domingo, 2 de julho de 2017

KUMFUATA KRISTO KWA UPENDO KAMILI NA WA KIPEKEE


Kutafakari kuhusu 2Waf 4,8-11.14-16a; Mt 10: 37-42


       Mungu anampenda binadamu kwa hiari na bure, yaani halazimishwi kupenda wala anamlazimisha binadamu ampende yeye. Lakini anatarajia tu upendo wa binadamu kwake ufuate njia yake ya kumpenda. Nabii Elisha alitumwa kwenye Shunemu kutembelea wanandoa ambao hawakuwa na mtoto. Mwanamke mwenye nyumba alimkaribisha vizuri akimtambua kama mtu mtakatifu wa Mungu. Pamoja na mumewe walimtendea nabii mema kama mshiriki wa familia yao. Kwa sababu ya ukarimu wake, nabii Elisha alimpatia zawadi ya kumzaa mtoto mmoja. Kujitolea kwake mwanamke kwa ajili ya nabii Elisha ni kwa sababu aliweza kutambua katika mtu huyo maonyesho ya upendo wa Mungu mwenyewe aliyepanga kusababisha hali mpya maishani mwake.

        Katika injili Yesu anaomba upendo kamili na wa kipekee kutoka kwa wanafunzi wake, yaani “Ampendaye baba au mama yake kuliko anipendavyo mimi, hanistahili. Ampendaye mwana au binti kuliko mimi, hanistahili. Mtu asiyechukua msalaba wake na kunifuata, hanistahili.” Kama mwendelezo, yeye aliongeza haja ya kuyasalimisha maisha kwa ajili yake. Inamaanisha kwamba kwa Yesu upendo ni kujisalimisha kwa ajili yake. Wazazi na familia nzima ni zawadi ya Mungu, lakini hawawezi kuchukua nafasi ya Mungu katika maisha ya wanafunzi. Hakuna upinzani kati ya upendo kwa Mungu na kwa wazazi, lakini ni tofauti na tena Yesu anaomba kwamba upendo kwa ajili yake uwe kipaumbele kwa sababu ndio upendo huu unaozaa upendo kwa ajili ya wazazi na ya wengine. 

        Kabla ya andiko hili, Yesu alikwisha sema kwamba hakuja kuleta amani bali kuleta upanga unaowaimarisha watu kuchukua uamuzi katika familia na kumhusu Mungu. Upendo ambao Yesu anaomba kutoka wanafunzi wake unatukumbusha mazungumzo ambayo Yeye alimwuliza Petro kwa mara tatu kuhusu upendo wake, yaani “Simoni, mwana wa Yohane! Je, wanipenda mimi kuliko hawa?” Naye akajibu, “Bwana, wewe wajua yote; wewe wajua kwamba mimi nakupenda.” Ingawa Yesu anajua udhaifu wa wanafunzi wake, anaomba upendo “mara tatu”, yaani “kamili”, maana yeye mwenyewe anawawezesha wanafunzi kupenda hivyo. Yeye anajitambulisha na wanafunzi wake na kwa hivyo anawaalika kuchukua ahadi ya kumpenda hadi mwisho kama yeye alivyo.

        Maneno yake yalikuwa nafasi ya kutafakari kwa kweli maana ya safari yao. Yesu ni wazi sana akiwajulisha masharti ili wawe wanafunzi wa kweli. Hivyo, alizuia kwamba wamfuate kwa njia yoyote. Ikiwa wanataka kupata mafanikio katika safari yao wanapaswa kuchukua matokeo ya uamuzi huu. Hapo tuko na jambo la msalaba ambao ni ishara ya upendo wa Yesu mpaka upeo na tabia ya wanafunzi ambao wanajitambulisha na mwalimu wao. Pendekezo la Yesu linajumuisha kujinyima, kwa sababu yeyote anayekutana na Yesu kwa kweli amekwisha pata hazina ya kweli kwa maisha yake naye hawezi kubaki alivyo, yaani mambo mengine hayana maana tena. Kwa maneno mengine, Yesu anataka kuwa kipaumbele maishani mwa wanaoamua kumfuata. Hakuna jambo lingine ambalo liweze kuitoa maana ya kweli kwa maisha yao ila Yesu mwenyewe.


        Kama wanafunzi wapya wa Yesu sisi tunaalikwa kumtegemea Mungu katika mambo yote na kumpenda juu ya yote kama Yesu alivyo. Yeye anatukabidhi ufalme wake na kutujulisha njia ya msalaba ili tuweze kufanya mapenzi ya Baba yake. Kupitia njia hii, tunatambua kwamba Kumfuata Yesu hakuuleti upendeleo au hadhi, bali nafasi ya kujisalimisha kwa upendo kwa ajili ya ufalme wa Mungu. Basi, yeyote ambaye anataka kuishi shwari na bila ahadi hawezi kumfuata Yesu. Tena yeyote ambaye anatamani kumfuata Kristo bila msalaba hatamfuata Yeye kwa kweli kamwe. Kuchukua msalaba ni ishara ya utayari wetu wa kuyakaribisha mapenzi ya Mungu kwa maisha yetu. Kwa kufikia lengo hili tunapaswa kujikana ili Mungu aweze kujifunua kwa nguvu yote ya upendo wake. Kuacha mahali muhimu ama nafasi ya kuwa rejeo ni njia kamili ili tuweze kuwapa wengine nafasi zaidi. Kwa maneno mengine, tunapaswa kuwafikiria wengine kuwa wa muhimu kuliko sisi wenyewe. Tukifanya hivyo hakika tunaweza kumfuata Yesu kwa upendo kamili na wa kipekee.

Fr Ndega
Mapitio ya kiswahili: Christine Githui

Nenhum comentário: