domingo, 29 de janeiro de 2017

NJIA KAMILI YA KUPATA FURAHA YA KWELI


Kutafakari kutoka Sf 2,3;3,12-13; 1Cor 1, 26-31; Mt 5, 1-12



Tafakari yetu inasisitiza kwamba njia kamili ya kumtafuta Mungu inapitia kwa unyenyekevu na haki. Yeye hana macho kwa waliotenda udhalimu wala kwa wanafiki bali kwa wanyenyekevu na kwa maskini. Yeye yu makini sana kwa kilio chao naye yuko tayari kuwatendea mema kwa maana maisha yao yana thamani kubwa kwake. Kupitia Yesu, yeye anatoa maneno ya faraja akionyesha upendo maalum hasa kwa maskini na wanyenyekevu kwa sababu wanamtumainia yeye.  
Katika andiko la Kwanza, nabii Sefania anatambua ndani ya maskini na wanyenyekevu uwezo mkubwa wa kumtafuta Mungu na kumtegemea yeye katika mambo yote. Mungu anaijua hali ya maskini na ya wanyenyekevu naye anaguswa na mahitaji yao. Maisha ya maskini na ya wanyenyekevu yanashuhudia kimbilio ambalo linatuhakikishia usalama sio pesa wala ulaji/ukusanyaji, bali ni Mungu peke yake. Kweli Mungu anapatikana kwa wale wanaotaka kukutana naye, lakini ndio wanyenyekevu wa moyo tu wanaoweza kuuona uso wake. Bila tabia hii ni ngumu tukubali mipango ya Mungu kwa maisha yetu. Kulingana na Mtakatifu Paulo, sisi tulio jumuiya ya Kikristo, hatujaitwa kuifuata hekima ya kibinadamu wala kuutafuta umaarufu wa kijamii. Wito wetu unatoka kwa Mungu na kuyafuata mawazo na njia zake kama Kristo mwenyewe alivyo.    
Andiko la injili ni mwanzo wa ile iliyojulikana kama “Hotuba ya mlimani” iliyotangazwa na Yesu. Hotuba hii kabisa inajumuisha sura tatu, yaani, ya 5 hadi ya 7. Kwanza kabisa ni muhimu sana kuifahamu nia ya Mathayo alipoandika toleo lake. Yeye aliandika kwa Wayahudi na kwa hivyo, alimjulisha Yesu kama “Musa Mpya”. Mambo yote ambayo yanamhusu Kristo yanaileta hali mpya, yaani, Mlima wa “heri nane” unatukumbusha hali ya Mlima wa Sinai; ujumbe huu wa “Heri nane” ni mafundisho mapya kuhusu Amri za zamani; upendo wa kindugu ni haki mpya ambayo inashinda haki ya walimu wa Sheria na Mafarisayo, n.k. Tuko mbele ya hotuba ya kuuanzisha ufalme, yaani mapendekezo ya kupata furaha ya kweli kwa njia tofauti kabisa na matarajio ya jamii. Huu ni mpango wa maisha ambao Yesu aliishi kwanza kabla ya kupendekeza kwa wote. Nyuma ya heri nane tunaweza kukuta nafsi ya Yesu mwenyewe katika uhusiano wake na Mungu aliye Babaye. 
Wakati Yesu alipotangaza Ufalme wa Mungu kwa mara ya kwanza, aliamua kuhubiri maneno ya faraja kwa wale waliokuwa na mahitaji na mateso mengi na kumtumainia Mungu, yaani walio kipaumbele katika Ufalme. Tunahitaji kuchukua andiko hili la leo pamoja na lile la Luka linalosema kwamba kuwa maskini yatosha kuumiliki ufalme. Yesu alifanyika mwili kuonyesha ukaribu wa Mungu. Wale waliomkaribia Yesu mlimani walikuwa na moyo uliofunguliwa kwa ukaribu huu wa Mungu kwa maana walikuwa na tabia zinazompendeza. Watu Hawa walionyeshwa na nyuso nyingi, yaani, walio maskini wa roho ndio wasio na tamaa ya makuu bali wanaweza kuyasalimisha maisha yao mikononi mwa Mungu; wenye huzuni ndio wanaoguswa na uchungu wa wenzao; wenye upole ndio wanaoishi kwa ushirika na moyo wa Mungu; wenye njaa na kiu ya haki ndio wanaojitolea kwa kujenga jamii nzuri; wenye rehema ndio wanaoguswa na huruma ya Mungu ili wawe chombo cha huruma hii; wenye moyo safi ndio wanaoweza kumjua Mungu; wapatanishi ndio wanaosaidia uzoefu wa kindugu katika jumuiya zetu; wanaoteswa kwa ajili ya haki na kwa jina la Yesu ndio walio mashahidi wa wema wa Mungu kati yetu. Ufalme wa mbinguni ni tuzo yao.  

Sisi, tulio wafuasi wa Yesu, tunaalikwa kuchukua ujumbe wa “Heri nane” kama mpango wa maisha. Hatuhitaji njia nyingine ya kuishi kwa ajili ya kupata furaha ya kweli. Mambo yote Yesu aliyotaka kusema kwa wanaotaka kumfuata yapo hapa. Mungu anataka tuwe wenye furaha, lakini njia zake zina masharti yaliyo Heri nane yanayotualika tuweze kubadilisha njia ya kuona na ya kuishi. Hii ni njia ngumu, lakini hatuko pekee yetu. Maisha yetu yana thamani kubwa kwa Mungu. Yeye yu pamoja nasi kwa sababu hawaachi wale wanaomtumainia yeye. Jibu letu kwake ni tuweze kuishi kwa uaminifu yale aliyoishi na kufundisha Yesu. Huu ni utabiri wa wakati mpya. Ingawa ufalme upo katika Yesu, yeye mwenyewe anatambua thamani za ufalme huu duniani na katika hali ya jumuiya zetu. Neema yake ituimarishe tuwe vyombo vya thamani za ufalme huu.

Fr Ndega
marekebisho: Carlistus Mulama


Nenhum comentário: