quinta-feira, 11 de novembro de 2021

JIBU LA KIKRISTO KATIKA WAKATI WA MGOGORO

 

Kutafakari kuhusu Dan 12: 1-3; Waeb 10: 11-14; Mk 13: 24-32

 


Tuanze tafakari hii tukijiuliza swali moja: “Je, Wakristo wanapaswa kuwa na tabia gani wakati wa mazingira magumu na mbele ya kosa la uhakika lililo tabia ya wakati huu wetu? Sisi tu watu wa tumaini kwa sababu maisha ya mtu anayemfuata Yesu yamejaa maana. Basi, ujumbe wa liturgia hii ni msukumo kwetu tulioalikwa kutoa maana za tumaini letu kupitia imani yetu katika Kristo. Uhakika wa ukaribu wake ndiyo nguvu yetu. Tukikumbuka kwamba leo ndiyo Siku ya Maskini Duniani, tujaribu kuwa kidugu na wenye mshikamano, tukiwafikiria wengine kuliko sisi wenyewe. Kulingana na Papa Francis, "umaskini si tunda la hatima bali ni matokeo ya ubinafsi". Hivyo, hakuna mtu anayeweza kusema: "Hali hii haina uhusiano wowote nami”.     

Somo la nabii Danieli ni mojawapo kati ya maandiko ya Agano la Kale yanayoongelea imani katika ufufuko (angalia pia 2 Mac 7, 9). Watu wa Israeli walitumwa na Wagiriki na kuteseka sana. Wengi miongoni mwao walishindwa kumwamini Mungu, lakini wengine ambao waliendelea kumwamini walihitaji ujumbe wa tumaini na kutia moyo ili kuendelea safari yao kwa uvumilivu. Mungu ndipo daima kati ya watu wake na kuwasaidia mbele ya mazingira magumu ambayo wanakabiliana. Ufufuo ulioahidiwa ulitimizwa kwa ufufuo wa Mwana wake kutoka kwa wafu, kama wa kwanza ya wengi wa ndugu na dada.

Kulingana na somo la pili toleo la Kristo lilishinda dhabihu zote za makuhani wa Agano la Kale. Dhabihu zao zilitendeka mara nyingi bila nguvu ya kuondoa dhambi za watu, yaani zilikosa ufanisi. Kwa upande wa Kristo, hali ni tofauti. Toleo lake lilitendeka mara moja tu nayo ilitosha kwa kuwatakasa watu wote katika nyakati zote kwa sababu alijitolea mwenyewe. Katika kila misa takatifu tunasherehekea fumbo la toleo hili. Ndiye Kristo mwenyewe ambaye anatuhusisha katika mwendo huu kwa ajili ya wokovu wetu na wa wengine.

    Mwanzoni mwa sura ya kumi na tatu ya injili hii ya Marko Yesu aliongelea uharibifu wa Yerusalemu. Ufunuo huu uliwaimarisha wanafunzi wake wamwulize kuhusu ishara gani na siku na saa gani ya uharibifu huu. Kisha, Yesu alitumia nafasi hii ili kuongelea mambo mengi yatakayotokea kuhusu historia na kuhusu utume wa jumuyia ya wanafunzi iliwekwa naye. Yeye Atarudi tena mara ya pili kwa ajili ya ukamilifu wa uumbaji na kuwakusanya mataifa yote karibu naye. Hivyo, “mpago wa Mungu unatimiza: kufanya Kristo awe moyo wa ulimwengu”.

    Mbele ya udhihirisho mtukufu wa Kristo “nguvu za mbingu zitatikiswa”. Hali hii inamaanisha kwamba miungu ya uongo, yaani jua, mwezi, itapoteza mwanga wao. Hata wale waliojiona watu wa kimungu (nyota za angani) ambao wanawatesesha watu wa mataifa hasa walio maskini, hao (miungo ya uongo) wataanguka na mtazamo wa wote utamwelekezea Mwana wa Mtu akija amejaa nguvu na utukufu kama mshindi. Hakuna mtu anayejua wakati kamili ambao mambo yote yatatokea ila Baba peke yake. Kwa hivyo ni lazima kumwamini yeye.  

    Ingawa uharibifu wa mji wa Yerusalemu ulitokea katika mwaka wa 70 B.K., nia ya Yesu haikuwa kuwajulisha kuhusu tukio hili, bali kuhusu matokeo ya tukio hili maishani mwa wafuasi wake. Ni lazima kutafakari injili hii kulingana na mazingira ambayo jumuiya ya Marko ilikuwa inaishi, yaani wanafunzi wa Yesu waliishi kipindi cha machafuko na kujaribiwa kukata tamaa kuhusu utambulisho wao wa wafuasi wa Yesu kwa sababu ya majaribio na mateso mengi. Kweli ulionekana mwisho wa dunia. Wale ambao walidumu kwa imani walijiuliza: “hayo yatokeayo yamaanisha nini?”. Kumbukumbu ya mafundisho ya Yesu ilikuwa muhimu sana kwa kuchukua tena lile ambalo liliwapa maana kwa maisha yao. Walikuwa na uhakika kwamba ikiwa ni Yesu kipimo cha kila jambo na lengo la historia, hivyo maisha na historia haziongozwi kwenye mwisho fulani bali kwenye lengo kamili: Yesu Kristo mwenyewe.

    Yesu ni mshindi juu ya dhambi na kifo na atawafanya wote wanaomfuata wawe washindi. Wakati wa kuja kwake katika mwisho wa nyakati (utimizaji wa nyakati) anataka kutukuta sisi "wavumilivu na macho", waaminifu kwa mafundisho yake ili tushiriki naye furaha yake mwenyewe. Neno lake linatuambia kwamba majaribu na magumu ni sehemu ya hali yetu kama Wakristo, lakini pia linatuhakikishia ukaribu wa Bwana: "Tambueni ya kuwa Yeye yu karibu, yu karibu milangoni! (Mk 13, 29)." Anataka tu kutambuliwa na kukaribishwa. Kwa kuwa sikuzote hatuwezi kuelewa matukio yanayotuzunguka, ni lazima tuwe na imani katika Baba, tukitambua kwamba “tuko mikononi mwake na kwa hiyo, tuko mikononi mwema. Hakuna kinachofikiwa na macho yake. Kila jambo linalotokea linaelekezwa kulingana na mpango wake mwenyewe wa hekima na wema” (Mt. Yohane Calabria).

    Basi kwa upande wetu tumwaminie Yule ambaye anaiongoza historia.Sisi tulioalikwa kuendelea utume wa Mwana wake Yesu, tunapaswa kuwa macho kwa ishara za uwepo wake ambazo zimetokea kati yetu. Ili hali mpya ikatokee maishani mwetu, miungu mingi ya uongo yapaswa kuanguka na kupoteza thamani yao. Kwa maneno mengine, tunapaswa kuacha picha za uongo za Mungu, mawazo na tabia ambayo inayapinga mafundisho ya injili. Tuishi wito wetu kwa shauku na furaha kwa sababu kuna tumaini kwa wakati ujao wetu.


Fr Ndega

Nenhum comentário: