domingo, 16 de julho de 2017

MBEGU ZILIANGUKA PENYE UDONGO MZURI NA KUZAA MATUNDA MAZURI


Kutafakari kutoka Mt 13, 1-23



        Tunataka kutafakari juu ya ufanisi wa Neno la Mungu katika maisha yetu na majibu yetu mbalimbali mbele ya tendo la neno hili. Kulingana na maneno ya nabii Isaya, neno la Mungu ni kama mvua na theluji ambazo hazimrudii Mungu bila kuipandishia ardhi na kuifanya kuota (angalia Isaya 55:10). Hivi ndivyo Neno la Mungu katika maisha yetu liko. Mungu anapoongea, yeye huumba na kuumba tena, yaani, anatoa uhai kulingana na mapenzi yake. Picha nyingine ambayo tunataka kutafakari kwa kina ndiyo “mbegu”, ambayo huleta nguvu kubwa ndani yake yenyewe, lakini inahitaji mazingira mazuri ya kuzaa matunda. Lengo la Neno ndilo kuyatimiza mambo yanayompendeza Mungu, yaani, mabadiliko ya maisha yetu.

      Katika mwanzo wa injili, watu walikusanyika ili wasikilize Neno la Mungu kwa kinywa cha Yesu. Tunajua kwamba Katika tangazo la Ufalme wa Mungu, Yesu alipendelea kutumia lugha rahisi ili watu waweze kuyakaribisha mafundisho yake vizuri sana. Yeye aliitumia mifano kuihusu hali ya kimungu na hali ya kibinadamu. Alianza akitumia ishara ambazo watu walizijua na baadaye hatua kwa hatua aliwafunulia upya wa hali ijayo. Hivyo, Yesu aliwafanya watu waone, kwa matarajio, uzima ambao anaahidi, akiongeza matumaini ya wokovu moyoni mwao. Yule ambaye anaongea maneno ya uzima wa milele anataka kusikika, lakini makaribisho hayakuwa sawa kwa upande wa wasikilizaji wake. Kama matokeo, maneno ya Yesu hayakuweza kusababisha mabadiliko aliyotarajia. Haya ndiyo mazingira ambayo mfano wa mpanzi ulizaliwa.

       Kuhusu watu ambao walisikia mifano yake, Yesu alisema, “Mtasikia, lakini hamtaelewa. Mtatazama, lakini hamtaona.” Kwa upande wa wanafunzi wake, Yesu alisema: “Heri yenu nyinyi, maana macho yenu yanaona na masikio yenu yanasikia”. Basi, ikiwa lengo la mifano ni kuwa lugha rahisi ili watu wafahamu siri za Ufalme, kwa nini Yesu alianzisha tofauti kati ya wanafunzi wake na watu wengine? Ndiyo kwa maana wanafunzi wake walikubali mafundisho yake kwa moyo ambao umefunguliwa na kuishi kulingana na mapenzi ya Mungu. Wengine walikuwa na tabia tofauti. Hao walimpinga Yesu tangu mwanzo. Katika Yesu hali ya ufalme imekuwa halisi kupatikana; upinzani dhidi yake ni upinzani kwa mafanikio ya ufalme huu. Tufikirie sasa mfano wa mpanzi.

     Mpanzi alikwenda kupanda mbegu zake nyingi na mbegu zile zilianguka katika mahali mbalimbali. Kama mpanzi huyo, ndivyo Mungu anavyofanya kwa midomo ya Yesu. Yeye ameongea sana na Neno lake lina nguvu ya kuumba na kuzaa maisha mapya. Kwa upande wa Mungu anaona furaha kubwa kuwaambia watu wake kitu. Kila mazungumzo na Yesu ni mwaliko wa kufikiri na kutenda tofauti. Mbegu ni Neno la Mungu. Nia ya Yesu ilikuwa kuongea kuhusu nguvu ya neno lenyewe na kwamba ni lazima kulisikiliza kwa uangalifu ili neno hili liweze kutimiza mapenzi ya Mungu maishani mwa watu. Katika Biblia neno kusikiliza linamaanisha vitendo viwili, yaani, kusikia na kuishi/kushika. Kuhusu mahali pengi, tunafikiria tabia mbalimbali za watu mbele ya Neno la Mungu na tena matokeo mbalimbali katika hali ya kawaida.

     Mbegu zilizoanguka njiani zinaonyesha kwamba mara nyingi tunaposikia Neno la Mungu, bila ahadi kwa Neno hili tunaruhusu ibilisi aliondoe neno lililopandwa mioyoni mwetu. Tendo letu hili linaiondoa maana ya Neno. Mbegu zile zilizoanguka penye mawe zinaonesha kwamba tunaposikia Neno la Mungu tunapokea kwa furaha, lakini kwa sababu ya imani ndogo sisi husadiki kwa muda mfupi tu, na tunapojaribiwa sisi hukata tamaa. Zile zilizoanguka kwenye miti ya miiba ni tunaposikia neno la Mungu, lakini wasiwasi, mali na anasa za maisha zinatuzuia tubadilishe tabia zetu.  Zile zilizoanguka kwenye udongo mzuri ni tunapolisikia Neno la Mungu na kulikaribisha vizuri kwa kuyafananisha maisha yetu kulingana na neno hili. Lakini hali hii ni tendo la Neno lenyewe kwa neema ya Mungu kwa sababu neno la Mungu “ni ufanisi na halimrudii yeye tupu.”


         Kulingana na andiko hilo, kuna tofauti kati ya moyo wa wanaomfuata Yesu na wengine wanaomsikiliza tu. Njia ya kupanda mbegu ni mfano wa ukarimu wa Mungu. Kwa upande wake hakuna mipaka; ni ukarimu tu. Kutoka ukarimu wake tumepokea neema juu ya neema, lakini uwezo wetu wa kuipokea neema yake ni mdogo sana. Hata hivyo, ikiwa tuko tayari kulisikiliza na kulishika neno la Mwanawe, Mungu mwenyewe anazidisha uwezo na ukarimu wetu ili tuweze kusonga mbele kwa matendo mema mengi kulingana na matarajio yake. Tena na tena tunahitaji kufahamu kwamba Mungu anatarajia mafanikio yetu, lakini uamuzi ndio wetu. Tukaribishe pendekezo la Yesu kwa utayarisho wa moyo ili tuweze kupata maisha mapya ambayo Neno lake linatoa.

Fr Ndega
Mapitio ya Kiswahili: Christine Githui

Nenhum comentário: