sábado, 25 de fevereiro de 2017

“MUNGU YU BABA, MAMA NA YOTE”


Kutafakari kuhusu Isa 49,14-16; Mt 6,24-34


        “Kwa njia yake ya kututunza Mungu yu mama kuliko baba”. Maneno haya yalisemwa na baba mtakatifu Yohane Paulo wa Kwanza na kuonyesha mtazamo tofauti kuhusu hali ya Kimungu, kulingana na andiko la kwanza la tafakari yetu (Isa 49,14-16). Mungu ni kama mama ndiye mpole na mwangalifu. Yeye hawezi kutusahau kwa sababu sisi tu watoto wake wapendwa na maisha yetu yanathamini sana kwake. Anataka tuonje upendo wake wa kimama nasi tuweze kujikabidhi mikononi mwake kwa imani kubwa. Mtakatifu Yohane Calabria alikuwa na haya ya kusema, “Riziki ya Mungu ni kama mama mpole anayepatia mambo yote kwa manufaa yetu sisi. Tujione kuongozwa na mikono yake ya kimama.” Yeyote anayeishi imani kama hiyo anaweza kuenda mbele akitangaza Ufalme wa Mungu kama kipaumbele katika maisha yake.  
         Kwa wale walioamua kumfuata Yesu ni lazima kupanga maisha yao kulingana na hali mpya ambayo walichukua. Hawawezi kutumikia mabwana wawili. Kumtumikia Mungu ni muhimu kuliko mambo yote. Hivyo, baada ya kukutana na Kristo, pesa na mali zingine hazina maana tena maishani mwao kama ilivyotokea kabla ya mkutano huu. Ilikuwa hivyo mwanzoni mwa wito, yaani Yesu aliwaita; mara waliacha kila kitu... Lakini tunajua kwamba, wakati wa safari, mara nyingi walikuwa na hofu na mashaka kuhusu kesho, mfano Petro alipomwambia, “Na sisi je? Tumeacha yote, tukakufuata wewe; tutapata nini basi?” (Mt 19,27). Yesu alijua mahitaji yao na kwa hivyo, akawahakikishia maisha mapya ambayo yanajumuisha mambo hayo yote kwa njia tofauti na iliyo bora, pamoja na kujitolea kwao kwa ajili yake.  Kulingana na Mtakatifu Augustino, “Petro aliacha ulimwengu wote na akapata ulimwengu wote. Walikuwa kama wale ambao hawakuwa na kitu, wakati huo wana kila kitu.”
        Umuhimu wa mafundisho ya Yesu katika andiko hili ni utunzaji wa Mungu kwa ajili ya watumishi wake. Yeye ndiye Baba mwema anayejua mahitaji ya wanae na kuwasaidia bora kuliko anavyofanya kwa ajili ya ndege na maua ya mashamba. Yesu aliwaalika kufungua macho na kuangalia kandokando yao. Katika Vyote kuna ishara za upendo ya Baba huyo ambaye anashughulika hata kwa mambo madogo. Anayaongoza mambo yote kulingana na mpango wake wa hekima na wema. Hakuna jambo ambalo linakosa mtazamo wake wa upendo. Hivyo, tunaalikwa kufikiria kwamba tuko mikononi mwake ambapo ni pazuri. Maandiko Matakatifu yanashuhudia hivyo, yaani “Mpaka sasa hivi Bwana ametusaidia”, na tena “Ni nani aliyetumaini Bwana akaaibika?.” Ushuhuda huu unatualika “kunaangalia ya nyuma na kuona jinsi Mungu alivyotutendea mema na hivyo tunaweza kuona yale anayotufanyia sasa. Hivyo, tunaweza kuangalia mbele kwa matumaini na imani kwamba Mungu atatutendea vile alivyotutendea”. Hii ni njia yake ya kutenda.
Yesu hakanushi kwamba baadhi ya mambo ni muhimu kwa maisha. Lakini anajua pia kwamba mtu anayeishi kwa wasiwasi na kusumbulika anakosa uangalifu katika yale yasiyo muhimu sana. Ikiwa Mungu Baba anajua kwamba tunahitaji mambo hayo yote na kutusaidia, tunaalikwa kujisalimisha mikononi mwake kwa imani kubwa na kuzitumia juhudi zetu kwa ajili ya kujenga ulimwengu bora kila siku. Mtakatifu fulani alisema: “Tufanye tunayopaswa kufanya kama yote yanatutegemea sisi, kwa kumwamini Mungu kama yote yanamtegemea Mungu.” Mtakatifu Yohane Calabria aliishi hali hii kwa hamu sana. Ugunduzi wake wa injili ulikuwa ugunduzi wa ubaba wa Mungu. Kwa Yohana Calabria, Mungu ni Baba na Mtoaji daima ingawa hatujaishi kama watoto daima. Alichukua maneno ya mstari wa 23 kama mpango wa maisha kwake na kwa Familia yake ya Kiroho, yaani, “Mtafuteni kwanza Ufalme wa Mungu na haki yake na hayo yote mtapewa kwa ziada.” Kwa mtakatifu huyo, hapo tuko na njia halisi ya kumjibu Mungu anayewapenda na kuwalinda wana wake bila kumsahau hata mmoja wao. Kwa hivyo, kama kutafuta kwa ufalme wake kunayaongoza maisha yetu, “matatizo yote yapaswa kufikiriwa na kusomeka kwa maelewano na ubaba wake” na kamwe nje yake.

     Mungu anatupenda, yeye anatujua na kwa hivyo anatutunza. Kwa utunzaji wake maalum, yeye ameshiriki zawadi zake nasi, akitarajia tuweze kufanya vivyo hivyo kwa ajili ya wengine ili undugu kati yetu uwe maonyesho ya ubaba wake. Basi, tunaalikwa kuchukua historia yetu ya maisha na kutambua kwamba tumepokea sana. Ingawa sisi hatupokei daima yale tunayomwomba yeye, tuwe na uhakika kwamba yeye ametupatia daima tunayohitaji. Hivyo, tufanye upya imani yetu katika riziki yake kwa maana yeye yu BABA, MAMA, YOTE naye hawaachi wale wanaomtumainia.

Nenhum comentário: