sábado, 1 de dezembro de 2018

TUINUE KICHWA KWA SABABU UKOMBOZI WETU WAKARIBIA



Kutafakari kuhusu Lk 21, 25-28, 34-36

    Tumeanza wakati mpya katika liturujia ya kanisa uitwao Majilio. Wakati huu unayaimarisha matumaini yetu katika matarajio ya Kuja kwake Bwana mara ya pili katika mwisho wa nyakati na kukumbuka pia Kuja kwake kwa kwanza kwa kutuandaa ili tusherehekee sikukuu ya kuzaliwa kwake katika Krismasi. Basi, Liturujia ya msimu huu ni mwaliko kwa kukesha ili tutambue na kuzikaribisha ishara za uwepo wa Bwana katika hali yetu ya kila siku. Ni mwaliko pia kwa shukrani kwa sababu Bwana anakuja daima kukutana na sisi, kutupa wokovu wake. Matukio yote makuu yanahitaji maandalizi mazuri ili yaweze kusherehekewa vizuri. Hivyo ndiyo Majilio kulihusu tukio kubwa la Krismasi.

         Mwanzoni mwa sura ya kumi na tatu ya injili ya Luka Yesu anaongea kuhusu uharibifu wa Yerusalemu. Ufunuo huu uliwaimarisha baadhi ya wanafunzi wake wamwulize swali kuhusu ishara gani, siku na saa gani ya uharibifu huu. Yesu anatumia nafasi hii kutabiri kuhusu mambo mengi akiiandaa mioyo ya wafuasi wake kwa wakati ujao. Aliwaambia kuhusu ishara nyingi mbinguni, taabu, mateso, dhiki kuu na kuja kwake, kulingana na unabii wa Danieli, yaani, juu ya mawingu ya angani mwenye nguvu na utukufu mwingi. Kanisa katoliki hutafsiri tukio hili kama kuja kwake Yesu mara ya Pili ili kuwahukumu wazima na wafu. Hiyo ndiyo imani yetu ambayo sisi hutangaza kila jumapili. Kuhusu siku na saa hii hakuna mtu ajuaye. Hii ni sehemu ya mpango wa hekima na wema wa Baba. Kwa hivyo huu ni pia mwaliko kwa kukesha.

         Yesu anatabiri kuhusu hali ngumu na matokeo ya hiyo katika maisha ya wafuasi wake. Wanafunzi wa Yesu wataishi kipindi cha machafuko na watajaribiwa kuiacha imani katika Kristo na kukata tamaa kuhusu utambulisho wao wa wanafunzi kwa sababu ya matusi, majaribio, matatizo na mateso mengi. Ilionekana kwamba walikuwa peke yao mbele ya machafuko hayo yote. Lakini Yesu mwenyewe alikuwa amewaahidi uwepo wake daima kupitia maneno haya, “mimi nipo pamoja nanyi sikuzote, hata ukamiliifu wa dahari.” Maneno haya ni mwaliko kwa ushuhuda kama njia ya kukesha. Hao wana jukumu la kuendelea utume wa Mwalimu, wakiwa makini kwa ishara za kuja kwake ili akutane nao na kuwatuza kwa maana ya uaminifu wao.

Andiko hili linatuambia kwamba Kristo ni mshindi na ujio wake unaanzisha wakati mpya anaoshiriki na wanafunzi wote wanaobaki wamesimama na kuinua vichwa vyao kupitia imani na ushuhuda kwa uaminifu. Tunapaswa kuishi imani yetu ya kikristo kwa uhusiano na kila kitu ambacho kinatokea kandokando yetu. Jamii inatarajia imani yenye maana na kuhitaji jibu kwa hali ngumu binadamu anayoiishi. Je, Wakristo wanapaswa kuwa na tabia gani wakati wa mazingira magumu? Kama alivyowaambia wafuasi wake wa zamani, Yesu anatuhakikishia kuwa mazingira magumu ni sehemu ya safari ya wale ambao wanamfuata katika nyakati zote, lakini Yeye anatukumbusha pia kwamba ni katika machafuko haya ya dunia hii tunapojiandaa kukutana naye mwishoni mwa maisha yetu binafsi hapa duniani. Kwa hivyo kila hatua ya safari yetu ni maandalizi kwa mkutano wa mwisho na Bwana wetu.

        Liturjia linataka kuimarisha imani yetu na kufufua tumaini letu kwa tendo la wokovu wa Mungu ndiye mkuu katika nyakati zote, zilizopita na zijazo. Hali hii inatualika kuishi wito wetu wa wafuasi kwa uaminifu katika nyakati zote pia, hata wakati wa dhiki. Baada ya machafuko yote tutakuwa washindi pamoja na Bwana wetu mshindi. Kulingana na mithali fulani, “hakuna usiku hata wa muda mrefu pasipo mapambazuko”. Basi, kwa wale wanaomfuata Kristo, mazingira magumu si ishara za mwisho wa nyakati bali ni wakati mpya, wakati wa kuishi wito wetu kwa shauku zaidi, furaha na tumaini, kuushuhudia kwa uaminifu uwepo wa Bwana miongoni mwetu. Anakuja kwa upendo na kutuokoa. Tukaribishe ishara za nyakati kama msaada tutambue uwepo wa Bwana na kuishi mafundisho yake kwa njia mpya.

Fr Ndega

Nenhum comentário: