 1, 17-21; Lk 24, 13-35



Yesu alishiriki uwezo wake na wanafunzi wake akiwawezesha waendelee kazi yake. Kwa msaada wa Roho Mtakatifu, hasa katika siku ya Pentekoste, walitangaza kwa furaha uzoefu walioishi pamoja na mwalimu wao na ushindi wake juu ya mauti kwa uwezo wa Mungu. Tangazo hili ni mwaliko wa tumaini kwa sababu ushindi wa Yesu unatoa nafasi ya wokovu kwa wote. Kwa sababu ya Kristo imani yetu na tumaini letu linamwelekea Mungu ndiye Baba na kutaka tutende kulingana na mfano wa Mwanawe. Ingawa Yesu haonekani tena kwa macho, yeye anaweza kutambuliwa kwa matendo yetu mema hasa tunaposikiliza neno na kusherehekea Ekaristi. 

Mazungumzo ambayo injili inatujulisha ni mamoja kati ya mazungumzo ya ajabu na ya kamili ya Biblia. Hapo tuko na mwendo wetu wa upevu wa imani na sehemu za sherehe ya Ekaristi takatifu, yaani hali ya jumuiya inayokusanyika kwa jina la Bwana, uwepo wa Bwana Mfufuka anayetueleza Maandiko Matakatifu na kuumega mkate kwa kutualika kuendelea kama yeye alivyo.  

Tuko na wanafunzi wake wawili walikuwa wakielekea mji uitwao Emau, Kilomita 11 kutoka Yerusalemu. Wanafunzi walihuzunika sana, wamekata tamaa, wamekufa moyo na wakaiacha jumuiya na kurudi nyumbani, wakiwa tayari kusahau kila kitu walichoshiriki pamoja na Yesu. Walitarajia Masihi mtukufu na mfalme mwenye nguvu, lakini matokeo yalikuwa mbali sana na matarajio yao: mtu mpendwa alishindwa na akafa msalabani. Hakukuwa chochote cha kufanya isipokuwa kurudi kwa maisha waliyoyajua kabla ya kukutana na Yesu.

Ghafla alitokea mtu mgeni, ambaye alitembea pamoja nao na kuongea nao kuhusu matokeo ya hivi punde, yaani Yesu aliye nabii mwenye nguvu katika kazi na maneno mbele ya Mungu na watu, lakini alikuwa na mwisho usiotarajiwa. Huyo Mtu Hija aliyatafsiri Maandiko ambayo yanazungumza kuhusu Masihi. Walimsikiliza kwa uangalifu na mioyo yao ilianza kuchoma. Hatimaye, wanafunzi walifika nyumbani na kumwalika: “Kaa pamoja nasi, Bwana”!

Baada ya kulikaribisha Neno la Mtu hija, walimkaribisha nyumbani kwao. Yule mgeni alikubali kuingia sio kwa kukaa pamoja nao usiku mmoja tu, bali kubaki nao daima. Wakati wao walikuwako mezani,  mtu Hija  alifanya ishara inayojulikana, ishara ya karamu ya mwisho, wakati Yesu alipoanzisha Ekaristi. Macho ya wanafunzi yalifunguliwa na kumtambua Bwana Mfufuka. Hivyo Neno linaichoma mioyo; kuumega mkate hufanya kufungua macho. Kristo alitoweka maana jumuiya imekwisha pata ishara halisi za uwepo wake, yaani Neno lake na Mkate Uliomegeka. Asiyeonekana kwa macho, Bwana ndiye kuwepo na kubaki daima. Sasa ni wakati wa kushuhudia.

Yesu yu hai na kuandamana na binadamu katika safari yetu, ingawa hatambuliwi daima. Anajifanya kujulikana katika uzoefu wa kuumega mkate. Kama wanafunzi wake tunahitaji kuwa pamoja naye, kujiruhusu kuandamana naye, kusikiliza maneno yake na kumwalika kukaa nasi. Ni thamani yake kukaa nasi na kutuonyesha njia ya kweli ya kuishi. “Ni maonyesho haya ambayo Wakristo wa kwanza walitumia kuonyesha ushirika wao wa Ekaristi. Kwa kufanya hivyo walimaanisha kwamba wote ambao wanakula mkate mmoja uliomegwa, yaani Kristo, wanaingia katika ushirika pamoja naye na kufanya mwili mmoja naye” (CCC 1329).


Katika safari yetu ya imani hatuko peke yetu kamwe. Yesu anatujia na kutembea pamoja nasi. Yeye anapatikana kwetu hasa wakati tunapokata tamaa na kutaka kuacha ahadi yetu kabisa. Yeye anatusikiliza na kutuongoza kwa neno lake ambalo linachoma mioyo yetu ili tuweze kumtambua katika Ekaristi na kuishi hali hii katika uzoefu wetu wa kila siku. Ndio uzoefu huu unaotufanya kuwa mashahidi wenye furaha na ujasiri wa uwepo wake hai na ufanisi kati yetu.   

Fr Ndega

Nenhum comentário: