domingo, 30 de julho de 2017

FURAHA KUBWA NA KAMILI


Kutafakari kuhusu Mt 13, 44-52


             
           Sura kumi na tatu ya injili ya Mathayo inajulisha mifano mingi ya Yesu ili kuonyesha kwamba hali ya Ufalme wa Mungu siyo mbali na hali zetu bali inatokea miongoni mwetu na ndani yetu. Baada ya mtaguso wa Vaticano wa pili, baba mtakatifu Paulo wa VI aliandika waraka mmoja unaoitwa Evangelii Nuntiandi akiwaimarisha Wakristo kwa kazi ya kueneza injili kwa njia mpya. Kati ya mambo ya waraka, yeye alitaja jambo la ufalme wa Mungu/mbinguni, akisema, “Ufalme ambao injili inatangaza huchukuliwa na watu walio wa utamaduni halisi kwa njia ya ndani. Haiwezekani kujenga ufalme huu kwa kuacha thamani za ustaarabu na tamaduni za kibinadamu” (EN 20). Kwa maneno mengine, hali ya ufalme inachanganyika na hali yetu. Thamani za ufalme zinapaswa kuwa rejeo la maisha yetu. Kwa hivyo Yesu anatujulisha siku ya leo mifano mitatu.

         Katika mfano wa kwanza ufalme wa mbinguni unafanana na hazina iliyofichika na kukutwa shambani; wa pili, unafanana na lulu nzuri kuliko nyingine zote; na tatu, na wavu uliotupwa baharini, ukanasa samaki wa kila aina. Mifano miwili ya kwanza inadhihirisha kwamba Ufalme wa mbinguni ni hali inayopatikana, lakini ni muhimu pia kuitafuta hali hii. Kulingana na utabiri wa nabii Isaya, ndiye Mungu mwenyewe anayepatikana na kwa hivyo tunaalikwa kumtafuta. Anasema Carlo Dellari kwamba, “Sio sisi tuliomfikia Mungu ili kumjua bali ndiye yeye aliyetutangulia katika mkutano na kutuimarisha kutembea ili kukutana naye. Mtakatifu Agustino alikwisha sema uthibitisho huu wakati ulipomfanya Bwana kusema maneno haya, yaani ‘wewe haungenitafuta ikiwa haungalikwisha nikuta mimi’”.

     Basi ufalme sio muundo wa nguvu kama falme za nchi bali ni tendo la Mungu mwenyewe ambaye anapatikana kwa wote. Lakini sio wote ambao wanapatikana kukutana nawe. Ufalme huu una thamani sana na husababisha furaha kubwa katika maisha ya mtu ambaye aliugundua ama aliukuta. lakini kwa ajili ya furaha hii mwanafunzi anaalikwa kujinyima kila kitu, yaani kuacha mahali, mali na “usalama” wa uwongo kwa sababu “bila juhudi za kutafuta na kujinyima, furaha ya mkutano haiwezekani." Uzoefu wa kugundua ufalme kama hazina ni uzoefu wa kukuta maana ya kweli ya maisha. Hali nyingine haina maana tena. Furaha tunayoiona ndiyo matokeo ya chaguo letu.

      Katika mfano wa tatu Yesu alifananisha ufalme na wavu uliotupwa baharini ambao unanasa samaki ya kila aina. Mfano huu unadhihirisha kwamba Mungu ana mpango wa wokovu kwa wote kwa sababu anataka kuwakaribisha wote katika ufalme wake. Lakini ni lazima hukumu iwe kwa sababu makaribisho ya pendekezo lake si sawa kwa wote. Kulingana na maana ya mfano huu, katika mwisho wa nyakati wabaya hawatakuwa na nafasi sawa na wema. Kila mmoja atakuwa na nafasi ambayo alichagua kulingana na maisha aliyoishi. Lakini hakuna sababu ya kukata tamaa kwa maana Mungu anataka kuwaokoa wote na kutuimarisha kutafuta kwanza ufalme wake kama chaguo kamili. 


       Basi, Huu ndio mwendo wa kumfuata Yesu. Yeye ndiye hazina yetu ya kweli. Anatuvutia kwake kwa sababu ya wema, ukweli, uvumilivu na unyenyekevu wake. Yule ambaye anakutana  na Kristo habaki alivyo kwa sababu alikuta lile ambalo linatoa maana kwa kila kitu. Kweli mkutano unaweza kubadilisha maisha yetu kabisa kwa sababu unaleta njia tofauti ya kuona na kutenda. Furaha ndio matokeo ya mkutano naye na kumchagua kama rejeo la pekee la maisha yetu. Yesu alitushirikisha Ufalme wake nasi tunaalikwa kujikabidhi mikononi mwake kwa ajili ya kuchagua vizuri katika kila kitu. Yule ambaye alimchagua Kristo yeye alichagua ufalme ulio hali ya ahadi ya kindugu, ya amani na ya upatanisho. Ndicho kipimo cha furaha kubwa na kamili. 

Fr Ndega
Mapitio ya Kiswahili: Christine Githui

Nenhum comentário: