sábado, 17 de novembro de 2018

KUNA TUMAINI KWA WAKATI UJAO WETU



Kutafakari kuhusu Dan 12: 1-3; Waeb 10: 11-14; Mk 13: 24-32


Tuanze tafakari hii tukijiuliza swali moja: “Je, Wakristo wanapaswa kuwa na tabia gani wakati wa mazingira magumu na mbele ya kosa la uhakika lililo tabia ya wakati huu? Sisi tu watu wa tumaini kwa sababu maisha ya mtu anayemfuata Yesu yamejaa maana. Basi, ujumbe wa liturgia hii ni msukumo kwetu tulioalikwa kutoa maana za tumaini letu kupitia imani yetu katika Kristo. Uhakika wa ukaribu wake ndio nguvu yetu. Tukikumbuka kwamba leo ndiyo Siku ya Kidunia ya Maskini, tunataka kuwa manabii wa tumaini dhidi ya utabiri wa kukata tamaa ambao unatuzuia kupanga wakati mwema kwa maskini wa jamii yetu. Jambo hili lina uhusiano gani nasi? Baba Mtakatifu Francisco anatuambia kwamba: “Manabii wako upande wa maskini kwa sababu wanajua ndipo katika upande huu kwamba Mungu ako”.  
   
Somo la kwanza linalotokana na kitabu cha nabii Danieli ni ufunuo kuhusu hukumu na ufufuko. Hilo ndilo mojawapo kati ya maandiko ya Agano la Kale yanayoongelea imani katika ufufuko (angalia pia 2 Mac 7, 9). Watu wa Israeli walitumwa na Wagiriki na kuteseka sana. Wengi miongoni mwao waliacha kumwamini Mungu, lakini wengine ambao waliendelea kumwamini walihitaji ujumbe wa tumaini na kutia moyo ili kuendelea safari yao kwa uvumilivu. Mungu ndipo daima kati ya watu wake na kuwasaidia mbele ya mazingira magumu ambayo wanakabiliana. Tendo lake kupitia malaika yake linahakikishia ukombozi na tena uzima kwa wale ambao walikufa kwa sababu ya kumwamini Bwana na kutenda mema hadi upeo.

Kulingana na somo la pili toleo la Kristo lilishinda dhabihu zote za makuhani wa Agano la Kale. Dhabihu zao zilitendeka mara nyingi wala hazikuwa na nguvu ya kuondoa dhambi za watu, yaani zilikosa ufanisi. Kwa upande wa Kristo, hali ni tofauti. Toleo lake lilitendeka mara moja tu nayo ilitosha kwa kuwatakasa watu wengi katika nyakati zote kwa sababu alijitolea mwenyewe. Katika kila misa takatifu tunasherehekea fumbo la toleo hii. Ndiye Kristo mwenyewe ambaye anatuhusisha katika mwendo huu kwa ajili ya wokovu wetu na wa wengine.

       Mwanzoni mwa sura ya kumi na tatu ya injili hii ya Marko Yesu aliongea kuhusu uharibifu wa Yerusalemu. Ufunuo huu uliwaimarisha baadhi ya wanafunzi wake wamwulize kuhusu ishara gani na siku gani na saa gani ya uharibifu huu. Kisha, Yesu alitumia nafasi hii ili kuongelea mambo mengi yatakayotokea na haja ya ushuhuda ili kukutana naye tena na kushiriki katika furaha yake. Aliporudi tena atawakusanya wateule wake kutoka dunia nzima. Alitabiri kwamba “nguvu za mbingu zitatikiswa” akimaanisha kwamba miungu ya uongo, yaani jua, mwezi, itapoteza mwanga wao. Hata wale waliojiona watu wa kimungu (nyota za angani) ambao wanawatesesha watu wa mataifa hasa walio maskini, hao (miungo ya uongo) wataanguka na mtazamo wa wote utamwelekezea Mwana wa Mtu akija amejaa nguvu na utukufu kama mshindi. Hakuna mtu anayejua wakati kamili ambao mambo yote yatatokea ila Baba peke yake. Kwa hivyo ni lazima kumwamini yeye.

         Ingawa uharibifu wa mji wa Yerusalemu ulitokea katika mwaka wa 70 B.K., nia ya Yesu haikuwa kuwajulisha kuhusu tukio hili, bali kuhusu matokeo ya tukio hili maishani mwa wafuasi wake. Ni lazima kutafakari injili hii kulingana na mazingira ambayo jumuiya ya Marko ilikuwa inaishi, yaani wanafunzi wa Yesu waliishi kipindi cha machafuko na kujaribiwa kukata tamaa kuhusu utambulisho wao wa wafuasi kwa maana ya majaribio na mateso mengi. Hao walijiuliza: “hayo yatokeayo yamaanisha nini?”. Mbele ya hali hii mwinjilisti aliwakumbusha mafundisho ya Yesu yasemayo kwamba baada ya mambo yote wanafunzi watakuwa washindi kama mwalimu kwa sababu ya uvumilivu wao mpaka upeo. Bwana wa Mtu ndiye msingi na lengo la historia. Kwa hivyo historia haiendi kwa mwisho bali kwa lengo kamili: Yesu Kristo mwenyewe.

        Andiko hili linatuambia kwamba Kristo ni mshindi na atafanya kuwa washindi wale ambao wanamfuata. Ujio wake mara ya pili utaanzisha historia mpya na ubinadamu mpya. Yeye anataka kushiriki na wanafunzi wote watakaobaki wamesimama kupitia imani na ushuhuda kwa uaminifu. Maneno yake yatuambia kuwa mazingira magumu ni sehemu ya safari ya wale ambao wanamfuata katika nyakati zote, lakini tena yatuhakikishia kwamba ikiwa tunabaki tumesimama kwa uvumilivu mpaka upeo tutaokolewa. Kuhusu wakati huu, hakuna mtu anayejua. Hii ni sehemu ya mpango wa hekima na wema wa Baba. Kwa hivyo ni lazima kumwamini yeye ambaye anaiongoza historia ya kibinadamu kwa lengo kamili. Tuko mikononi mwake; kwa hivyo tuko katika mikono mizuri”. Ujumbe huu unatoa tumaini kwa maisha yetu. Sisi tulioalikwa kuendelea utume wa Mwana wake Yesu, tunapaswa kuwa macho kwa ishara za uwepo wake ambazo zimetokea kati yetu. Ili hali mpya ikatokee maishani mwetu, miungu mingi ya uongo yapaswa kuanguka na kupoteza thamani yao. Kwa maneno mengine, tunapaswa kuacha picha za uongo za Mungu, mawazo na tabia ambayo inayapinga mafundisho ya injili. Tuishi wito wetu kwa shauku na furaha kwa sababu kuna tumaini kwa wakati ujao wetu.

Fr Ndega

Nenhum comentário: