sábado, 8 de dezembro de 2018

UZOEFU WA KWELI WA NENO LA MUNGU


Kutafakari kuhusu Bar 5, 1-9; Wafil 1: 3-6, 8-11; Lk 3, 1-6


      Liturujia ya jumapili hii inaendelea kutumwalika kumkaribisha Bwana anayekuja kutuletea wokovu. Tunapaswa kujiandaa vizuri ili tuweze kumpokee Masiya wakati wowote. Wakati wa Majilio unatusaidia kutambua kwamba kwa matayarisho kamili ni lazima mabadiliko ya moyo, kwa njia mpya kabisa.  Maneno ya nabii Baruku yaliimarisha watu utumwani Babeli yakitangaza ukombozi karibu. Baada ya mateso hayo yote wataweza kurudi nyumbani Yerusalemu kwa furaha kubwa kwa sababu Mungu aliwakumbuka na kuwaongoza katika mwangaza na utukufu wake. Huu ni mfano wa wokovu wetu katika Kristo. Paulo anatambua kwamba imani na ushirika wa Wafilipi ni uenezi wa injili waliyochukua kwa shauku na utayari. Kwa njia ya Kristo na injili yake wanaweza kuzaa mazao mazuri kwa utukufu na sifa ya Mungu.  

         Injili inaongelea Yohane Mbatizaji anayefikiwa na Neno la Mungu jangwani. Katika biblia jangwa ni mahali maalum pa uzoefu wa Neno la Mungu. Katika mahali huko watu wengi walijibadilisha kuwa viongozi wenye nguvu kwa kuwaongoza Watu wa Mungu kulingana na mwongozo wake. Yohane Mbatizaji anafikiriwa kuwa nabii wa mwisho na mkuu wa manabii wote. Toleo la Luka linataja makuhani na viongozi wa kisiasa ili kuonyesha kwamba kupitia mjumbe wake, Mungu huingia katika maisha halisi ya watu kwa wakati fulani. Mungu haongei moja kwa moja bali kwa kupitia matukio mazuri au mabaya  ya historia ya watu. Mungu alijifanya mmoja wetu na bado yuko nasi kwa namna mbali mbali. Kwa kiyo hakuna tukio lolote la historia lisilokuwa na maana. Kwa kuonyesha wito wa Yohane katika matukio ya wakati wake, Luka anaonyesha kwamba tukio kubwa liko karibu. Mungu anaingia katika historia kwa namna ya pekee na kuomba watu watayarishwe kumkaribisha Masiya aliyetarajiwa kwa muda mrefu.

Kuja kwake Yohane Mbatizaji kuna maana na kuufuata mpango wa Mungu ambaye ana wakati kamili kwa kila kitu. Neno lake linayabadilisha maisha ya Yohane katika chombo cha wokovu. Kama Yohane ni kiungo kati ya Agano la kale na Jipya, kazi yake inatangaza kwamba nyakati za Masiya ziko karibu kuanza. Yeye ni sauti tu ambayo inatayarisha njia za Bwana. Yohane aliwatayarisha watu kumpokea Masiya kwa ubatizo. Kupitia ishara hii alitangaza huruma ya Mungu iliyopatikana kwa kila mtu kwa sababu ni mpango wa Mungu kwamba wokovu wake ufikie wote. Basi ishara ya Yohane ilikuwa kipimo cha kupita kutoka katika dhambi na mauti kwenda katika neema na maisha mapya ya Mungu. Kipengele muhimu katika tendo hili la Yohana ni kwamba aliwabatiza wale waliomhitaji Mungu na kutubu dhambi zao. Yohane na watu hao waliamini kwamba ndiye Mungu anayesamehe dhambi zao.

Ubatizo wa Yohane ni tofauti na ubatizo wetu, lakini yote mbili ni nafasi ya kuishi maisha mapya. Kwa upande wetu maisha mapya ni zawadi ya Kristo na matokeo ya utume wake. Ubatizo wa Kikristo, pamoja na maondoleo ya dhambi, unadhamini ushiriki katika uzima wa Mungu mwenyewe. Ubatizo ni wa kwanza kati ya sakramenti tatu za mwanzo ukifuatiwa na Kipaimara na Ekaristi. Ubatizo wetu ni ishara ya nje ya kufa kwa maisha ya dhambi, na tena ndiyo ishara ya ufufuko wa maisha mapya katika Kristo aliye mshindi dhidi ya dhambi na mauti. Yeye ni mwanga wa kweli ambao unamtia nuru kila mtu. Kupitia mwendo huu tumekuwa wana wa nuru ili tutembee katika nuru ya Mungu kila siku ya maisha yetu.


Kipindi cha Majilio kinatusaidia kujiandaa kusherehekea kuzaliwa kwa Yesu. Wakati ulimwengu wa biashara unashauri watu wajiandae kwa Noeli kwa kununua vitu, kipindi cha Majilio kinatupendekezea matayarisho ya kiroho na hamu ya kuishi kupatanishwa na Mungu na wenzetu. Kuna vikwazo vya kuondoa katika maisha yetu kwa msaada wa neema ya msamaha wa Mungu. Kwa hivyo tuchukue wakati mzuri huu kuadhimisha msamaha wa Mungu kwa sacramenti ya Upatanisho (na kitubio) na kuishi kwa njia mpya uhusiano wetu na Mungu na wengine.

Fr Ndega

Nenhum comentário: