domingo, 17 de abril de 2016

KUJITOLEA KWA AJILI YA KONDOO


Mdo 13,14.43-52; Ufu 7,9.14b-17; Yoh 10,27-30

     Tunasherehekea Jumapili ya Mchungaji mwema na Jumapili ya miito. Ni Yesu mwenyewe ambaye anajifunua kama Mchungaji aliye na uhusiano wa ndani na wafuasi wake, kumwita kila kondoo kupitia jina lake na kumjali kwa upendo. Safari ya wito ni historia ya upendo, kudhihirisha njia maalum ya Mungu ambaye anawaita watu kwa sababu anawapenda na kutarajia jibu la ukarimu kama alama ya upendo. Hii ni nafasi ya kumshukuru Mungu kwa zawadi kubwa ya miito yote na kumwomba aendelee kulibariki Kanisa lake kwa kuongezeka kwa miito. Pendekezo hili la kusali kwa ajili ya miito lilianzishwa na baba mtakatifu Paulo wa VI, katika mwaka wa elfu moja mia tisa sitini na nne, akiimarisha Kanisa zima kuchukua ahadi kwa ajili ya hali hii. Maombi kwa ajili ya miito ni pia utiifu kwa mavutio ya Yesu kwa wafuasi wake ili waombe kwa mwenyeji wa mavuno ili atume wafanyakazi mavunoni mwake kwa sababu mavuno ni makubwa, lakini wafanyakazi ni wachache (cf. Mt 10, 37-38). Wito ni zawadi ya Mungu. Huu ni utambulisho wetu wa ubatizo kwa ajili ya mahitaji ya kanisa. Kilimo cha wito huanza katika familia na yule anayealika hutarajia jibu la ukarimu daima kutoka kwa wale ambao wanaalikwa. Basi tutafakari kuhusu hali hii kupitia utajiri wa masomo ya liturujia ya siku ya leo ili tuuishi wito wetu kwa shauku na furaha.  
         Katika Somo la kwanza mitume Paulo na Barnaba waliongea na watu wakiwatia moyo ili waendelee kuishi wakitegemea neema ya Mungu. Upinzani waliokabili kutoka kwa viongozi wa wayahudi uliwafanya Paulo na Barnaba wafahamu haja ya wawe mwanga kwa mataifa ili watu wote ulimwenguni wapate wokovu. Ujumbe wa neno la Mungu hausababishi matokeo mazuri kwa wote kwa sababu sio wote wanaoupokea vizuri. Kwa wale ambao walipokea ujumbe huu kama ipasavyo wakawa wamejaa furaha na Roho Mtakatifu. Kwa upande wa mitume, muhimu ni kuchukua kazi kwa hamu na bidii, na kuruhusu kwamba wapinzani wachukue matokeo ya uamuzi wao. Katika mtazamo wake, Yohane aliona umati wa watu waliochukua ahadi ya kuwa mashahidi wa Kristo. Ingawa waliteseka sana, wanaleta ishara za ushindi wao, yaani mavazi meupe na matawi ya mitende mikononi mwao. Walipata kushinda taabu na mateso mengi kwa sababu ya nguvu iliyotoka kwa damu ya Mwana-Kondoo aliye Kristo. Uaminifu wake ni faraja na nguvu katika safari yetu.      
      Katika injili ya Yohane tuna ufunuo wa Yesu kama Mchungaji Mwema. Yeye ni Mchungaji Mwema kwa sababu anawapenda kondoo wake naye yuko tayari kufa kwa ajili yao. Anawatendea mema na anazitumia nguvu zake kwa ajili ya maisha yao. Uhusiano wa ndani kati ya Mwana na Baba ni kipimo cha uhusiano kati ya Yesu na kondoo wake. Uhuru wa Mwana ni alama ya upendo aliopokea kutoka kwa Baba. Anawalinda kondoo wake kwa sababu wanathamini sana kwake. Anashiriki nao uhai wake kwa sababu anataka waishi milele. Anajua kondoo wake kwa sababu ana uhusiano wa ndani nao. Hao wanasikiliza sauti yake na kuyafuata mafundisho yake. Hakika maneno haya yalithibitisha uhusiano ambao Yesu aliishi na wanafunzi wake tangu mwanzo, aliwaalika kuyafananisha maisha yao na njia yake ya kuishi na kujifunza jinsi ya kuwa wachungaji kama mwalimu wao. Kulingana na Yesu Kundi linahitaji wachungaji wema.

       Kupitia Yesu, Mchungaji Mwema, Mungu anaonyesha ulinzi wake kwetu kwa njia maalum. Upinzani dhidi ya sauti ya Yesu ni upinzani kwa ulinzi wa Mungu na kwa kuishi uhusiano wa ndani naye. Tunaonyesha jibu kamili kwa mwito wake kupitia tabia nzuri ya kuishi Maneno yake. Kupitia maneno haya tunaendelea kusikiliza sauti ya Yesu na kukubali ahadi kwa ajili ya kundi lake. Kundi lake ni Kanisa ambalo linahitaji miito mizuri ili liendelee kwa uaminifu kazi liliyopokea kutoka kwa Yesu. Tunaalikwa kutenda kama wanafunzi wa kwanza, ambao waliuchukua wito na kazi kwa furaha na shauku. Utambulisho upya kama wafuasi wa Yesu unatukumbusha kuhusu umuhimu wa wito tuliopokea kupitia ubatizo wetu ambao ulitufanya mapadri, manabii na wachungaji. Kwa kuishi wito wetu kwa kweli tunapaswa kushiriki katika hisia za Mchungaji Mwema ambaye analilinda na kulisha kundi lake kwa sababu anatarajia liwe na uzima wa milele.

Fr Ndega 
Mapitio na marekebisho: Sarah 

Nenhum comentário: