domingo, 12 de março de 2017

SAFARI YETU YA IMANI NI MWALIKO WA KUGEUKA SURA DAIMA


Kutafakari kuhusu Mwanzo 12: 1-4a; Mathayo 17:1-9

Safari ya wale wanaomwamini Mungu ina maana kwa sababu wanatembea kwa tumaini la kuishi milele. Binadamu ni “mtafuta wa Mungu” tangu kuzaliwa kwake. Baada ya kila hatua, tunaalikwa kuendelea kwenye nyingine maana hamu fulani ndani yetu inatuimarisha kusonga mbele na kutuambia, “upeo wa macho bado”, lakini ni lazima kuendelea kutembea. Kuna mambo mengi ya kuacha kwa sababu kila hatua mpya ya maisha yetu inatuongoza kuchukua mambo mapya.

Ili tufikie lengo kamili la maisha yetu hatuhitaji haraka bali uamuzi ulioandamana na imani unakuta mwelekeo wake kamili kwa sababu yule anayetualika kwa “tukio la kuishi” anatuvutia kwake kweli, kulingana na Mt. Augustine anayesema, “Ee Mungu, umetufanya kwa ajili yako na mioyo yetu inahangaika hadi ikapumzike kwako”. Tukimwangalia Yesu anayegeuka sura ni rahisi kuelewa maana ya kweli ya maisha yetu. Hivyo ndivyo tunaalikwa kuelewa mwaliko wa Mungu kwa Ibrahimu kwenye hali isiyojulikana na mwaliko wa Yesu kwa wanafunzi wake waandamane naye kwenye mlimani.  

Ibrahimu anafahamika kama “baba yetu katika imani” kwa sababu alikuwa wa kwanza aliyesadiki tofauti kabisa na matarajio ya kibinadamu. Yeye alialikwa kuacha yote na kufunga safari. Hakujua mahali ambapo alipaswa kufika, hata hivyo aliamua kumwamini Mungu na kuzikubali ahadi zake kama kipimo katika safari yake. Mambo yote yaliyosemwa na Mungu yalitimia kwa sababu ni mwaminifu yule aliyeahidi. Ibrahimu alisonga mbele sio kwa ajili ya kutimiza mpango wake wa kibinafsi tu bali pia kwa kufanya mapenzi ya yule aliyemwalika kufunga safari. Safari yetu siyo tofauti na ile ya Ibrahimu. Labda tunahitaji imani kama vile yake.

Tukio la kugeuka sura kwa Yesu kulitokea baada ya siku sita ya ufunuo kuhusu mateso, kufa na kufufuka kwake. Wakati huo huo aliwaalika wanafunzi wamfuate kwa “kujikana wenyewe, kuuchukua msalaba wao na kumfuata Yesu.” Kweli mambo hayo yalikuwa dhidi ya matarajio yao yote kuhusu mtu huyo waliyetambua kama Kristo wa Mungu. Hata yeye aliongea kuhusu kufufuka kwake, lakini mioyo yao ilikwisha sumbuliwa nao hawakuweza kuelewa vizuri. Basi, Yesu aliwaalikwa baadhi ya wanafunzi waandamane naye kwenye Mlima Tabor. Safari hii ilibadilisha mtazamo wao. Huko mlimani Yesu aligeuka sura mbele yao. Yesu aliwaonyesha kidogo utukufu wake na hali ijayo ya maisha ya wale wanaomfuata kwa uaminifu. Yesu aliwaalika kwa uzoefu wa juu ili waone kwa mtazamo wa juu na kuweza kuona vizuri hali ya kujisalimisha kwake na hali ambayo waliakwa kuichukua kama ahadi na Mwalimu wao.

Uwepo wa Musa na Elia unaeleza kuhusu rejeo la ufunuo katika Agano la Kale. Wote wawili waliongea na Yesu wakionyesha kwamba hakuna kupasuka kati ya mafundisho yao na yale ya Yesu, bali uhusiano na mwendelezo. Lakini kulingana na sauti iliyosikika kutoka kwenye wingu, ingawa mafundisho ya Yesu ni mwendelezo, ndiye yeye kwa uwezo wa kufundisha na kutafsiri kamili yale yaliyosemwa na mababu wa zamani. Baba alishuhudia kuhusu Mwana wake, akimuweka kama rejeo la maisha yetu, yaani, “Huyu ni Mwanangu mpendwa, msikilizeni”. Wote wanaalikwa kumsikiliza[1]. Kusikiliza katika Biblia ni kitenzi chenye nguvu sana. Hii ni tabia kamili ya Myahudi mbele ya Neno la Mungu, akifanya mazoezi kuhusu yale aliyosikia. Basi, kusikiliza kuna uhusiano wa kidani na kushika/kutenda.

“Wanatamani kubaki mlimani, lakini sauti inatoka mbinguni iliwaalika kumsikiliza na kumtii Yesu.” Mara nyingi Mungu anatualika kufanya uzoefu wa uwepo wake kama ilivyotokea na Ibrahimu ama kama vile wale kwenye mlimani. Mfano, tunaposhiriki katika sherehe fulani ama siku za maombi na kadhalika. Uzoefu kama huu unaiimarisha imani yetu na hamu yetu kwa ajili ya kazi ya Mungu. Kwa kawaida tunataka uzoefu huu uwe wa muda mrefu. Lakini safari yetu yapaswa kutendeka kati ya “kupanda mlimani” (mfano wa uzoefu wa Mungu wa kibinafsi) na “kushuka milimani” (mfano wa changamoto za undugu na kazi). Kila siku tunaalikwa kufanya uzoefu wa “kugeuka sura” kwa kusikiliza Neno la Yesu na kufanya mazoezi kuhusu Neno hili. Uzoefu huu unatusaidia kutambua nyuso bila heshima za ndugu wengi kandokando yetu na kuona hisia na tabia za Kristo kwa ajili yao. “Kusikiliza neno lake kunatupatia nguvu ya kumfuata mpaka mwisho.” Hii ni njia kamili ili tuwe pia “wana wapendwa” wa Mungu.


Fr Ndega


[1] Yesu ni ufunuo wa kipekee wa Mungu. Hakuna mwingine ambaye aweze kumdhihirisha Mungu kama Yesu alivyo. Kweli Mungu aliongea wakati wa zamani kwa mababu zetu. Lakini “siku hizi” mambo yote ambayo Mungu anaendelea kudhihirisha kwa watu anafanya kwa Mwanawe Yesu Kristo. Hata wale ambao hawamjui Yesu wanapokea ufunuo wa Mungu kwa njia yake. Katika kila ndugu ambaye wanamsaidia wanaweza kukutana na Kristo ambaye alijitambulisha na walio na mahitaji mengi (cf. Mt 25,31-46). Kipimo ni upendo/huruma. Matendo yao ya huruma yanaongelea Kristo.

Nenhum comentário: