domingo, 15 de janeiro de 2017

PADRE NI ZAWADI YA MUNGU KWA UHAI WA JUMUIYA



Kutafakari kuhusu Is 49,3.5-6; 1Cor 1, 1-3; Yoh 1, 29-34

* Ubatizo wa mtoto Tamele na miaka kumi na mitano ya padre Josuel Ndega


       Tunataka kutafakari kuhusu shuhuda tatu ambayo inatusaidia kuishi vizuri wito wetu, yaani, kwanza, ushuhuda wa Mungu kuhusu mtumishi wake (somo la kwanza); pili, ushuhuda wa mtakatifu Paulo kama mtume kwa mapenzi ya Mungu (somo la pili); na tatu, ushuhuda wa Yohane Mbatizaji juu ya Yesu kama Mwana kondoo wa Mungu (injili). Tutalenga ushiriki wetu katika upadre wa Kristo.

    Kuhusu ushuhuda wa Mungu, huu ni mmoja wa nyimbo ya mtumishi wa Bwana iliyoandikwa wakati wa utumwa wa Babeli nasi tunaweza kuukuta wimbo huu katika sehemu ya pili ya kitabu cha Isaya. Ni jambo la ajabu njia ya Mungu ya kuongea kuhusu mtumishi wake. Kwanza kabisa kuna mpango. Mungu wetu hatendi kwa njia yoyote. Yeye anajua mtumishi wake kwa maana yeye mwenyewe alimwandaa tangu tumboni mwa mama yake na kumjulisha kwa upendo kwa sababu maisha ya mtumishi huyo yanampendeza. Mtu aliyeamua kuwa padre alichagua kuwa mtumishi na maisha yake yanampendeza Mungu kwa sababu hatafuti nafsi yake mwenyewe bali utukufu wa Mungu. Uhusiano wa upendo na Bwana wake ni maana ya uaminifu katika safari yake ya wito (cf. 1Sm 2,35). Huu ndio uzoefu unaozaa utambulisho na kutoa maana kwa utume, ukimsaidia kuishi wito wake kwa furaha. Kutafakari kuhusu wimbo huu ni nafasi ya kufanya upya ahadi yangu kama mtumishi nikimshukuru Mungu kwa zawadi ya upadre na kwa maana yupo pamoja nami daima.

       Maandiko matakatifu yanashuhudia kuhusu uaminifu wa Mungu kwa ajili ya watumishi wake kama njia yake mwenyewe ya kutenda na kama njia kamili ya kufanya mapenzi yake. Anajua kuhusu udhaifu ya watumishi wake; kwa hivyo, anabaki karibu na kutenda pamoja nao ili wawe waaminifu. Uaminifu wa Mungu ndio mwaliko ili tufanye vivyo hivyo. Huu ndio muhtasari wa maisha ya Mtakatifu Paulo katika somo la pili. Yeye anajua sana kwamba wito wake kama mtume wa Yesu Kristo ni mapenzi ya Mungu. Mtakatifu Paulo aliishi wito wake kwa hamu sana na kwa upatikanaji kabisa kwa ajili ya kuinjilisha. Ushuhuda wake wa maisha unatusaidia sana kufahamu maana ya ushiriki wetu katika upadre wa Kristo kupitia ubatizo. Kama wabatizwa sisi ni washiriki wa mwili wa Bwana nasi tunaalikwa kutenda kwa ajili ya kulijenga kanisa, ambalo ni mwili wake. Katika kila mmojawapo aliyebatizwa tunatambua uwepo wa kanisa zima. Kile kinachotokea katika maisha ya mmoja wetu ni jukumu la mwili mzima. Wito wetu tunaishi katika jumuiya moja, lakini kwa ajili ya kanisa zima.

    Mfano mwingine muhimu sana ni ushuhuda wa Yohana mbatizaji. Yeye aliweza kumtambua Yesu kama “Mwana kondoo wa Mungu aondoaye dhambi za dunia”, kwa sababu alikuwa macho kwa msukumo wa Mungu kama vile imetokea daima (tumboni mwa mama Elizabeth, jangwani, mtoni Yordani na kupita kwake Yesu, kulingana na andiko la leo). Kubatizwa ni kushiriki uhai wa Mungu kwa kuingia katika mwendo wa Roho Mtakatifu anayesababisha kuzaliwa upya na furaha kubwa katika familia yetu ya kiroho, yaani Kanisa. Kulingana na Baba mtakatifu Fransisko, “Kila mtoto anayezaliwa ni zawadi ya furaha na matumaini, na kila mtoto anayebatizwa ni muujiza wa imani nayo ni sikukuu kwa familia ya Mungu.” Jina linalotajwa wakati wa ubatizo linapokea maana mpya na utambulisho mpya. “Mungu mwenyewe anataka jina lako liwe jina lake la pili. Uingizwe katika orodha hii: Mungu wa Abrahamu, Mungu wa Isaka, Mungu wa Yakobo, Mungu wa Anna, Mungu wa Daudi,” Mungu wa Clementina, Mungu wa Josafá, Mungu wa Maria, Mungu wa Tamele.


      Yohane alisema mara mbili kwamba hakumjua Yesu, lakini kwa msukumo wa Mungu, aliweza kumtambua Mwanawe. Na baadaye Yohane alisema “niliona na kushuhudia”. Kuwa padre ni kuwa shahidi wa yale anayotenda Mungu duniani na maishani mwa watu. Padre ni mtu anayetafuta kumjua Mungu daima ili aweze kumtambua na kumwonyesha kwa wengine. Padre ni chombo cha huruma kwa maana yeye kwanza ameguswa na huruma hii. Upadre ni kama “Ubuntu”, yaani huu ni uzoefu ambao mtu anajiona mmoja na wenzake wa jumuiya, kwa maana kuwa padre ni kuwa ndugu kati ya wenzake na kwa ajili ya uhai wao. Tumshukuru Mungu kwa upadre!

Fr Ndega

Nenhum comentário: