domingo, 5 de março de 2017

CHAGUA INAYOFANYA TOFAUTI


Kutafakari kuhusu Mwanzo 2, 7-9; 3,1-7; Waroma 5, 12-19; Mathayo 4, 1-11 


Binadamu alifanyika kwa mavumbi ya ardhi ili kupokea uhai wa Mungu ndani yake. Pamoja na mahali pazuri pa kuishi, binadamu alipewa pia zawadi zote alizohitaji aishe kwa ushirika na Mungu na kwa maelewano na ardhi iliyo sehemu ya maisha yake. Lakini majaribio ya kutumia zawadi zake kwa ajili ya nafsi yake mwenyewe yalimwongoza binadamu kuacha ushirika na Mungu na kupanga maisha yake tofauti kabisa na mpango wa Mungu kwake. Binadamu wa kwanza alipendelea kumtii “nyoka”, aliye mfano wa “yule mwovu,” kuliko kumtii Mungu. Hali hii ilisababisha mauti kwa watu wote. Ndiye Yesu “Adamu wa kweli” aliyegundua tena mpango Mungu na kushinda uovu akimtii Baba yake. Chagua yake ilifanya tofauti kwa sababu ikawaletea wote uzima.  
Mambo yote ambayo Yesu aliweza kufanya alipata mafanikio kwa msaada wa Roho Mtakatifu. Ndiye huyo Roho ambaye alimwongoza nyikani na huko pia alijaribiwa na shetani. Kweli Yesu alionyesha ahadi na hali yetu ya kibinadamu. Mfano, yeye alienda jangwani baada ya ubatizo. Ingawa hakuhitaji kubatizwa alikubali uzoefu huu kwa ajili ya mshikamano nasi tulio wenye dhambi na ya kuiheshimu kazi ya Yohane. Vivyo hivyo, alikubali kushawishiwa jangwani. Anataka kutuonyesha kwamba “baada ya ubatizo majaribio mengi yanatujia.” Kwa upande wake, ingawa alijaribiwa jangwani, “alichagua kubaki mwaminifu kwa Mungu.” Yesu alijua wazi sana kwamba yeye ni Mwana wa Mungu na kwamba alikuja kwa ajili ya kufanya mapenzi ya Baba yake. Kwa kifupi, ndiye Roho Mtakatifu aliyemsaidia Yesu kuwa mwaminifu kwa mpango wa Mungu.
Katika uzoefu wake wa jangwa, Yesu alifunga kwa siku arobaini na akaona njaa. Arobaini[1] ni namba ya mfano iliyomaanisha “muda mrefu.” Kabla ya Yesu tuko na baadhi ya mifano ya Viongozi wa kibiblia ambao, kabla ya kuchukua kazi ama kabla ya tukio muhimu, waliruhusu kuongozwa jangwani na kubaki bila kula chakula wakati wa muda mrefu ili waweze kuandaliwa vizuri kwa ajili ya kazi aliyowakabidhi Mungu. Tukumbuke ule muda wa siku arobaini ambao Musa alibaki milimani Sinai ili azipokee Amri Kumi; na pia siku arobaini wa Eliya akitembea mpaka milima Horeb ili akutane na Mungu na kuyapokea maelekezo ya kazi yake kama nabii. Namba arobaini inatumika pia kuongea kuhusu kiasi ya miaka ambayo Waisraeli walibaki jangwani kabla ya kuingia katika nchi ya ahadi. Kwa watu hawa wakati huu ulikuwa wa utakaso na kukomaa. Lakini hawakuwa na uaminifu kama Yesu alivyo.
Uzoefu jangwani ni maalum kwa ajili ya upweke, utakaso na kukomaa. Lakini jangwa ni pia maisha yetu ya kawaida ambapo tumeongozwa na Roho Mtakatifu, lakini tunajaribiwa kukata tamaa kwa sababu ya majaribio ya yule mwovu, kama ilivyotokea na Yesu. Mshawishi alianza kutoka mambo madogo akichukua nafasi ya kosa la nguvu mwilini mwa Yesu kwa sababu ya kufunga. Matarajio yote yalikuwa dhidi ya namna ya kuwa masiha ambayo Yesu alichagua. Yesu alimshawishiwa kutumia uwezo wake kwa manufaa binafsi badala ya upendo, huruma na utumishi kwa wengine. Tena Yesu alishawishiwa kusifiwa badala ya kutangaza Mungu na Ufalme wake. Majaribu matatu ya Yesu yanamaanisha majaribio yote ambayo yalikuwapo maishani mwake nyakati zote za kazi yake. Hata hivyo, alipata kushinda yote kwa sababu akaongozwa na Roho Mtakatifu na kuwa mtiifu kwa Baba yake.
Majaribu ya mali, nguvu na utukufu Yesu aliyokabiliana nayo hayakumzuia ya kufanya mapenzi ya Mungu. Kama ilivyotokea na Yesu, na Adam na Waisraeli, sisi pia tunashawishiwa kuishi bila kumwamini Mungu. Mitego ya mshawishi inatuongoza kupendelea kutumia mamlaka kuliko utumishi, kuamuru kuliko kutii, kudanganya kuliko kusaidia, kulazimisha kuliko kupendekeza, kutafuta upendeleo kuliko kupenda, kuwa wanafiki kuliko kuwa binadamu wa kweli. Kama Yesu amekwisha kumshinda adui ya Mungu, ndiyo chagua yake msukumo ili chagua zetu ziweze kufanya tofauti. Kulingana na Mt. Agustino “Ikiwa katika Kristo tumeshawishiwa, katika yeye tutamshinda shetani. Kristo angeweza kumtupa mshawishi mbali sana naye; lakini ikiwa yeye hakuwa ameshawishiwa hangetufundisha jinsi ya kushinda juu ya majaribu.” Kweli yeyote ambaye anaufuata mfano wake wa kumtii Baba na kufunguliwa kwa msaada wa Roho Mtakatifu anapata kufanya mapenzi ya Mungu na kushinda majaribio yote.

Fr Ndega



[1] Katika Jumuiya za Kikristo umeanzika wakati wa toba unaoitwa Kwaresima. Kwaresima ni siku arobaini za maandalizi kwa adhimisho la fumbo la Pasaka ya Kristo. Kutokana na uzoefu wa Kristo jangwani, wakati wa kwaresima unalenga kuwa ni uzoefu wa jangwa na kuwaalika waamini kuweka juhudi zaidi maishani mwao hasa kuhusu sala, upendo na kutubu.

Nenhum comentário: