domingo, 23 de julho de 2017

KUIFUATA NJIA YA MUNGU ILI KUONDOA UOVU WA ULIMWENGU


Kutafakari kuhusu Hek 12, 13.16-19; War 8,26-27; Mt 13, 24-43


       Kulingana na tafakari yetu katika wiki iliyopita, kati ya mbegu zilizoanguka kwenye ardhi, moja peke yake ilipatikana kuwa hali nzuri ili kupokea mbegu njema na kuzaa matunda. Mbegu njema ni neno la Mungu ambalo lina nguvu ndani yake ili kuzaa maisha mapya katika mahali linapokaribishwa. Kulingana na andiko la siku ya leo, hata ikiwa ardhi ni sawa, inaweza kupatikana magugu pia. Magugu ni mfano wa ishara za mauti ambazo tunaweza kukuta mahali ambapo ishara za maisha zipo. Hali hii inamaanisha kwamba hata ikiwa moyo fulani ni mwema unaweza kubeba mbegu ya uovu, yaani unaweza kuwa na mwelekeo mbaya. Adui ya Mungu atatenda daima kuwazuia watoto wake waishi kulingana na mapenzi yake.

          Andiko la Hekima ni wimbo unaoongelea wema na uvumilivu wa Mungu kwa watoto wake wote. Enzi na nguvu yake haimzuii kutenda kwa upole na upendo, akiwatunza wote, hasa wale wasio na nguvu. Akitenda hivyo, aliwaelimisha watu wake akiwapa nafasi ya toba na mabadiliko ya maisha ili yawe kulingana na matarajio yake. Mungu ndiye mwenye huruma na mvumilivu kwa sababu anapenda kwa  upendo wa milele, yaani upendo unaotoa tumaini zuri kwa kufungua milango ambayo tumefunga kwa sababu ya makosa yetu. Tunahitaji upendo huu na tunataka sana kupenda kama Mungu alivyo. Hilo ndilo tendo la Roho wake anayekaa ndani yetu ili tujifunze kuomba kwa imani ya watoto, kwa kutamani moyoni mwetu Mungu anayetamani ndani yetu.

         Mfano ambao Yesu anatujulisha unaongelea mwendo wa Ufalme ulio kama mtu mmoja aliyepanda mbegu njema katika konde lake, lakini wakati wa usiku adui yake alikuja na kupanda pia magugu kati ya ngano. Tunataka kutafakari kidogo juu ya tabia mbili, yaani: tabia ya kosa la uvumilivu kwa upande wa watumishi na uvumilivu wa mwenye konde (mbele ya tendo la adui na ya kutokomaa kwa watumishi). Nia ya Yesu ni kuongelea Mungu kama Yule anayepanda mbegu njema katika konde kubwa la ulimwengu wala hawezi kufanya tofauti maana yeye ndiye mwema. Adui yake alipanda magugu, yaani mbegu mbaya. Je, inawezekana kufanya nini kwa magugu haya? Mwenye konde ana mpango mmoja, lakini anapendelea kusubiri na kutenda katika wakati mwafaka, yaani katika wakati wake mwenyewe. Adui aliyepanda magugu alitenda katika usiku, yaani amefichwa. Matendo dhidi ya mapenzi ya Mungu yaonyesha hali za giza maishani mwetu.     

         Ni wazi katika andiko hili kwamba uovu hautoki kwa Mungu; yeye hataki uovu. Yeye mwenyewe anawaimarisha wanafunzi wa Mwanawe waangalie njia yake ya kutenda kwa kuondoa uovu wa ulimwengu na wa maisha yao. Kwa bahati mbaya, binadamu anabeba pia uovu ndani yake pamoja na wema unaotoka kwa Mungu. Haikuwa hivyo tangu mwanzo. Mungu alifanya binadamu kama mtu mwema na mwenye uhuru ili aweze kuchagua, yaani “Mungu alimwambia binadamu, ikiwa unachagua wema na uhai wewe utaishi milele; ikiwa unachagua uovu na mauti wewe utakufa.” Wakati uhuru wa binadamu ‘haufanywi upya na injili’ unaweza kutenda kama adui. Basi, kama matokeo ya uamuzi wa kibinadamu, wema na uovu umekua pamoja ulimwenguni. Mara nyingi uovu unaonekana wenye nguvu kuliko wema kwa sababu tunaulisha zaidi. Tena mara nyingi tumeshangaa tunapoona kwamba mtu fulani anayeonekana mwema ndiye mbaya na yule anayeonekana mbaya ndiye mwema. Kwa matarajio siyo mazuri na kwa haraka tuko na mazoea ya kuwahukumu wengine. Tendo hili siyo kazi yetu.

          Kulingana na mwendo wa mfano huu, ni lazima kuwa na uvumilivu na utambuzi ili kuondoa uovu katika wakati mwafaka na kwa matendo kamili ili yaweze kuimarisha wema pia na sio kupunguza nguvu zake. Ndiyo katika hali hii ya wema na uovu ambayo thamani za Ufalme zilipandwa. Kama Mungu ndiye wa kwanza kwa nia ya kuondoa uovu wa ulimwengu, yeye mwenyewe anatualika kusubiri kwa uvumilivu kwa kujifunza kutoka kwake ambaye anawanyeshea mvua watu wa haki na wasio na haki ama watu wema na wabaya. Kwa uvumilivu wake Mungu ametupa nafasi nyingi za toba na mabadiliko ya maisha. Basi, kuwa na uvumilivu sio kukubali uovu bali kuifuata njia ya Mungu ambaye ana milele mbele yake na kujua jinsi ya kubadilisha uovu kuwa wema kwa sababu anajua jinsi ya kupenda. Kweli huu ndio mwaliko tubadilishe mtazamo wetu kwa kutenda kulingana na moyo wa huruma ya Mungu.


Fr Ndega
Mapitio ya Kiswahili: Christine Githui

Nenhum comentário: